METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 20, 2019

BODI YA KOROSHO KUUNDWA UPYA - MHE HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha ubanguaji korosho cha Micronix kilichopo Wilayani Newala wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji mkoani Mtwara. Juzi 19 Machi 2019. (Picha Zote Na Mathias  Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu malipo ya wakulima wakati akizungumza na wananchi katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba wakati wa ziara ya kikazi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji mkoani Mtwara. Juzi 19 Machi 2019. 
Wakazi wa Wilaya ya Tandahimba wakimlaki Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) mara baada ya kuzuru Wilayani humo akiwa katika ziara ya kikazi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji mkoani Mtwara. Juzi 19 Machi 2019. 
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ikikagua kiwanda cha ubanguaji korosho cha Micronix kilichopo Wilayani Newala wakati wakiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Mtwara. Juzi 19 Machi 2019. 
Sehemu ya wananchi Wilayani Newala wakifatilia mkutano wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati wakiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara. Juzi 19 Machi 2019. 

Na Mathias Canal, Waziri wa Kilimo-Mtwara

Mwezi Octoba mwaka 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli aliivunja rasmi Bodi ya Korosho nchini huku Mkurugenzi Mkuu akiondoshwa pia kutokana na mwenendo hafifu kwenye biashara ya zao hilo.

Maamuzi hayo ya Rais yalitangazwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa akiwa katika kikao na wakuu wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo kikao hicho kililenga kujadili hatua ya mgomo wa wakulima wa korosho juu ya kushuka kwa bei ya zao hilo ukilinganisha na miaka miwili iliyopita yaani 2016/2017 na 2017/2018.

Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ametangaza maamuzi ya serikali kuwa imejipanga kuiunda upya Bodi hiyo ya Korosho ili iendelee na majukumu yake ya kulisisimamia zao hilo kwa ufanisi.

Mhe Hasunga ametangaza maamuzi hayo ya serikali Tarehe 20 Machi 2019 wakati akijibu hoja za wakulima mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati ikiwa katika ziara ya kikazi kwenye Mkoa wa Lindi na Mtwara.

“Tumechakata vya kutosha kuhusu mustakabali wa zao la Korosho na sasa tumedhamiria kama serikali kuiunda upya Bodi ya Korosho ambayo itatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo”  Alisisitiza Mhe Waziri wa Kilimo wakati akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wakulima wa Korosho Wilayani Tandahimba

Katika mkutano huo pia Waziri Hasunga alieleza kuwa mara baada ya kukamilika kwa malipo ya wakulima Machi 31 mwaka huu Wizara ya Kilimo itapitia upya mfumo ulioutumika kuwalipa wakulima wa korosho ili kubaini kama kuna mapungufu iyaweze kuboreshwa ama vinginevyo.

Alieleza kuwa serikali ina kusudio la kuimarisha na kujenga viwanda vya kubangua korosho ili kuanzia msimu ujao korosho zote za wakulima ziweze kubanguliwa nchini.

“Tukifanikiwa katika uwekezaji wa viwanda na korosho zote tukazibangua wenyewe tutakuwa tumefanikiwa kuongeza ajira za wananchi wetu sambamba na kuongeza thamani ya zao la korosho ndani na nje ya nchi” Alisema

Kadhalika, Waziri wa Kilimo ameeleza kusudio la serikali kufanya mapitio ya sheria ya korosho kubaini mapungufu yaliyopo na kuirekebisha upya.

Katika hatua nyingine Mhe Hasunga aliieleza kamati hiyo kuwa wizara ya kilimo inaendelea na mkakati wake wa kuwasajili wakulima wote nchini ili kujiimarisha, kuwatambua na kuongeza tija katika kuwahudumia.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com