
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitembelea kiwanda cha maziwa cha ASAS cha mjini Iringa akiwa katika
ziara ya kikazi mkoani humo Septemba 25, 2019. Kushoto ni Mkurugenzi
Mtendaji wa kiwanda hicho, Fuad Abri
…………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli itaendelea kudhibiti uingizwaji wa bidhaa mbalimbali kutoka nje
ili kulinda viwanda vya ndani.
Ameyasema hayo leo (Jumatano,
Septemba 25, 2019) alipotembelea kiwanda cha maziwa cha Asas, akiwa
katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa. Amesema Serikali imedhamiria
kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kupitia sekta ya
viwanda.
Waziri Mkuu amesema Serikali
inaamini kuwa uchumi wa viwanda ukiimarika uchumi utakuwa kwa kasi kubwa
na matokeo yake yataonekana wazi kwa kupanua wigo wa ajira, soko la
huduma na shughuli nyingine za kiuchumi.
“Serikali imefanya mageuzi
makubwa kwenye sekta ya mifugo ili kuhakikisha inaleta tija kwa wafugaji
na taifa kwa ujumla, hivyo wafugaji endeleeni kuimarisha ushirika wenu.
Wizara ya Mifugo iendelee kuwaelimisha wafugaji ili wafuge kitaalamu.”
Waziri Mkuu ameipongeza kampuni
ya Asas kwa sababu ni miongoni mwa kampuni chache ambayo imeanza kutoa
elimu kwa wafugaji juu ya namna bora ya ufugaji ikiwa ni pamoja na
kufuata kanuni bora za ufugaji wa kisasa pamoja na kuwapa uhakika wa
soko.
Amesema Serikali inathamini sana
uwekezaji uliofanywa na kampuni ya Asas kwa sababu wameitikia wito wa
Serikali wa ujenzi wa uchumi kupitia sekta ya viwanda, hivyo
itahakikisha wawekezaji wote wananufaika na uwekezaji wao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kiwanda cha Maziwa cha Asas, Fuad Abri amesema kiwanda chao
kinampango wa kupanua uzalishaji kwa kujenga kiwanda kingine cha
kusindika maziwa katika wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na kipo katika
hatua za mwisho kukamilika.
Awali,Waziri Mkuu alizindua
kiwanda cha maji cha Mkwawa cha mjini Iringa na kusema kuwa ujenzi huo
ni njia ya uhakika ya kupunguza tatizo la ajira na kwamba itaendelea
kushawishi wawekezaji wa ndani na nje ili wananchi wengi wapate ajira.
“Serikali imetoa wito kwa
wawekezaji wawekeze katika viwanda mbalimbali nchini, hivyo ni muhimu
wawekezaji hao wakalindwa na wasibugudhiwe ili waweze kuendelea na
uzalishaji wa bidhaa zao. Watumishi mlioajiriwa fanyeni kazi kwa
uaminifu.”
Naye,Mkurugenzi na Mwenyekiti wa
Bodi ya kiwanda cha Maji cha Mkwawa,Ahmed Huwel alisema kiwanda chao
kilianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kuzalisha na kufanya biashara ya
maji safi na salama pamoja na kuunga mkono mkakati wa Serikali wa ujenzi
wa uchumi wa viwanda.
Alisema kiwanda chao kimeajiri
watumishi158 kati yao wanaotoka nje ya nchi ni watatu tu na kwa upande
wa ajira zisizo rasmi ni zaidi ya 3,000 na kwamba wanatarajia kuongeza
ajira kwa wananchi wengi zaidi baada ya kukamilisha ujenzi wa kiwanda
kingine cha kutengeneza vinywaji baridi.
Akizungumzia kuhusu changamoto
zinazokikabili kiwanda hicho alisema ni pamoja na ukatikaji wa umeme wa
mara kwa mara hali inayosababisha kuharibika kwa baadhi ya mitambo hivyo
ameiomba Serikali iwasaidie.
0 comments:
Post a Comment