Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto ndani ya msingi) akisaidia kuchimba msingi wa itakayokuwa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga baada ya kushirikiki na wananchi wa bonde la ziwa Rukwa kwenye songambele ya uchimbaji wa misingi ambao ungegharimu shilingi milioni 8 kama wangetumika mafundi.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (ndani ya msingi) akisaidia kuchimba msingi wa itakayokuwa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga baada ya kushirikiki na wananchi wa bonde la ziwa Rukwa kwenye songambele ya uchimbaji wa misingi ambao ungegharimu shilingi milioni 8 kama wangetumika mafundi.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (kulia) akiendelea kuhamasisha wananchi walioshiriki kwenye songamebele ya kuchimba misingi kwaajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga.
Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga
kufuatilia na kusimamia wananchi wa vijiji 12 vya bonde la ziwa Rukwa
kuhakikisha kuwa wanaanza kujenga zahanati ili zahanati hizo ziweze kupunguza
mzigo kwa vituo vya afya na hospitali ya wilaya.
Amesema
kuwa ili hospitali ya Wilaya isiweze kuzidiwa na wagonjwa ni vyema vijiji
vikawa na zahanati zao na kwa ngazi ya kata kuanza ujenzi wa vituo vya afya ili
mgonjwa apitie katika ngazi hizo na hatimaye kufika katika ngazi ya hospitali
ya wilaya tofauti na hapo hospitali hiyo inaweza kutumiwa na hata wagonjwa
ambao wanaweza kutibiwa katika ngazi ya zahanati.
“Kwa
upande wa vituo vya afya, jamani nisikitike hapa, katika kata 13 ambapo kila
kata inapaswa iwe na kituo chake cha afya tunavyo vituo vya afya viwili peke
yake, tuna kituo cha afya pale milepa na kituo cha afya hapa mtowisa, kwahiyo
kata 11 hazina vituo vyake vya afya, kwahiyo hapa pia DC jipange tuanze,”
Alisema.
Mh.
Wangabo aliyasema hayo wikiendi hii katika songambele ya kuchimba msingi wa
majengo saba kwaajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya katika kata ya Mtowisa
na kuhusisha wananchi kutoka katika vijiji 10 na madiwani 13 wa kata zote za
bonde la ziwa Rukwa ambapo hospitali hiyo inajengwa.
Akitoa
taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo, mganga mkuu wa halmashauri ya Wilaya ya
Sumbawanga Dkt. Fani Musa alisema kuwa hospitali hiyo itatumika kama kituo cha
rufaa kutoka vituo vya afya na zahanati zote za halmashauri ya wilaya ya
Sumbawanga na kuongeza kuwa mradi utagharimu shilingi Bilioni 7.5 hadi
kumamilika kwake ambapo itakuwa na majengo 22 na mpaka sasa halmashauri
imepokea shilingi bilioni 1.5 kwaajili ya kuanza ujenzi huo.
“Fedha
hizi za awamu ya kwanza zitatumika kujenga majengo saba, jengo la Utawala
ambalo litatumia shilingi milioni 332, jengo la wagonjwa wa nje litatumia
shilingi milioni 271, jengo la “Pharmacy” litatumia shilingi milioni 120, jengo
la maabara litatumia shilingi milioni 171, jengo la vipimo vya mionzi
(radiology, X-ray na Ultra Sound) litatumia shilingi milioni 121, jengo la
kufulia litatumia shilingi milioni 110 na jengo la mwisho ni la wazazi
litakalotumia shilingi milioni 379,” Alisema.
Katika
hatua nyingine Mh. Wangabo amewataka wakala wa umeme vijijini kuhakikisha
wanaongeza kasi ya kufikisha umeme kwenye bonde hilo ambalo lina wakulima wengi
wa mahindi na mpunga pamoja na wavuvi ambapo mazao yao mengi huvushwa na
kupelekwa mikoa ya jirani hivyo kuukosesha mkoa mapato na pia kwaajili ya
kusaidia huduma za kiafya katika bonde hilo na kuongeza kuwa bila ya
halmashauri kuongeza kasi ya kukusanya mapato malengo hayo ya kumalizia maboma
hayatafikiwa.
Bonde la
ziwa Rukwa lina vijiji 63, kati ya vijiji hivyo vijiji 24 vina zahanati, vijiji
17 vina maboma ya zahanati ambayo hayajaezekwa na vijiji 12 havina zahanati
wala maboma, na kati ya kata 13 zilizopo katika bonde hilo ni kata 2 tu ndio
zenye vituo vya afya na kufanya kata 11 kukosa vituo vya afya huku kata 3
zikiwa na maboma ya vituo hivyo.
0 comments:
Post a Comment