NA MWANDIHI WETU, MTERA
SHIRIKA
la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa tahadhari kwa wananchi wa vijiji jirani na
vyanzo vya kufua umeme kwa maji vya Mtera na Kidatu kufuatia taarifa
iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuwa mvua bado zinaendelea
kunyesha na zipo juu ya wastani.
Kufuatia
taarifa hiyo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini, Meneja Mwandamizi Uzalishaji
Umeme Mhandisi John Skauki amesema wataalamu wa TANESCO wanafanya tathmini
iwapo siku za usoni maji yahamie upande wa pili kwa ajili ya usalama wa Bwawa
na mitambo.
Alisema
Wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari na kuongeza maji hayatakuwa yanasambaa
bali yatapita kwenye mkondo wake wa asili ambako wananchi wanafanya shughuli
zao za kijamii.
"TANESCO
tumeona ni muhimu leo kutoa tahadhari kwa Wananchi kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha, kwa kawaida Bwawa la Mtera kulijaza huchukua miezi 3
hadi 4 kwa mvua za masika, lakini kwa kipindi hiki mvua za vuli zimekuwa nyingi
ndani ya mwezi mmoja kina kimeongezeka", alisema Mhandisi Skauki.
Alisema
tahadhari inatolewa kwa Wananchi kusitisha shughuli zao za kijamii kama uvuvi,
kulisha mifugo, kilimo na nyingine kwenye mkondo wa maji au sehemu zenye
vidimbwi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Aliongeza
kuwa, kawaida kina cha maji kujaa ni mita 698.50 juu ya usawa bahari na
kuongeza hivi sasa kina cha maji kimefikia 698.03 juu ya usawa wa bahari.
"Ikitulazimu
tutaruhusu maji kwenda upande wa pili, hili ni zoezi la kawaida na halina
madhara yoyote kwa jamii, mara ya mwisho maji kuzidi kiwango ilikuwa mwaka 2008
zoezi lilifanyika na hakukuwa na madhara yoyote kwani maji hupita kwenye mkondo
wake wa asili", alisisitiza Mhandisi Skauki.
Aidha,
maji yatakapofika kina cha mwisho TANESCO itatolea taarifa aliongeza.
Kwa
upande wake Kaimu Meneja Uhusiano Bi. Leila Muhaji akizungumzia jinsi ambavyo
jamii inayoishi kandokando na vyanzo vya maji inahusishwa alisema, TANESCO
imekuwa ikitoa elimu kwa Wananchi hao, lakini pia kushirikiana na viongozi wa
Vijiji, Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji, Maafisa wa Uvuvi.
"Tumefika
hapa kuwatoa hofu Wananchi na hii tunayotoa ni tahadhari tuu kwa Wananchi", alisema Bi. Muhaji.
Afisa
Mtendaji Kata ya Mtera Bi. Naomi Fungulia alisema siku zote wamekuwa
wakishirikiana na TANESCO na wamekuwa wakitoa tahadhari kwa wananchi kupitia
vikao mbalimbali wanavyovifanya.
Bwawa
la Mtera lilijengwa mwaka 1988 na limekuwa likitumika kwenye uzalishaji wa
umeme kwa vituo viwili vya Mtera megawati 80 na Kidatu megawati 201. Vyanzo vya
maji vya bwawa la Mtera ni vitatu ambavyo ni Mto wa Ruaha Mkuu, Ruaha Mdogo
ambvyo vipo Mkoani Iringa na Mto Kisigo unaopata maji kutokea Mikoa ya Singida
na Dodoma.
Kwa
hivi sasa bwawa la Mtera ndio bwawa kubwa na linachangia takribani asilimia 30
ya umeme kwenye gridi ya Taifa.
Aidha,
inatarajiwa maji ya Mtera pia yatachangia kwenye ufuaji wa umeme bwawa la
Nyerere kupitia mto Kilombero, bwawa la Julius Nyerere litakuwa na uwezo wa
kufua megawati 2115 za umeme
Meneja Mwandamizi Uzalishaji
Umeme kutoka TANESCO, Mhandisi John Skauki akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la bwawa la Mtera leo Februari 7, 2020
Sehemu ya bwawa la Mtera.
Kaimu Meneja Uhusiano wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Bi. Leila Muhaji akifafanua baadhi ya mambo kwa waandishi wa habari
Meneja Mwandamizi Uzalishaji
Umeme kutoka TANESCO, Mhandisi John Skauki akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la bwawa la Mtera leo Februari 7, 2020
Eneo la bwawa la kufua umeme wa maji la Mtera
0 comments:
Post a Comment