METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, January 9, 2019

WIZARA YA YA KILIMO IPO KATIKA MAPITIO YA SIFA ZA VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA – MHANDISI MTIGUMWE

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Rukwa

Wizara ya Kilimo ipo katika mapitio ya sifa za viongozi wa Vyama vya Ushirika nchini ili kupata viongozi watakao ongoza kwa weledi sekta ya Ushirika.

Dhana ya kuchagua viongozi wa ushirika wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika imepitwa na wakati hivyo kuna kila sababu ya kuchagua viongozi wenye weledi na utashi katika utendaji.

Hayo yameelezwa jana tarehe 8 Januari 2019 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe wakati akizungumza kwenye kikao kazi na maafisa wa Kilimo wa Wilaya za Mkoa wa Rukwa, Wadau mbalimbali wa Kilimo wakiwemo mawakala wa pembejeo, wasindikaji, wawakilishi wa vyama vya msingi vya ushirika na wakulima, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Alisema kuwa mfumo wa ushirika  ni nyenzo muhimu ambayo ukitumika vizuri itasaidia kuondoa  umaskini wa wakulima hapa nchini na utaimarisha uanzishwaji wa viwanda kuleta tija katika kilimo hivyo ni lazima kuwa na juhudi za makusudi kuwa na viongozi wenye weledi.

Katibu Mkuu huyo katika ziara yake mkoani Rukwa alitembelea maduka na maghala ya mbolea yanayomilikiwa na kampuni za ETG, YARA na PREMIER na kujionea hali halisi ya upatikanaji wa mbolea ambapo amepongeza utoshelevu wa mbolea uliopo mkoani humo.

Akizungumzia swala la masoko ya mazao ya wakulima Mhandisi Mtigumwe alisisitiza kuwa ubora wa mazao ya wakulima ni suala la msingi kulizingatia ili kuweza kusaidia wakulima kupata masoko ya uhakika na kujiongezea kipato, kwani mazao bora yana ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kuhusu Milipuko ya visumbufu vya mimea, Mhandisi Mtigumwe alisisitiza kuwa ili kunusuru mazao ya wakulima nchini, hatua madhubuti zinaendelea kuchukuliwa ili kuweza kudhibiti wadudu wanaothiri mazao akiwemo Kiwavijeshi Vamizi (FAW).

Hivyo, alitoa rai kwa Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa na Makatibu Tawala wote nchini, kuwaagiza Maafisa Kilimo kufanya tathmini ya awali na kubaini maeneo ambayo kiwavijeshi vamizi ameanza kuonekana ili Wizara kwa kushirikiana na halmashauri ziweze kuchukua hatua za kudhibiti milipuko ya kiwavijeshi vamizi kabla hajasambaa zaidi na kuleta athari kubwa.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com