METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, January 16, 2019

KAULI YA DC MUHEZA YAMNUSURU MKUU WA IDARA YA ARDHI KUTUMBULIWA


 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angelina Mabula akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halamashauri ya Wilaya ya Muheza Salehe Kang'e wakati wa ziara ya kushtukiza kufuatilia maagizo aliyoyatoa katika halmashauri hiyo jana. kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza Hajjat Muhandisi Mwanaasha Tumbo.
 Mkuu wa Wilaya ya Muheza Hajjat Muhandisi Mwanaasha Tumbo akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula katika wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akimpa maelekezo Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halamashauri ya wilaya ya Muheza Salehe Kang'e alipofanya ziara ya kushtukiza katika halmashauri hiyo jana.
Na Munir Shemweta, MUHEZA
Kauli ya Mkuu wa wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga Hajjat Mhandisi Mwanaasha Tumbo kuwa idara ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Muheza haina mtendaji wa sekta ardhi anayeweza kuvaa viatu vya ukuu wa idara iwapo anayeshikilia sasa nafasi hiyo Salehe Kang'e ataondolewa imemnusuru mkuu huyo wa sekta ya ardhi kutumbuliwa katika nafasi yàke.
Kauli hiyo inafuatia Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula kueleza kuwa Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri hiyo hafai kuwa mkuu wa idara kutokana na kushindwa kusimamia vyema ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza Bakari Mhando alimuomba Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutomuondoa katika nafasi hiyo mkuu huyo wa Idara na kubainisha kuwa mapungufu aliyoyaonesha atahakikisha yanarekebishwa ndani ya mwezi mmoja.
Akiwa katika ziara ya kustukiza katika halmashauri ya wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga tarehe 15 Januari 2019 Dk Mabula alionesha kuchukizwa na mkuu huyo wa idara kushindwa kusimamia ukusanyaji kodi ya ardhi ikiwemo kutoa hati za madai kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi katika wilaya ya Muheza.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Ardhi halmashauri ya wilaya ya Muheza Kang'e ambaye amebakiza mwaka mmoja kustaafu kazi, halmashauri ya wilaya yake imeingiza viwanja 3000 katika mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya kielektronik na mashamba1009 lakini imetoa hati moja ya madai kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi.
Dk Mabula alisema alichotegemea baada ya kuingizwa viwanja na mashamba kwenye mfumo huo wa ulipaji kodi kwa njia ya kielektronik mkuu wa idara ya ardhi angehakikisha wadaiwa wote sugu wanafuatiliwa ili walipe kodi lakini kinyume chake kazi hiyo haijafanyika na ni mdaiwa mmoja tu aliyepelekewa hati ya madai.
Alisema msisitizo wa serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inakusanya mapato yakiwemo ya kodi ya ardhi ili kuweza kusaidia shughuli za maendeleo ambazo haziwezi kupatikana iwapo serikali haitakuwa na makusanyo mazuri ya kodi.
" Haya yote yanayofanyika ununuzi wa ndege ujenzi wa SGR bila ya kukusanya kodi hayawezi kufanyika na siku zote Rais wa Janhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli amekuwa akisisitiza ukusanyaji kodi,  people are not serious" alisema Dk Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa mwezi mmoja kwa Mkuu huyo wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Muheza  kuhakikisha wadaiwa wote wa kodi ya ardhi wanapelekewa hati za madai na watakaokaidi wafikishwe katika mabaraza ya ardhi na ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi kanda ya Kaskazini ifuatilie utekelezaji wa agizo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Muheza Hajjat Mhandisi  Mwanaasha Tumbo alisema,  baada ya maelekezo ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alihakikisha utekelezaji  unafanyika na matunda yameanza kuonekana katika baadhi ya maeneo ya  sekta ardhi ikiwemo uingizaji wamiliki wa viwanja na mashamba katika mfumo na amemuahidi Dk Mabula kuwa suala la hati za madai nalo atalisimamia kikamilifu ilii liweze kutekelezwa.
Alisema, changamoto kubwa inayoikabili halmashauri ya wilaya ya Muheza ni kukosekana watendaji wa sekta ya ardhi wenye uwezo mkubwa wa kusimamia masuala ya ardhi na kubainisha kuwa mbali na mkuu wa idara aliyepo sasa lakini halmashauri hiyo haina watendaji wa kutosha.
------------MWISHO----------
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com