Tito Mselem
Waziri wa Madini Doto
Biteko amewamwagia sifa Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini ya Tanzanite mkoani
Manyara kwa kuongeza mchango wao kwenye pato la Taifa.
Biteko ametoa pongezi
hizo leo wakati wa Mkutano baina ya wachimbaji na wafanyabiashara hao pamoja na
viongozi wa Wizara ya madini na Tume ya madini uliofanyika wilayani
Sumanjiro, mkoani Manyara.
Miaka iliyopita
tulikuwa tunakusanya milioni 60 hadi milioni 70 kwa mwaka lakini tokea tumeujenga
ukuta huu, mapato yameongezeka mpaka kufikia makusanyo ya billion 2.1 kwa mwaka
ambapo ni ongezeko kubwa sana hivyo nawashukuru sana watu wote wanaofanya
shughuli zao hapa Mirerani.
Biteko aliongeza kuwa,
ameamua kufanya mkutano huo akiambatana na viongozi waandamizi wa wizara ya
Madini pamoja na Tume ya Madini ili nao pia wasikie maagizo ninayotoa na waanze
kuyafanyia kazi badala ya kurudi na kuitisha kikao kingine ofisini.
Akizungumza manufaa ya
ukuta huo kwa wakazi wa Mirerani, Biteko alisema ukuta uliojengwa hapo umeleta
manufaa makubwa kwa Serikali na kwa jamii kwa ujumla sababu watu hawatoroshi
madini tena na hivyo kupelekea ongezeko la mapato mpaka kufikia bilioni 2.1.
Aidha, Waziri Biteko,
amebainisha kwamba, bei ya Madini ya Tanzanite imepanda katika soko la dunia,
na hiyo inatokana na udhibiti mzuri uliowekwa na Serikali ya awamu ya Tano.
Amekiri kuwa kwa sasa
watu hawatoroshi madini hivyo madini hayo yamekuwa bidhaa adimu katika soko la
dunia hivyo kupelekea bei kupanda.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila, amewataka wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite mkoani Manyara kufuata utaratibu na sheria
zilizowekwa na Serikali, na pia kutoa taarifa sahihi kwa Serikali.
Aidha, Profesa
Masanjila, ameiagiza Tume ya Madini iongeze watumishi wa kutathimini madini ya
Tanzanite ili kazi ziende kwa haraka na uhakika.
0 comments:
Post a Comment