Na Issa Mtuwa- Ulanga Morogoro
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof.
Idris Kikula amewataka Watumishi wa tume
hiyo ofisi ya Morogoro na Ulanga kutambua kwamba agizo la Waziri linalowataka
kufuta leseni zisizofuata utaratibu wa kisheria sio la kujadili bali ni
kutekeleza.
Prof. Kikula ameyasema hayo Aprili 10,
2019 wilayani Ulanga wakati akizungumza na watumishi wa tume hiyo wakati wa
ziara yake.
Taarifa iliyosomwa kwake na Afisa
Migodi Mkazi ofisi ya Mahenge Ulanga, Tandu Jilabi inaonyesha kuwa wilaya ya Ulanga
ina leseni za wachimbaji wadogo 221 kati ya hizo ni leseni 9 tu ndio zinazofanya
kazi huku leseni za uchimbaji wa kati zikiwa 5 na leseni za utafiti wa madini
13.
Kufuatia hali hiyo, Afisa Migodi Mkazi ofisi
ya Mahenge ameiomba tume ya madini kufuta leseni zisizofanya kazi ili wapewe
wenye uhitaji ili waweze kuziendeleza. Kufuatia ombi hilo, Mwenyekiti wa tume
amesema jukumu la kuzifuta leseni hizo ni la kwake pamoja na Afisa Madini Mkazi
Morogoro na halina mjadala kwakuwa muongozo wa utekeleza wa suala hilo
ulishatolewa na waziri wa Madini.
“Suala la leseni zisizofanya kazi sio
la kujadili, hili ni agizo la Waziri na kazi yetu ni kutekeleza na wenye
kuzifuta ni ninyi, fuateni taratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria katika
kuzifuta na sio kuzifuta lazima wote waliozishikilia leseni hizo kwa muda wote
walipe fidia na wasipo fanya hivyo taratibu za kisheria zifuatwe kwani katika
kipindi hicho chote serikali imekosa mapato yake. Kuanzia leo pitieni leseni
zote na ifikapo Juni 30 mwaka huu leseni zote zisizo hai ziwe zimefutwa”, amesema
Prof. Kikula.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa tume
amekutana na kuzungumza mwakilishi wa mwekezaji wa kampuni ya TanzGraphite (T)
Ltd ambae ni Meneja Uhusiano wa Jamii na kuzungumzia kuhusu mgogoro uliopo
baina ya mwekezaji huyo na baadhi ya wananchi wanaotakiwa kufanyiwa tathimini
ili kupisha shuguli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo.
Prof. Kikula ameonyesha kusikitishwa
na mgogoro huo ambao amesema ni wa muda mrefu sasa na unachelewesha maendeleo
ya watu na kuikosesha serikali mapato.
Ameongeza kimsingi wananchi wanapaswa
kuelewa kuwa “right surface” (haki ya
kumiliki vitu vilivyo juu ya ardhi) inampa mwananchi haki ya kulipwa fidia ya mali zilizo juu ya ardhi anayo
miliki lakini watambue kuwa kuna “resource
right” (haki ya kumiliki raslimali zilizo chini ya ardhi) ikiwemo madini
ambayo mmiliki wake ni serikali, ndio maana inapohitaji raslimali hizo
humuondoa na kumfidia mliliki wa mali za juu ya ardhi, hivyo wananchi wanapo ng’ang’ania
wanatakiwa walitambue hilo.
Pia, amesema kuwa, kwa mpango ulioanishwa
na mwekezaji huyo unaonyesha manufaa kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo
(CSR) ambapo amebainisha kuwa mwekezaji ameahidi kuwalipa fidia, kuwajengea
nyumba za kisasa wale wote walio ndani ya eneo.
Mambo mengine ni pamoja na kuwapatia
chakula kwa muda wa miaka miwili wakiwa kwenye makazi mapya watakayo jengewa na
kila kaya kusomesha mtoto mmoja kwenye vyuo vya veta na wakihitimu wataajiriwa na
mgodi ili waweze kupata kipato cha kusaidia na kuendeleza kaya zao.
Pamoja na hayo, mwekezaji huyo
amemweleza mwenyekiti wa tume kuwa tayari wameshakubaliana kujengaa kituo cha
afya, matundu ya vyoo kwa baadhi ya shule, kujenga shule na ukarabati wa vyumba
vya madarasa katika shule mbalimbali.
Hata hivyo hakusita kuonyesha
kusikitishwa kwake na watu wachache wanaogoma kuondoka kupisha shuguli za
uchimbaji huku kila kitu ikiwemo mtaji wa shuguli hizo ukiwa tayari.
Katika mgogoro huo, kaya 347
zinatakiwa kuondoka kupisha mwekezaji huyo na kati ya hizo kaya 62 ndio zinazo
goma kuondoka ili mwekezaji aanze kazi ya uchimbaji. Mwenyekiti amesikitishwa
na hali hiyo na na kuuomba uongozi wa mkoa na wilaya kuzungumza na kaya hizo
sambamba na Baba Askofu aliyeko ndani ya eneo hilo ili mradi huo uanze kwani ni
wa muda mrefu na serikali inakosa mapato.
Amesema kwa sasa anaziachia juhudi za
serikali ya mkoa na wilaya katika kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Mapema mwenyekiti alikutana na kufanya
mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngolo Malenya ambapo amemshukuru kwa
ushirikiano anao utoa kwa viongozi na wafanyakazi wa tume ya madini wilaya ya Ulanga.
Amesisitiza suala la uadilifu kwa
wafanyakazi wa tume na amesema hilo litakuwa jambo la kwanza kulisema kila
aendapo sambamba na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.
Aidha, amesema kipimo kikubwa cha kila mkuu wa
kituo cha tume ya madini kitakuwa ni ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika Mwaka
wa Fedha 2018/2019 tume ilipangiwa kukusanya Bilioni 310 na mwaka wa fedha ujao
tume imepangiwa kukusanya Bilioni 467.
Upande wake, Kamishna wa tume hiyo Dkt.
Athanas Macheyeki amewakumbusha na kuwasisitiza watumishi wa tume na wachimbaji
wa madini kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji na ulipaji wa tozo na stahiki zote
za serikali kwa wakati.
Amesema kwa kufanya hivyo raslimali za
madini zitakuwa na tija kwa taifa kama anavyo sisitiza Rais John Pombe Magufuli
kuwa anataka raslimali za madini ziwanufaishe watanzania wote na namna za
kuwanufaisha ni kulipa stahiki za serikali zinazo tokana na madini ili zikatumike
kujenga uchumi wa taifa.
Prof. Kikula na Dkt. Macheyeki wanaendelea
na ziara yao mkoani Morogoro kukagua shuguli za Tume katika Wilaya mbalimbali ambapo
leo walitembelea eneo la wachimbaaji wadogo ipanko wilayani ulanga.
0 comments:
Post a Comment