Waziri
wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akihoji jambo wakati wa kikao na Balozi wa
Canada nchini Pamela O’Donnel (wa pili kutoka kushoto)
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akiagana na Balozi wa Canada nchini mara baada ya kumaliza kikao baina yao. Katikati ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya wizara na Balozi wa Canada nchini Pamela O’Donnel (wa pili kutoka kushoto).
Waziri
wa Madini, Doto Biteko amewatoa hofu Wawekezaji wa Nje na kueleza kuwa, Mabadiliko
yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, hayana lengo la
kuwakandamiza isipokuwa yamelenga katika kuifanya rasilimali madini
kuwanufaisha wote, wawekezaji na watanzania.
Aliyasema
hayo Januari 4, 2019 katika kikao baina yake na Balozi wa Canada nchini Pamela
O’Donnel, ambacho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, Mkurugenzi wa Idara ya Sera
na Mipango, Augustine Ollal.
Akielezea
lengo la kuonana na uongozi wa juu wa Wizara, Balozi O’Donnel alisema amefika
ili kupata uelewa wa mabadiliko mbalimbali yaliyotokea katika sekta ya madini
pamoja na maeneo mengine ili kuwatoa hofu wawekezaji kutoka katika taifa lake
wanaopenda kuwekeza nchini.
Pamoja
na nia yake ya kupata ufumbuzi kwa masuala ya Sheria ya Madini, Balozi O’Donnel
alihoji kuhusu masuala mengine ikiwemo utawala wa kisheria, mikataba ya madini,
kodi na tozo mbalimbali pamoja na upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi nchini
kwa wananchi kutoka nchini Canada.
Akijibu
hoja hizo, Waziri Biteko aliwataka wawekezaji kutoka nchini Canada kutokuwa na
wasiwasi kwa mabadiliko hayo na kuwataka kutembelea ofisi ya madini ili kupata
ufafanuzi wa jambo lolote lenye utata katika kufanikisha nia njema ya kuwekeza
nchini. “Tupo kwa ajili yao, wasisite kupata ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu
sekta ya madini,” alisisitiza.
Aliongeza
kuwa, mataifa mbalimbali duniani yanafanya mabadiliko katika masuala mbalimbali
na kueleza kuwa, si vibaya kwa Tanzania kufanya mabadiliko kwa jambo lolote ambalo
lina manufaa kwa taifa.
Waziri
Biteko alieleza kuwa, madini ni rasilimali inayokwisha, hivyo ni muhimu madini
yanapochimbwa yawaletee faida watanzania
na pindi yatakapokwisha wajivunie
rasilimali madini iliyokuwepo kutokana na maendeleo yaliyoletwa na Madini hayo
kama vile barabara bora, shule, ujenzi wa vituo vya Afya na masuala mengine ya
maendeleo.
“Sheria
ya awali ilikuwa hainufaishi taifa na watanzania ndio maana mabadiliko
yanafanyika.Mabadiliko ni kitu kizuri, tunahitaji rafiki atakayesababisha
mabadiliko kutokea hivyo hawana haja ya kuogopa, tunawakaribisha kuwekeza” alisisitiza
Biteko.
Akifafanua
zaidi, Biteko alieleza kuwa, mabadiliko ya sheria ya madini yamekuwa
yakifanyika kulingana na sera inayoongoza. Alieleza kuwa tangu kutungwa kwa
sheria ya madini mwaka 1998 mabadiliko yamefanyika kwa awamu mbili yaani mwaka
2010 na mwaka 2017 lengo likiwa ni moja tu, rasilimali madini iweze kulinufaisha
taifa na Watanzania.
Aidha,
alibainisha kuwa mabadiliko ya kisheria yanayotokea katika sekta ya madini yanapitia
mchakato wa kutosha kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta na hayatokei
kwa ghafla kama inavyozungumzwa.
