Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisalimiana na Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Duniani (ICA) Dkt Ariel Guarco wakati walipokutana na kufanya mazungumzo Jana tarehe 21 Januari 2019 Jijini Dar es salaam.
Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Duniani (ICA) Dkt Ariel Guarco akikagua Samani zinazotengenzwa na Chama cha Ushirika DACICO cha eneo la Kariakoo Jijini Dar es salaam, Jana tarehe 21 Januari 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Duniani (ICA) Dkt Ariel Guarco wakati walipokutana na kufanya mazungumzo Jana tarehe 21 Januari 2019 Jijini Dar es salaam. Wengine ni viongozi wa Shirikisho hilo Barani Afrika na Tanzania.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Duniani (ICA) Dkt Ariel Guarco wakati walipokutana na kufanya mazungumzo Jana tarehe 21 Januari 2019 Jijini Dar es salaam. Wengine pichani ni viongozi wa Shirikisho hilo Barani Afrika na Tanzania.
Na Mathias Canal,
Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo
Mhe Japhet Hasunga (Mb) Jana tarehe 21 Januari 2019 katika ukumbi wa Wizara ya
Kilimo maarufu (Kilimo I) Mtaa wa Tazara Jijini Dar es salaam amekutana na
kufanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika Duniani (ICA)
Dkt Ariel Guarco.
Katika mkutano huo
uliotanguliwa na ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vyama vya Ushirika
Jijini Dar es salaam Rais huyo ameambatana Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho
hilo Ndg Bruno Roelants pamoja na Rais wa Shirikisho la vyama vya Ushirika
Afrika Ndg Japhet Magomere na Katibu Mkuu
wa Shirikisho la hilo barani Afrika Bi Chiyoge Sifa
Pamoja na mambo
mengine Mhe Hasunga amemuhakikishia kiongozi hugyo wa Shirikisho hilo kuwa
serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli
imedhamiria kuboresha mapungufu ya muda mrefu kwenye vyama vya Ushirika ikiwemo
kushughulikia viongozi wabadhilifu.
Hasunga alisema
kuwa serikali kupitia Wizara ya Kilimo ipo
katika mapitio ya sifa za viongozi wa Vyama vya Ushirika nchini ili kupata
viongozi watakao ongoza kwa weledi sekta ya Ushirika.
Alimueleza Rais
huyo kuwa Dhana ya kuchagua viongozi wa ushirika wenye sifa ya kujua kusoma na
kuandika imepitwa na wakati hivyo kuna kila sababu ya kuchagua viongozi wenye
weledi na utashi katika utendaji.
Aliongeza kuwa
mfumo wa ushirika ni nyenzo muhimu ambayo ukitumika vizuri itasaidia
kuondoa umaskini wa wakulima hapa nchini na Dunia kote utaimarisha
uanzishwaji wa viwanda kuleta tija katika kilimo hivyo ni lazima kuwa na juhudi
za makusudi kuwa na viongozi wenye weledi.
Alisema kuwa Wizara
yake pia imeanza kupitia upya sheria ya vyama vya Ushirika ili kuwa na Ushirika
imara na wenye nguvu na tija kwa wakulima kwani kufanya hivyo kutaongeza Imani
ya wananchi waliokata tamaa na Ushirika.
Alisema pia
miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya Ushirika nchini ni kukosekana
kwa taarifa sahihi za wanachama (Data Base) kuanzia vyama vya msingi (Union)
hadi vyama Vikuu vya Ushirika (AMCOS) jambo ambalo kwa muda mrefu limepelekea
kuwa na Ushirika usiokuwa na tija na manufaa kwa wakulima wanaotumia nguvu na
rasilimali zao nyingi katika kilimo.
Naye, Rais wa
Shirikisho la vyama vya Ushirika Duniani (ICA) Dkt Ariel Guarco amesema kuwa
msingi wa ziara yake hiyo katika Afrika Mashariki pamoja na nchi zingine ni
sehemu ya utekelezaji wa wajibu wake ambapo alianzia Kenya, Rwanda na sasa
Tanzania.
Alisema kuwa
Tanzania ni miongoni kwa nchi zilizopo chini ya Jangwa la Sahara ambayo
imepokea vyema dhana ya Ushirika ambapo serikali inaunga mkono kwa kiasi
kikubwa hivyo ana Imani miaka michache ijayo kupitia mfumo huo wakulima
watakuwa na mafanikio yasiyopimika.
Alisema kuwa
amezuru nchini Tanzania kwa ajili ya kuonana na kufanya mazungumzo na wana
Ushirika ikiwa ni sehemu ya kubaini na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka
changamoto mbalimbali kwenye sekta ya Ushirika. Vilevile ameeleza kuwa
ziara hiyo ni sehemu ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano uliyopo baina ya
Tanzania na Shirikisho hilo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirikisho la vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) Bi Aberhad
Mbepera alisema kuwa ziara ya Rais huyo ni sehemu ya ushirikiano uliopo
kati ya Tanzania na ICA.
Alitoa wito kwa
wakulima kujiunga na vyama vya Ushirika kwani katika Ushirika kutaimarisha
umoja na mshikamano kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa na kauli moja katika
kupanga bei ya bidhaa zao pasina kugalalizwa.
Akitoa neno la
shukrani Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt Titus Kamani
alisema kuwa maisha ya watanzania yataimarika kupitia Ushirika hivyo Tume hiyo
imejipanga kutoa elimu kwa wakulima nchini kuelewa umuhimu wa kujiunga na mfumo
wa Ushirika.
Alisema Ushirika ni
nyenzo pana katika maisha halisi ya wananchi kwani hatua mbalimbali za wananchi
zinategemea Ushirika kuanzia maisha ya kawaida, biashara na kilimo.
Aliongeza kuwa Tume
ya Maendeleo ya Ushirika imedhamiria kuwanufaisha watu masikini kuwa na kipato
cha kati kitakachomudu ukali wa maisha na kuwa na utajiri.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment