Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi waliyohudhuria
katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria, iliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere
Square jijjini Dodoma Februari 2, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi waliyohudhuria
katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria, iliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere
Square jijjini Dodoma Februari 2, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Asema uelewa mdogo wa sheria unachangia wananchi kupoteza haki
MASUALA ya kisheria si
mepesi kujulikana kwa kila mwananchi na kwa sababu hiyo, wananchi wengi
wamekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo, jambo linalochangia baadhi kukosa au
kupoteza haki zao.
Pia, wananchi wengi hawajui
taratibu na mienendo ya kimahakama, hivyo wamekuwa wakipoteza haki kwa kigezo
cha kutofuata taratibu ili kupata haki zao hizo na wakati mwingine unaweza
kukuta ni suala dogo tu.
Kila mwaka, Mahakama ya
Tanzania imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Sheria, ambapo pamoja na mambo mengine,
wiki hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi kwa kuwa inatoa fursa ya
wananchi kupata elimu kuhusu masuala ya sheria.
Maadhimisho hayo ya Wiki ya
Sheria yamekuwa yakifanyika kimkoa na kitaifa kwa wadau mbalimbali wa masuala
ya sheria kutoa huduma kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kusikiliza masuala yao
na kuyapatia ufumbuzi na kwa yale ambayo huhitaji ufumbuzi zaidi, hupewa
msaada.
Kwa mwaka huu, maadhimisho
ya Wiki ya Sheria, yamefanyika kwa mara ya kwanza Jijini Dodoma, baada ya
Serikali kuhamishia makao makuu ya nchi katika jiji hilo.
Maadhimisho hayo
yalihudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwemo wadau wa sheria. Mgeni rasmi alikuwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Akifungua maadhimisho hayo,
Waziri Mkuu aliwataka wananchi wayatumie ipasavyo maadhimisho hayo ili waweze
kupata elimu na huduma mbalimbali za kisheria.
Majaliwa alisema wananchi
wa mikoa mbalimbali, ukiwemo Dodoma, wanatakiwa kutumia maadhimisho hayo kwa
kujitokeza kwa wingi kupata elimu na kwa wale wenye matatizo ya kisheria
kuyaeleza ili yatatuliwe.
“Kwa yule ambaye hana
tatizo, aje kupata elimu ya sheria, kutoa maoni au mapendekezo yake kuhusu
mfumo mzima wa utoaji wa haki. Waswahili husema, elimu haina mwisho. Kwa kuwa
elimu ya sheria imesogezwa hapa Dodoma, tumieni fursa hii kujifunza kadri
iwezekanavyo,” alisema.
Waziri Mkuu alibainisha
kuwa, Serikali imeendelea kushirikiana na mhimili wa Mahakama katika
kuhakikisha huduma bora za utoaji haki zinawafikia wananchi kwenye maeneo
wanayoishi kwa wakati.
“Serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli ni mdau muhimu wa Mahakama na
inafuatilia kwa karibu changamoto zote zinazoikabili pamoja na wadau wengine
katika mfumo wa utoaji haki,” alibainisha.
Waziri Mkuu
alisema dhamira ya Mahakama kutumia Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), katika kuleta mabadiliko ya utoaji haki ni hatua nzuri na
itasaidia kuboresha utoaji wa haki kwa wakati.
Hivyo, Waziri Mkuu
aliwasihi watumishi wa Mahakama kujikita katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA
bila kukatishwa tamaa na changamoto zitakazojitokeza kwani mara nyingi kitu
kipya chochote hakikosi changamoto za hapa na pale.
“Binafsi naunga mkono
uamuzi wa Mahakama kutumia TEHAMA katika usajili wa mashauri, kwani unakwenda
sanjari na azma ya Serikali kuhakikisha TEHAMA inatumika vema kwenye taasisi za
umma,” alisema.
Aliongeza kuwa matumizi ya
TEHAMA katika taasisi za umma yanalenga kutoa huduma bora na kuipunguzia
Serikali na mihimili mingine gharama za uendeshaji, hususan katika utoaji
huduma kwa wananchi.
Alisema lengo la Serikali
ni kuona huduma bora zinawafikia wananchi kwa urahisi na pia zinapatikana kwa
wakati.
“Nitoe wito kwa wadau,
wakiwemo mawakili wa serikali na wa kujitegemea, kutumia mifumo hiyo katika
kusajili mashauri na wasiwe wao wa kwanza katika kulaumu na kubeza,”
alisema.
Waziri Mkuu alisema
mawakili wote wa Serikali na wa kujitegemea, wanapaswa kuwa sehemu ya kutatua
changamoto zitakazoibuka katika matumizi ya mifumo hiyo kwa kuwasilisha
mapendekezo kuhusu namna bora ya kuiboresha.
Alisema matumizi
ya TEHAMA si tu yatawawezesha kutoa huduma kwa wakati, bali
pia yataweka uwazi, ambao utawapunguzia malalamiko mengi kuhusu
watumishi na utoaji haki.
Waziri Mkuu alisisitiza
kuwa Wiki ya Sheria ni muhimu kwa mfumo mzima wa utoaji haki nchini.
“Endeleeni kuienzi na itumieni vizuri katika kufanikisha malengo ya Mahakama ya
kumpatia haki kila mwananchi bila ubaguzi.”
Kwa upande wake, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, alisema kwa kipindi cha
wiki nzima, maonyesho ya Wiki ya Sheria yatafanyika Jijini Dodoma na
kwenye Mahakama zote nchini, kuanzia ngazi ya wilaya.
Profesa Juma
alisema kupitia maonyesho hayo, wananchi watakaoshiriki na
kutembelea mabanda, watapata elimu na kutathmini umuhimu na hadhi ya mfumo wa
kimahakama katika kustawisha maisha yao pamoja na kuwasaidia kupata haki kwa
mujibu wa sheria.
“Kujikumbusha umuhimu wa
Mahakama kutoa haki kwa wakati, kuzingatia misingi ya maadili na Mahakama
kuendeleza programu za maboresho yanayolenga kupeleka huduma za utoaji haki
karibu zaidi na wananchi,” alisisitiza.
Jaji Mkuu aliwakumbusha
viongozi wa vijiji, kata, wilaya, mkoa, idara na wizara, wabunge, majaji,
mahakimu na watumishi wa umma, wahudhurie maonyesho hayo ya Wiki ya Sheria bila
kukosa.
Alitolea mfano banda la
maonyesho la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwamba, kwa wale watakaoshiriki,
watakumbushwa kuwa mamlaka ya mihimili mitatu ya dola yanatokana na
nguvu ya sheria, ambayo haimuonei mwananchi yeyote.
Katika maadhimisho hayo,
ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam, Waziri Mkuu
alishiriki matembezi ya kilomita tano akiwa na Jaji Mkuu, Profesa Juma na
viongozi wengine, yakianzia Mahakama Kuu Dodoma hadi viwanja vya Nyerere
Square na kisha alitembelea mabanda.
0 comments:
Post a Comment