Waziri
Biteko alisema serikali imekusudia kuziwezesha benki za ndani kukua na hivyo
kuwataka wawekezaji kutunza fedha zao katika benki za ndani na endapo wawekezaji
watataka kutunza fedha zao katika benki za nje watumie benki zenye usajili
nchini Tanzania.
Kuhusiana
na suala la upatikanaji wa vibali kwa wataalamu wa kigeni kufanya kazi nchini,
Biteko alifafanua kuwa, Serikali haizuii
wataalamu kutoka nje kufanya kazi nchini isipokuwa kuwepo uwazi na uwajibikaji
na Serikali ikijiridhisha na kubaini
kuwa nchini hakuna mtaalamu wa kufanya kazi fulani serikali haitasita kutoa
kibali kwa watu kutoka nje ya nchi kuja kufanya kazi nchini.
Kwa
upande wa utawala wa kisheria, Biteko alikiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inaongoza nchi kwa Sheria na taratibu bila kuchagua wala kubagua.
Biteko
alitanabaisha kuwa kutokana na ukweli kwamba wapo watu ambao wamejikita katika
kuamini mitazamo hasi na hawataki ukweli ni suala gumu kubadili mitazamo yao,
na kueleza kuwa, itakuwa rahisi kwa wale watakaokubali ukweli na kubadili mitazamo
hasi waliyonayo juu ya serikali ili kwenda sambamba.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema, wawekezaji ni
wadau muhimu wa maendeleo na hakuna taifa lolote lililo tayari kuwakatisha
tamaa wadau wa maendeleo.
Aidha,
alibainisha mambo manne yaliyopelekea Sheria ya Madini kufanyiwa marekebisho
ili kukidhi matakwa ya taifa na watu wake kwa ujumla na kusema kuwa mambo hayo ni
pamoja na kuongeza mapato kwa taifa kwa kuongeza mrabaha wa madini ya vito na
almasi kutoka asilimia 5 mpaka asilimia 6.
Alisema,
suala lingine ni uongezaji thamani wa rasilimali madini inayopatikana nchini
ili inaposafirishwa nje ya nchi iwe ya viwango vyenye ubora mkubwa na hivyo
kusaidia kuongeza mapato kwa taifa. Aidha, amebainsha kuwa kuna baadhi ya
madini kama ya graphite yanayoongezwa thamani kwa asilimia 90 na kusafirishwa
nje ya nchi kuongezewa ubora zaidi.
Akifafanua
hilo, Nyongo alisema ili kulipelekea taifa kuwa na viwanda vya kutosha,
serikali imefanya mabadiliko hayo ili kupata wawekezaji watakaojenga viwanda
vya kuchakata madini nchini ili yasafirishwe yakiwa katika viwango bora na
kupelekea ongezeko la fedha za kigeni nchini.
Pia, Naibu
Waziri Nyongo alizungumzia suala la uwajibikaji wa wawekezaji kwa jamii ya kitanzania
na kusema kuwa, ili kuwafanya wawekezaji kuwatumia wazawa katika kufanikisha
shughuli za uchimbaji na biashara ya madini, Sheria mpya imeweka wazi masuala
mbalimbali yanayopaswa kufanywa na wazawa na manunuzi ya baadhi ya mahitaji
kufanyika ndani ya nchi na si vinginevyo ikiwa ni pamoja na kuajili wazawa.
Mwisho
Naibu Waziri Nyongo alizungumzia suala la kuzuia wawekezaji kumiliki leseni
wasizozifanyia kazi. Alisema kuwa, wapo baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakitumia leseni
za madini kuombea mikopo katika taasisi
za kifedha nje ya nchi na baada ya kupata mikopo hiyo wamekuwa wakiendesha shughuli zao nje ya Tanzania.
Alibainisha
kuwa, ili kuwabana wawekezaji hao sheria imekuja ikiweka wazi muda maalum wa
mmiliki wa leseni kumiliki leseni hiyo vinginevyo maeneo yanarudishwa
serikalini ili kutoa fursa kwa watu wenye nia ya kufanya kazi kuendelea na
kazi.
0 comments:
Post a Comment