METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 21, 2019

ZOEZI LA USAJILI HALINA GHARAMA KWA MKULIMA – MHE HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu mafanikio ya changamoto za Wizara ya Kilimo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One Stereo Mikocheni Jijini Dar es salaam, leo tarehe 21 Machi 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akihojiwa kwenye kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One Stereo kuhusu mafanikio ya changamoto za Wizara ya Kilimo, Mikocheni Jijini Dar es salaam, leo tarehe 21 Machi 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Tangu serikali kutangaza mchakato wa kuanza kuwasajili wakulima wote nchini kumekuwa na mapokeo tofauti tofauti kwa wakulima na jamii kwa ujumla kwa kuogopa gharama za uandikishwaji.

Kufuatia sintofahamu hiyo serikali imewatoa hofu wakulima nchini kuwa hakutakuwa na gharama ya aina yoyote itakayomuhusisha mkulima wakati wote wa zoezi la usajili.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 21 Machi 2019 wakati akizungumza kwenye kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One Stereo Mikocheni Jijini Dar es salaam kilichokuwa kinajadili changamoto na mafanikio ya Wizara ya Kilimo.

Ni hivi karibuni tu Waziri Hasunga aliziagiza Bodi zote zilizoko chini ya Wizara ya Kilimo kuanza mara moja usajili wa wakulima wa mazao yote na kuhakikisha kuwa zinawapa vitambulisho kwa ajili ya kuwatambua na wanapofanyika kazi zao ili iwe rahisi kuwahuduma.

Akizungumza katika kipindi hicho cha Radio One Waziri Hasunga alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwatambua na kuwasaidia wakulima kuboresha kilimo chao ili waweze kupata huduma za uhakika  kwa ajili ya manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Alisema hatua hiyo inalenga kuwatambua wakulima wote na maeneo ambayo wanalima ili kuwaondoa na kilimo cha kujikimu na kuelekea katika kilimo cha kibiashara na kisasa.

 “Lazima tuanze kuwatambua wakulima wetu walipo, mashamba wanayolima na ukubwa wake na mazao wanayolima na kiwango mazao ambacho wanatarajia kuzalisha ” alisisitiza. Na kuongeza kuwa ni lazima shughuli za kilimo zianzie kutambulika kama zilivyo taaluma nyingine.

Alisema kukosekana kwa takwimu halisi za wakulima , ukubwa wa mashamba yao na walipo kumesababisha kuwa vigumu huduma muhimu kwa ajili ya kuboresha kilimo kuwafikia na kusababisha wapatiwe huduma za kitaaalamiu ambao halizingani na mahitaji yao na wakati mwingine sio halisi.

Waziri hiyo wa Kilimo aliongeza kuwa nguvu kubwa lazima ielekezwe katika kuwasaidia wakulima kulima cha kisasa kwa sababu ndicho kinatoa ajira kubwa kwa Watanzania ambapo asilimia 65 ya wananchi wamejiari katika kilimo na asilimia 8 wanashughulika na biashara inayotokana na mazao ya kilimo.

Kadhalika, alisema kuwa kwa ujumla Wizara ya Kilimo ina mikakati kabambe ya kuimarisha sekta ya mbegu, upatikanaji wa mbolea kwa wakati, upatikanaji wa Viuatilifu sahihi sambamba na kutafuta masoko ya mazao yote ya wakulima nchini.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com