
***************************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli
itaendelea kuhakikisha kuwa kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa
na wenye tija kwa wananchi sambamba na kutoa mchango unaostahili katika
kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Katika kuhakikisha azma hiyo
ya Serikali inafikiwa, nitoerai kwa wafugaji nchini kuunda ushirika
imara utakao wawezesha kupata huduma mbalimbali za mifugo na ushirika
huo pia ulenge katika kuboresha uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa,
upatikanaji wa masoko pamoja na kuongeza kiasi cha usindikaji
viwandani.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumatano, Septemba 25, 2019)kwenye Maadhimisho ya Siku ya Unywaji
Maziwa Shuleni yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwembetogwa
mijini Iringa. “Unywaji maziwa shuleni si tu ni muhimu lakini pia inatoa
msukumo wa kuboresha afya zetu hususan za watoto shuleni kupitia
unywaji wa maziwa.”
Amesema wataalamu wa lishe
wanashauri kula chakula bora kinachokuwa na viini lishe vyote muhimu
kama wanga, protini, vitamini, madini, mafuta na maji ya kutosha. Hata
hivyo, ili kupata chakula bora, wananchi wanapaswa kuchanganya vyakula
vya aina nyingi katika mlo mmoja.
Waziri Mkuu amesema kutokana
na umuhimu huo, ndiyo maana watalaamu wa lishe wanashauri kuwa mtoto
apate glasi moja ya maziwa katikati ya siku itakayompatia lishe ya
kutosha hadi atakapomaliza masomo yake kwa siku hiyo. “Kwa bahati mbaya
hapa nchini, watoto wengi huondoka asubuhi kwenda shuleni bila kupata
chakula chochote. Aidha, shuleni nako mara nyingi hawapati chakula na
hivyo hukosa usikivu mzuri katika masomo yao.”
Zaidi ya nchi 70 duniani
ikiwemo Tanzania zinaadhimisha siku ya unywaji maziwa na tayari
zilishaanzisha mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa watoto wao, lengo ni
kuhakikisha mtoto anapata lishe kamili na anakuwa na usikivu mzuri
katika masomo yake. Mtoto amelengwa kwa sababu ni kundi ambalo ni muhimu
katika kujenga Taifa lililo bora na anatarajiwa kurithisha vema vizazi
vijavyo.
“Nimearifiwa kuwa hapa nchini
programu ya unywaji maziwa shuleni ilianza kutekelezwa katika mikoa ya
Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Iringa, Dar es Salaam na Njombe
ambapo shule 40 na wanafunzi 34,561wamenufaika katika kunywa maziwa lita
631,860 ambayo yamekuwa yakitolewa kwa ushirikiano na Serikali, wazazi,
wafadhili mbalimbali na wasindikaji wa maziwa. Lengo kuwafikia
wanafunzi wote.”
Waziri Mkuu amesema Serikali
ina nia ya dhati ya kufanya mpango huu uwe wa kitaifa. Serikali kupitia
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na wadau wengine itaendelea
kuhamasisha unywaji wa maziwa katika shule zetu hapa nchini. Juhudi
hizi zitakwenda sambamba na kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka
lita bilioni 2.7 zinazozalishwa sasa kwa mwaka mpaka lita bilioni saba
kwa mwaka ifikapo 2020.
Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kuwapongeza wafugaji wa Iringa kwa kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa
mafanikio yanayoonekana katika kuendeleza tasnia ya maziwa kupitia
ushirika. “Nitoe wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha
zinawezesha na zinasimamia uundwaji wa vyama vya ushirika imara na pia
kuimarisha vyama vya ushirika vilivyopo.”
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa
na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Josephat Kandege, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Maafisa wa Serikali, wadau wa mazima pamoja na wananchi.
0 comments:
Post a Comment