METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, February 18, 2019

Serikali imejipanga kukabiliana na uagizaji wa mafuta nje ya nchi -Mhe Mgumba

Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akipanda mti wa mchikichi ikiwa ni ishara ya kuzindua upanuzi wa shamba la zao hilo katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Bulombora wilayani Uvinza, Februari 17, 2019. Wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa yenye lengo la kuhamasisha  ufufuaji wa zao la michikichi. 
Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa akisisitiza jambomara baada ya kukagua shamba la mikungu ya mchikichi iliyochavushwa kitalaam ili kupata mbegu bora wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mikungu ya mchikichi iliyochavushwa kitalaam ili kupata mbegu bora wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019. 


Na Mathias Canal, wizara ya Kilimo-Kigoma
Serikali imeeleza dhamira yake ya kukabiliana na uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi kwa kuanzisha mashamba ya michikichi ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mafuta na uimarishaji wa sekta ya kilimo cha mazao hayo kwa wananchi.
Tayari Wizara ya Kilimo imetenga zaidi ya Bilioni 10 kwa ajili ya kuendeleza zao hilo katika Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine nchini yenye uwezo wa kuzalisha zao hilo katika mwaka wa fedha ujao.
Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 17 Februari 2019 wakati akieleza namna wizara yake ilivyojipanga kuimarisha zao la Michikichi wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) Mkoani Kigoma.
“Mhe Waziri Mkuu tusingeweza kusubiri hadi mwezi wa saba kwa ajili ya kupitisha bajeti badala yake tayari tumetumia mbinu zingine kwa kutumia fedha za matumizi ya kawaida (OC) kwa ajili ya kuanza kutekeleza adhma ya serikali ya kuendeleza zao la Michikichi na kumaliza zao la mafuta” Alikaririwa Mhe Mgumba
Alisema kuwa tayari Wizara ya Kilimo imepeleka watumishi wawili Mkoani Kigoma waliobobea katika utafiti wa Michikichi katika Taasisi ya utafiti wa Kilimo TARI-Kihinga huku wengine 10 wakiwa mbioni kuwasili mkoani Kigoma tayari kwa kuanza kazi hiyo.
Pia alisema kuwa Kituo cha Utafiti wa Michikichi TARI-Kihinga sio kituo kidogo tena badala yake kitakuwa kituo kikuu cha Utafiti wa zao hilo nchini huku vituo vingine vyote vya utafiti wa Michikichi vikiwa chini ya Kituo cha TARI-Kihinga.
Mhe Mgumba amezipongeza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Magereza kwa ushirikiano wanaouonyesha katika uimarishaji na uendelezaji wa zao la Michikichi.
“Kama unavyofahamu mchakato wa kuandaa miche ya michikichi unachukua zaidi ya mwaka mmoja na nusu kuanzia kuchavisha mpaka kuwa mche kwa ajili ya kupeleka kwa wakulima, hivyo ushirikiano huo tunaoupata ni utimilifu wa uratibu wa zoezi hili” Alisema
MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com