METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, January 16, 2019

ASASI ZA VIJANA ZAHIMIZWA KUWA CHACHU YA MAENDELEO NCHINI


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa asasi za maendeleo ya vijana nchini walipokutana kujadili maendeleo ya vijana kupitia programu ya mabadilishano ya vijana (Exchange Program) kati ya Nchi ya Ujerumani na Tanzania. Kongamano hili limefanyika hoteli ya Morena Januari 16, 2019, Jijini Dodoma.


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo kuhusu taulo za kike kutoka kwa Bi. Josephine Lyengi, alipokuwa akiangalia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na vijana. (Kulia) ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa, (Kushoto) ni Mkurugenzi wa Tanzania Youth Coalition (TYC) Bw. Lenin Kazoba.

Na; OWM (KVAU), Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amezitaka asasi mbalimbali zinazoshughulikia maendeleo ya vijana kuwa chachu ya maendeleo nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa asasi za maendeleo ya vijana nchini walipokutana kwa lengo la kukuza uelewa katika kutekeleza programu ya kuwawezesha vijana kati ya Ujerumani na nchi za Afrika (African – German Youth Initiative), Waziri Mhagama alisema kuwa, Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana na Sera ya Taifa ya Ajira imekuwa ikihamasisha wadau mbalimbali kuanzisha Miradi na Programu zinazowawezesha vijana kupata ujuzi na uzoefu wa kuwaweza kujiajiri au kuajiriwa katika Sekta mbalimbali ili waweze kuchangia kwenye maendeleo ya nchi.
“Vijana ndio chachu kubwa ya maendeleo endelevu, hivyo ni vyema wakatumia fursa zilizopo kuleta mabadiliko yatakayo kuwa na tija na mchango kubwa katika maendeleo ya taifa.” alisisitiza Mhagama
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa vijana wanawezeshwa ipasavyo kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Pia alifafanua kuwa, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau wanaoshughulika masuala ya maendeleo ya vijana katika kuwajengea ujuzi na uelewa vijana juu ya maendeleo. Hivyo aliipongeza Taasisi ya vijana ya Tanzania Youth Coalition katika kujenga ustawi na maendeleo endelevu kwa vijana ambao ndio wanufaika wa fursa ya programu hiyo ya mabadilishano ya vijana na Mataifa mengine.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa vijana nchini kufanya kazi kwa bidii na kuendelee kudumisha uzalendo, amani na utulivu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa alieleza kuwa Programu ya mabadilishano ya vijana (Exchange Program) imekuwa na manufaa makubwa sana katika kuwajengea uwezo vijana kupitia fani mbalimbali zinazoleta mabadiliko ya chanya katika Taifa.
Naye, Mkurugenzi wa Tanzania Youth Coalition (TYC) Bw. Lenin Kazoba alisema kuwa kongamano hilo litakuwa na manufaa kwa vijana na asasi zinazoshughulikia maendeleo ya vijana kwa kuweza kujadili kwa pamoja fursa zitakazoleta maendeleo kwa vijana na jamii inayowazunguka.
Programu ya mabadilishano ya vijana kati ya Nchi ya Ujerumani na Tanzania ilizinduliwa rasmi tarehe 30 Juni, 2016 Mjini Bonn, Ujerumani na Waziri wa Uchumi wa Ushirikiano na Maendeleo Mhe. Gurd Muller ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa moja kati ya Nchi Tatu (3) Barani Afrika zilizopewa heshima kubwa ya kuchaguliwa kutekeleza mradi huo kwenye hatua ya majaribio kupitia Tanzania Youth Coalition (TYC). Zaidi ya vijana 4,015 wamefaidika kupitia program hiyo kwa kupata ujuzi na uzoefu wa fani mbalimbali.
MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com