Na Stella Kalinga, Simiyu
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC)
kutoka Mikoa ya Arusha na Geita wamewapongeza viongozi Mkoani Simiyu kwa
ubunifu waliofanya kuanzisha kambi za kitaaluma kwa ajili ya kuongeza ufaulu na
kutoa wito kwa viongozi wengine kuiga ubunifu huu ili waweze kuwasaidia
wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao.
Hayo yamesemwa na Ndg. Anna Agatha Msuya Mjumbe wa
NEC (Arusha) na Ndg. Idd Kassim Idd Mjumbe wa NEC(Geita) mara baada ya
kutembelea wanafunzi wa Kidato cha Sita mwaka 2019 walio katika kambi ya
kitaaluma inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, mara baada
ya viongozi hao kuungana na Mjumbe wa NEC kutoka Mkoa wa Simiyu, Ndg. Emmanuel
Gungu Silanga kukabidhi msaada wa chakula kwa wanafunzi hao Aprili 11, 2019.
Akizungumza mara baada ya msaada wa chakula
kukabidhiwa Ndg. Anna Agatha Msuya amesema laiti kambi hizi zingekuwa
zinafanyika katika maeneo mengi matokeo ya Mitihani hususani ya Taifa yangekuwa
mazuri zaidi ya sasa kwani zimeonekana kuusaidia mkoa wa Simiyu kupanda
kielimu.
“Nimevutiwa na ubunifu wa Simiyu kuwa na kambi za
kitaaluma, tungekuwa na matokeo mazuri kama tungekuwa na viongozi wa Serikali
wabunifu kama hapa Simiyu, naomba tulichokiona Simiyu kifanyike na mikoa
mingine; mwaka juzi walikuwa wa 26 Kitaifa, mwaka jana wakawa wa 10 na naamini
kwa kambi hii hatutaikosa Simiyu katika mikoa mitano bora” alisema Anna Agata
Msuya.
Naye Ndg. Idd Kassim Idd Mjumbe wa NEC(Geita)
pamoja na kupongeza juhudi za mkoa wa Simiyu katika elimu, ameahidi kuwa
amejifunza kupitia kambi hiyo ya kitaaluma na kulichukua wazo hilo kwa jili ya
kushauri viongozi wa mkoa wa Geita kuona namna ya kulifanyia kazi ili kuwa na
ufaulu mzuri.
Aidha, Mwl. Ezekiel Mollel mwekezaji katika Sekta
ya Elimu amesema suala la kambi za kitaaluma ni la kipekee kwa mkoa wa Simiyu,
hivyo akatoa wito kwa mikoa mingine kuiga huku akiwaomba wadau mbalimbali wa
elimu kuendelea kuchangia mahitaji mbalimbali ya wanafunzi walio katika kambi
ili waweze kujifunza kwa amani wakiwa na mahitaji ya msingi.
Kwa upande wake Mjumbe wa NEC kutoka Mkoa wa
Simiyu, Ndg. Emmanuel Gungu Silanga amesema ametimiza ahadi yake ya kutoa kilo
1000 za mchele na kilo 400 za maharage kwa wanafunzi wa kidato cha Sita na
kueleza matarajiao ya wana Simiyu kwa wanafunzi hao kuwa, ni kuwaona wanasoma
kwa bidii na hatimaye waifanye Simiyu kuwa ya kwanza Kitaifa mwaka 2019.
Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi
wenzao wa kidato cha Sita mwaka 2019 walioko kambini Hidaya Simba(Maswa Girls)
na Masanja Ng’hwenu (Meatu) wamewashukuru viongozi hao kwa msaada wa chakula
walioutoa na kuahidi kuwa shukrani yao kubwa kwa walimu, viongozi, wazazi na
wadau wa elimu wanaowasaidia ni kufanya vizuri na kuifanya Simiyu iwe nambari
moja.
Pamoja na kilo 1000 za mchele na kilo
400 za maharage zilizotolewa na Mjumbe wa NEC (Simiyu),
Ndg. Emmanuel Gungu Silanga, Ndg. Idd Kassim Idd Mjumbe wa NEC(Geita) ametoa
kilo 200 za mchele, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Simiyu ametoa kilo 100, Mdau wa
Elimu Ezekiel Mollel kilo 50 na Ndg. Anna Agatha Msuya Mjumbe wa NEC (Arusha)
ameahidi kutoa zawadi kwa wanafunzi watakaopata daraja la kwanza(divion one)
MWISHO
0 comments:
Post a Comment