Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiongea na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais (TAMISEMI), Suleiman Jaffo, kwenye ofisi ya Wizara hiyo ya muda, wakati
akikagua ofisi za Wizara kwenye mji wa Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma,
Aprili 23, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akioneshwa jambo na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Suleiman Jaffo, wakati akikagua ofisi za Wizara
kwenye mji wa Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma, Aprili 23, 2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akitoka kwenye jengo la Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, wakati akikagua ofisi za Wizara kwenye mji
wa Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma, Aprili 23, 2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi, wakati akikagua ofisi za
Wizara kwenye mji wa Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma, Aprili 23,
2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua
ofisi mpya za wizara saba katika mji wa Serikali ulioko Mtumba, Dodoma na
kusisitiza waweke vibao vya ofisi na kukamilisha mazingira ya nje.
“Kuna wizara hazina majina kwa nje.
Hakikisheni majengo yote yanawekwa majina haraka ili kuondoa usumbufu kwa
wananchi wanaokuja huku kutafuta huduma. Kama kuna wizara mbili ziko jirani,
pale njia panda wekeni kibao kuonesha majina ya wizara zote mbili. Nia ya
Serikaili ni kutoa huduma zote kutokea hapa Mtumba,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumanne,
Aprili 23, 2019) wakati akitoa majumuisho ya ziara hiyo fupi kwa maafisa wa
Serikali waliokuwepo kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara ya nishati ambako
ndiko alimalizia ziara yake.
Waziri Mkuu ametembelea wizara saba
ambazo ni Maliasili na Utalii; Ofisi ya Rais - TAMISEMI; OWM - Sera, Uratibu na
Bunge; Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora; Mifugo na Uvuvi, Ulinzi na JKT
na ya mwisho ilikuwani ni Wizara ya Nishati.
“Nimefurahi kukuta Mawaziri, Naibu
wao na Makatibu Wakuu pamoja na wakuu wa idara wako huku na kazi zinaendelea,
lakini ni lazima nisisitize kwamba idara zinazohamia huku ziwe ni zile zenye
kutoa huduma za kila siku kwa wananchi,” amesema.
“Ni lazima tuwaeleze wananchi na
wadau wetu ili watambue kwamba Serikali imehamia huku, lakini wakija kutaka
huduma wasikute idara inayowahusu iko mjini au wengine wako huku na wengune
wako kule.”
Kuhusu miundombinu ya barabara, umeme
na TEHAMA, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali
kuhamia Dodoma inasimamia kazi hiyo ikiwemo suala la ujenzi wa kituo kikubwa
cha afya ambacho kitakuwa na huduma zote kwa viongozi lakini pia pia kitatoa
huduma kwa wananchi waishio vijiji vya jirani.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amewataka mawaziri walioko Mtumba wajiandae kwani kuna siku atakwenda kufanya
vikao vyake kwenye wizara zao kwa sababu amebaini kuwa kila wizara ina ukumbi
mkubwa wa mikutano.
Mapema, akitoa
taarifa kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla
alisema jumla ya watumishi 64 wameshamia kwenye ofisi za wizara hiyo ambapo
kuna vyumba 25 vya ofisi na ukumbi mmoja wa mikutano.
Pia alisema waligawa miche ya miti
13,570 kwa wizara mbalimbali na kwamba katika ofisi yake, wamepanda miti 980.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi
(OR-TAMISEMI), Bw. Suleiman Jafo alisema wamekwishahamia tangu Jumatatu
iliyopita na kwa sasa wanatumia ofisi za muda ambazo ni za mabati huku wakisimamia
ujenzi wa ghorofa yao hadi ukamilike.
Akielezea kuhusu ujenzi wa ofisi hizo
ulipofikia, Bw. Jafo alisema ifikapo mwishoni mwa wiki watakuwa wamekamilisha
kazi ya kuweka mabati na kupiga plaster. “Tunatarajia
kukamilisha kazi ya ujenzi Mei 30, kama ilivyopangwa. Jengo lilikamilika
litakuwa na kumbi mbili za mikutano na ofisi za kuchukua watumishi 88,”
alisema.
Naye Waziri wa
Nishati, Dk. Medard Kalemani alisema kuwa hadi sasa watumishi 73 kati ya 153
ndiyo wamehamia kwenye ofisi mpya za Mtumba.
Alisema kwa sasa wanatenegeza eneo la
maegesho ya magari na wameshatenga eneo la mgahawa kwa ajili ya wafanyakazi wa
wizara hiyo.
0 comments:
Post a Comment