Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Menejimenti ya PSSSF, katika jengo la ofisi hiyo, jijini Dodoma Aprili 18, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Menejimenti ya PSSSF, katika jengo la ofisi hiyo, jijini Dodoma Aprili 18, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameitaka menejimenti ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi
wa Umma (PSSSF) ijizatiti na kuweka mbinu mpya za kuongeza makusanyo.
Ametoa agizo
hilo leo jioni (Alhamisi, Aprili 18, 2019) wakati alipokutana na menejimenti ya
mfuko huo kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini
Dodoma.
Waziri Mkuu
ambaye aliamua kutembelea ofisi za mfuko huo ili afahamiane na menejimenti
hiyo, amesema amepokea taarifa ya Mkurugenzi Mkuu na kubaini kuwa ukusanyaji wa
michango hauridhishi.
“Mfuko huu ni
wa tofauti na wa NSSF kwa sababu umeunganisha mifuko mingine ya GEPF, PSPF,
LAPF na PPF. Mifuko yote hii ilikuwa na malengo na majukumu yake ya awali,
lakini sasa imeunganishwa kwa hiyo jukumu letu ni moja,” amesema.
“Natambua mna
kazi kubwa ya kusajili wanachama wapya lakini pia tunayo kazi ya kuwafikia
wanachama wa zamani ambao tumewachukua kutoka mifuko mingine na kuhakikisha
kuwa wanaingizwa katika mfuko mpya,” amesisitiza.
“Napenda
kusisitiza kuwa jukumu la kukusanya michango ni la muhimu sana. Ni lazima mjue
wastani wa makusanyo kwa mwezi ni kiasi gani, na kama zimepungua, ni kwa kiasi
gani na pia mtafute ni kwa nini zimepungua,” amesema.
Ameitaka
menejimenti hiyo pia ijiridhishe juu ya uhakiki wa mali walizorithi kutoka
mifuko mingine na izitambue ziko katika hali gani. “Menejimenti peke yenu
hamuwezi kufuatilia mali zote, kwa hiyo wapeni hiyo kazi wajumbe wa Bodi,
wagawane maeneo ili waende kuzitathmini hizo mali na kisha nipate hiyo
taarifa,” amesema.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya utendaji wa mfuko huo kuanzia Agosti Mosi
2018 hadi Machi 31, 2019, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Hosea Kashimba
alimweleza Waziri Mkuu kwamba majukumu makuu wa mfuko huo ni kusajili
wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao kwa wanachama.
Alisema baada
ya kuunganishwa kwa mifuko, uandikishwaji wa wanachama uliendelea ambapo hadi
kufikia Machi 2019, jumla ya wanachama wapya 7,575 walikuwa wamesajiliwa.
“Hapo awali
mfuko ulikuwa na wanachama 962,871. Kati ya hao, wanachama 279,564 wanatoka
sekta binafsi ambao wamehamishiwa NSSF. Hadi kufikia Machi 31, 2019, mfuko
ulikuwa na jumla ya wanachama 750,943 ambao ni watumishi wa umma ikijumuisha na
wanachama 67,636 waliohamia kutoka NSSF,” alisema.
Kuhusu
ukusanyaji wa michango, Bw. Kashimba alisema moja ya jukumu la mfuko ni
kukusanya michango na tangu Agosti 2018 hadi Machi 2019, mfuko huo ulikuwa
umekusanya jumla ya sh. bilioni 928.31 ikilinganishwa na lengo la lililowekwa
la kukusanya sh. trilioni 1.05 sawa na asilimia 88.62.
Kuhusu malipo
ya mafao, Bw. Kashimba alisema katika kipindi kilichoishia Machi 31, 2019,
mfuko huo umelipa mafao ya jumla ya sh. trilioni 1.65.
Alisema mfuko
huo hivi sasa una wafanyakazi 839 ambao kati yao, wanaume ni 470 na wanawake ni
369.
Kikao hicho
kilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, (OWM – Sera, Uratibu, Bunge na wenye
Ulemavu), Bibi Jenista Mhagama.
0 comments:
Post a Comment