Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia akihutubia wakati wa hafla ya utoaji Tuzo ya Kiswahili ya Mabati –Cornell ya Fasihi ya Afrika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda kurudisha fadhila kwa jamii ikiwemo
kuwekeza katika lugha ya Kiswahili.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo ya
Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasiji ya Kiafrika iliyofanyika kwenye ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es Salaam.
“kwa hakika hii lugha haiwezi kupiga hatua bila kuwekewa uwekezaji wa
dhati utakaojumuisha Serikali, sekta binafsi na asasi za kiraia”alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa maendeleo yeyote ya Taifa hayawezi
kufikiwa bila kuwa na lugha ya mawasiliano inayounganisha watu wa
ndani ya nchi na hata nje ya nchi.
Tuzo hizi zimedhaminiwa na kampuni ya kutengeneza mabati ya ALAF Limited
Tanzania pamoja na mshirikika wake kampuni ya Mabati Rolling
Mills,Kenya kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha, Serikali imeendelea kuwatafutia walimu wetu wa Kiswahili fursa
mbalimbali za ajira ikiwemo kuwapeleka nchi jirani pamoja na kuzishawishi nchi
hizi kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa waandaaji kuangalia namna ya kuhamasisha
washiriki kutoka nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.
Makamu wa Rais alionyesha umahiri wake pale alipoamua kughani moja ya
beti kutoka kwa mshahiri maarufu mkongwe Mzee Haji Gora.
Pamoja na mambo mengine Makamu wa Rais alisisitiza jamii kuienzi lugha
ya Kiswahili kwani imekuwa kiungo muhimu baina ya familia na koo mbali mbali
hapa nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Uwekezaji alisema matumizi ya lugha
rahisi yanachagia kukuwa kwa maarifa na uelewa mahala pa kazi.
Washindi wa tuzo ya Kiswahili mwaka huu ni Bi. Zainab Alwi Baharoon na
Bw. Jacob Ngumbau Julius.
Wakati huohuo Makamu wa Rais alizindua kitabu cha washindi wa mwaka
2017, Bw. Ally Hilal na Doto Rangimoto .
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi mbali mbali na wadau wa Kiswahili
kutoka sehemu mbali mbali duniani.
0 comments:
Post a Comment