Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe
Na Mathias Canal,
Wizara ya Kilimo-Rukwa
Wizara ya Kilimo ipo katika mapitio ya sifa za viongozi wa
Vyama vya Ushirika nchini ili kupata viongozi watakao ongoza kwa weledi sekta
ya Ushirika.
Dhana ya kuchagua viongozi wa ushirika wenye sifa ya kujua
kusoma na kuandika imepitwa na wakati hivyo kuna kila sababu ya kuchagua
viongozi wenye weledi na utashi katika utendaji.
Hayo yameelezwa jana tarehe 8 Januari 2019 na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe wakati akizungumza kwenye kikao kazi
na maafisa wa Kilimo wa Wilaya za Mkoa wa Rukwa, Wadau mbalimbali wa Kilimo
wakiwemo mawakala wa pembejeo, wasindikaji, wawakilishi wa vyama vya msingi vya
ushirika na wakulima, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Rukwa.
Alisema kuwa mfumo wa ushirika ni nyenzo muhimu ambayo
ukitumika vizuri itasaidia kuondoa umaskini wa wakulima hapa nchini na
utaimarisha uanzishwaji wa viwanda kuleta tija katika kilimo hivyo ni lazima
kuwa na juhudi za makusudi kuwa na viongozi wenye weledi.
Katibu Mkuu huyo
katika ziara yake mkoani Rukwa alitembelea maduka na maghala ya mbolea
yanayomilikiwa na kampuni za ETG, YARA na PREMIER na kujionea hali halisi ya
upatikanaji wa mbolea ambapo amepongeza utoshelevu wa mbolea uliopo mkoani
humo.
Akizungumzia swala
la masoko ya mazao ya wakulima Mhandisi Mtigumwe alisisitiza kuwa ubora wa
mazao ya wakulima ni suala la msingi kulizingatia ili kuweza kusaidia wakulima
kupata masoko ya uhakika na kujiongezea kipato, kwani mazao bora yana ushindani
katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kuhusu Milipuko ya
visumbufu vya mimea, Mhandisi Mtigumwe alisisitiza kuwa ili kunusuru mazao ya
wakulima nchini, hatua madhubuti zinaendelea kuchukuliwa ili kuweza kudhibiti
wadudu wanaothiri mazao akiwemo Kiwavijeshi Vamizi (FAW).
Hivyo, alitoa rai
kwa Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa na Makatibu Tawala wote nchini, kuwaagiza
Maafisa Kilimo kufanya tathmini ya awali na kubaini maeneo ambayo kiwavijeshi
vamizi ameanza kuonekana ili Wizara kwa kushirikiana na halmashauri ziweze
kuchukua hatua za kudhibiti milipuko ya kiwavijeshi vamizi kabla hajasambaa
zaidi na kuleta athari kubwa.
MWISHO
No comments:
Post a Comment