Ø Naibu Waziri Nyongo ataka Soko la Madini Arusha
kuanzishwa haraka
Waziri
wa Madini Doto Biteko amesema Serikali kupitia Wizara yake inalenga kurahisisha
Mazingira ya Biashara ya Madini ikiwemo kuwalea wachimbaji na kuwataka
wafanyabiashara na wachimbaji kuhakikisha wanajisimamia wenyewe kwa manufaa yao
na Taifa.
Waziri
Biteko ameyasema hayo alipokutana na viongozi wa Chama Cha Wafanyabiashara wa
Madini Tanzania (TAMIDA), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Sam Mollel
ofisini kwake jijini Dodoma Aprili 10, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali
yanayohusu biashara ya madini nchini.
Amekitaka
chama hicho kuendelea kushirikiana na wizara kwa lengo la kusukuma mbele Sekta
ya Madini ikiwemo kuhakikisha biashara ya madini inafanyika katika mazingira
yenye kuzinufaisha pande zote na kuwasisitiza viongozi hao kuhakikisha
wanachama wao wanafuata taratibu wanapofanya biashara ya madini.
Awali,
kabla ya kujibu hoja zilizowasilishwa na chama hicho, Waziri Biteko
amekipongeza chama hicho kwa kuwa kimekuwa kikitoa njia mbadala
pindi kinapowasilisha changamoto na kero zake badala ya kuishia kulalamika na kuongeza,
“wizara inaona fahari kwa hilo na tunayachukulia kwa umuhimu maoni yenu,”.
Akizungumzia
suala la kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya zuio ambayo imeondolewa kwenye
uchimbaji mdogo, Waziri Biteko amekitaka Chama hicho kutoa nafasi kwa serikali
kufuatilia suala hilo. Waziri Biteko ameleeza hilo kufuatia hoja
iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel ambaye ameeleza kuwa, katika
mkoa wa Arusha, kodi hiyo bado inatozwa licha ya serikali kuiondoa.
Aidha,
Waziri Biteko ametolea ufafanuzi wa changamoto kadhaa zilizowasilishwa na
Mwenyekiti Sam Mollel kwa niaba ya chama hicho ikiwemo. Kuhusu bei elekezi,
Waziri Biteko amesema wizara itaendelea
kushirikiana na wadau kuhakikisha suala hilo linakuwa shirikishi. Waziri Biteko
amesema hilo baada ya TAMIDA kutoa pongezi kwa serikali kwa kutoa nafasi kwa
wadau kukaa pamoja na serikali kujadili suala la bei elekezi ambapo Mwenyekiti
huyo amemweleza Waziri Biteko kuwa, katika hilo, serikali na wadau wameanza
vizuri.
Akitolea
ufafanuzi kuhusu suala la kurejesha maonesho ya madini jijini Arusha, Waziri
Biteko amesema suala la maonesho ya madini kufanyika arusha inawezekana lakini
si kwa madini ya Tanzanite, na kuongeza kuwa, serikali imedhamiria kufanya
shughuli zote zinazohusu madini hayo ndani ya ukuta unaozunguka machimbo ya
mirerani lakini pia ikilenga kuubadilisha
mji wa mirerani ufanane na madini
hayo.
Aidha,
Waziri Biteko amezungumzia suala la kuongeza wataalam wa kuthamini madini ya
Tanzanite Mirerani na kueleza kuwa, kutokana na unyeti na umuhimu wa suala
hilo, tayari serikali imeanza kulifanyia kazi ili kuhakikisha inaongeza idadi
ya wataalam kuwezesha shughuli za uthamini Mirerani, kufanyika kwa wakati.
Ufafanuzi huo umetolewa baada ya Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel kuwasilisha
changamoto ya kuwepo na upungufu wa
wataalam hao.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza katika kikao
hicho, ametaka kuanzishwa haraka kwa soko la Madini jijini Arusha na kueleza
kuwa, kwa upande wa wizara itahakikisha inashirikiana na serikali ya mkoa
kuhakikisha soko hilo linaanzishwa haraka.
Naibu Waziri Nyongo amesema hayo
akijibu hoja ya Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel ambaye ameleeza katika kikao
hicho kuwa, Chama hicho kinaunga mkono Serikali kuhusu uanzishwaji wa masoko ya
madini na kuitaka serikali ione umuhimu wa kuanzisha soko La madini la madini mkoani
arusha kuwezesha biashara ya madini ya vito kufanyika kwa urahisi.
Kuhusu
vibali vya Wataalam wa masuala ya ukataji na unga’rishaji wa madini kutoka nje
ya nchi, Naibu Waziri Nyongo amesema kuwa, ni kweli kwamba serikali inawahitaji
wataalam hao kwa kuwa pia watawezesha kutoa ujuzi huo kwa wataalam wa ndani ili
kuhamasisha viwanda vya ukataji madini na kuongeza, “ serikali inaangalia namna
ya kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika kwa
sababu pia tunataka watu wetu wanufaike na utaalam huo”,.
Pia,
ameongeza kuwa, kutokana na kulichukulia suala la uongezaji thamani madini kwa
umuhimu, inakitegemea kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kwa ajili ya kuzalisha
wataalam na kukitaka chama hicho kusaidia kuongeza idadi ya wanafunzi
wanaodahiliwa katika kituo hicho kwa kuwa hivi sasa idadi bado ni ndogo.
Kikao
hicho cha Waziri na TAMIDA ni cha kwanza tangu kuteuliwa kwa Waziri wa Madini
Doto Biteko kuiongoza wizara husika.
Wengine
waliohudhuria kikao hicho ni Viongozi Waandamizi kutoka wizara ya Madini na
Tume ya Madini.
0 comments:
Post a Comment