METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, August 16, 2026

TIB YAUNGA MKONO AJENDA YA NISHATI SAFI KUELEKEA DIRA 2050


 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akimkabidhi Tuzo pamoja na Cheti, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Deogratius Kwiyukwa, kama Ishara ya kutambua mchango wa benki hiyo katika kushiriki kukuza na kuchochea shughuli za uchuki jumuishi na shukrani kwa ushiriki na kuwa tayari kuchochea maono ya Taifa ya kumkomboa mwananchi kwa kumtengenezea mazingira bora ya uwajibikaji kwa Taifa lake, katika Kilele cha Tamasha la Kizimkazi 2026, lililohitimishwa mwishoni wa Juma lililopita.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Kizimkazi, Zanzibar)

Na Benny Mwaipaja, Kizimkazi-Zanzibar

Safari ya mageuzi ya kiuchumi kuelekea Dira ya Taifa 2050 imeanza kushika kasi, huku mijadala kuhusu vichocheo vya uchumi ikiendelea kupewa uzito mkubwa nchini.

Miongoni mwa matukio yaliyoibua mjadala huo ni Tamasha la Kizimkazi 2026, lililofanyika kusini mwa Unguja na kukutanisha viongozi wakuu wa serikali, taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Tamasha hilo lilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel John Nchimbi, pamoja na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, sambamba na viongozi wengine wa serikali akiwemo Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), vyama vya siasa, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mbali na kuwa jukwaa la kukutanisha wadau, tamasha hilo pia lilikuwa sehemu muhimu ya mdahalo wa kitaifa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, ambapo viongozi waandamizi walitoa maoni yao kuhusu umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama sehemu ya maendeleo endelevu ya taifa.

Ajenda ya nishati safi inaenda sambamba na nguzo ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ambayo ni sehemu ya msingi ya Dira 2050.

Kupitia nguzo hiyo, Tanzania inalenga kuwa kinara wa kimataifa katika uhifadhi wa mazingira kwa kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za asili na kuimarisha uwezo wa taifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Miongoni mwa taasisi zilizojitokeza kwa nguvu katika tamasha hilo ni Benki ya Maendeleo TIB, iliyoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Deogratius Kwiyukwa. TIB ni benki ya maendeleo ya Serikali iliyoanzishwa mahsusi kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini kupitia utafutaji wa mitaji, uandaaji wa miradi ili iweze kuvutia uwekezaji, pamoja na usimamizi wa mifuko ya maendeleo kwa niaba ya serikali na sekta binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari kando ya tamasha hilo, Bw. Kwiyukwa alisema

Benki ya Maendeleo ya Tanzania TIB, imejipanga kuongeza ufadhili wa miradi ya nishati safi nchini, kama sehemu ya jitihada za Taifa za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema benki hiyo imetenga fedha maalum za kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa miradi ya nishati mbadala ikiwemo ya jua, upepo, gesi asilia na nishati ya maji.

“Tunafahamu kuwa nishati safi ndio mkombozi wa viwanda, kilimo na nyumba za Watanzania. Kupitia ufadhili huu tunalenga kupunguza utegemezi wa nishati chafu na kuchochea uchumi wa kijani,” amesema Bw. Kwiyukwa.

Kwa mujibu wa TIB, hatua hii pia inalenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika miradi mikubwa ya miundombinu ya nishati, ambayo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ajira kwa vijana.

“Benki ya Maendeleo ya TIB imekuwa na mchango mkubwa hapa nchini katika kuleta mabadiliko chanya katika ukuaji wa sekta mbalimbali. Kupitia tamasha hili la Kizimkazi, tunaungana na Mheshimiwa Rais na wadau wengine kupambanua na kuonesha mchango wa sekta zote kufikia malengo ya Dira,” alisema.

Alieleza kuwa benki hiyo imejikita katika sekta mbalimbali muhimu ikiwemo miundombinu, nishati, utalii, uchumi wa buluu, vijana na wanawake, pamoja na utunzaji wa mazingira.

Kwa mujibu wa Bw. Kwiyukwa, TIB pia inasimamia mifuko mbalimbali ya maendeleo kwa niaba ya serikali na taasisi nyingine, ikiwemo mifuko ya maji, umeme vijijini, na nishati safi, katika Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema dhamira kuu ni kufikisha maendeleo kwa wananchi na kupunguza vihatarishi katika maeneo ambayo benki za biashara hushindwa kuyafikia.

Katika hatua nyingine, TIB kupitia kampuni yake tanzu ya TIB Rasilimali, imeendelea kufungua njia mbadala za upatikanaji na ukuzaji wa mitaji. Kampuni hiyo ni miongoni mwa mawakala wakubwa wa soko la hisa la Dar es Salaam, ikiwa na jukumu la kuuza na kununua hisa kwa niaba ya taasisi na watu binafsi. Pia hutoa huduma za elimu ya fedha, uwekezaji, pamoja na uwakala wa bima.

Bw. Kwiyukwa alisema kupitia TIB Rasilimali, taasisi na wananchi wamekuwa wakihamasishwa kutambua njia mbadala za kukuza mitaji yao bila kutegemea fedha za Serikali pekee.

Alibainisha kuwa Ofisi za Dar es Salaam na majukwaa ya mitandaoni zimekuwa zikiendesha madarasa maalumu ya kila wiki, hasa kwa vijana, ili kuwapa uelewa kuhusu njia salama na za uhakika za uwekezaji.

“Jitihada hizo zinaunga mkono malengo makubwa ya Dira 2050, yanayolenga kujenga uchumi wa thamani ya dola trilioni moja, kuongeza wastani wa kipato cha Mtanzania hadi dola 7,000 kwa mwaka, pamoja na kuhakikisha sekta binafsi inachangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa” alisema Bw. Kwiyukwa.

Sambamba na ushiriki wake katika tamasha hilo, Benki ya Maendeleo TIB pia ilitunukiwa tuzo na cheti kutoka kwa Mheshimiwa Rais kama ishara ya kutambua mchango wake na utayari wake wa kuchochea maono ya Taifa ya kumkomboa mwananchi kiuchumi kupitia maendeleo jumuishi.

Akihitimisha, Bw. Kwiyukwa aliipongeza Mwanamke Initiative Foundation (MIF) kwa kuandaa Tamasha la Kizimkazi, akieleza kuwa limefungua fursa pana kwa Watanzania kujadili masuala muhimu ya maendeleo. Pia aliahidi kuwa TIB itaendelea kushiriki katika matamasha na majukwaa mengine yenye lengo la kuchochea maendeleo ya Taifa.

Sambamba na hayo, katika Tamasha hilo la Kizimkazi 2026, Benki ya Maendeleo TIB ilitunikiwa tuzo pamoja na cheti na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama Ishara ya kutambua mchango wa benki hiyo katika kushiriki kukuza na kuchochea shughuli za uchuki jumuishi na shukrani kwa ushiriki na kuwa tayari kuchochea maono ya Taifa ya kumkomboa mwananchi kwa kumtengenezea mazingira bora ya uwajibikaji kwa taifa lake.

Kwa ujumla, ushiriki wa TIB katika Tamasha la Kizimkazi 2026 umeonesha wazi nafasi ya taasisi za maendeleo katika kusukuma mbele ajenda ya nishati safi, uhifadhi wa mazingira na uwezeshaji wa kiuchumi, yote ikiwa ni sehemu ya safari ya Tanzania kuelekea Dira 2050.


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com