Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Dk Angelina Mabula akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Idara ya
Ardhi katika Halamashauri ya Wilaya ya Muheza Salehe Kang'e wakati wa ziara ya
kushtukiza kufuatilia maagizo aliyoyatoa katika halmashauri hiyo jana. kushoto
ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza Hajjat Muhandisi Mwanaasha Tumbo.
Mkuu wa Wilaya ya Muheza Hajjat
Muhandisi Mwanaasha Tumbo akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula katika wilaya ya Muheza mkoa
wa Tanga.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akimpa maelekezo Mkuu wa Idara ya
Ardhi katika Halamashauri ya wilaya ya Muheza Salehe Kang'e alipofanya ziara ya
kushtukiza katika halmashauri hiyo jana.
Na Munir Shemweta, MUHEZA
Kauli ya Mkuu wa wilaya ya Muheza mkoa
wa Tanga Hajjat Mhandisi Mwanaasha Tumbo kuwa idara ya ardhi katika halmashauri
ya wilaya ya Muheza haina mtendaji wa sekta ardhi anayeweza kuvaa viatu vya
ukuu wa idara iwapo anayeshikilia sasa nafasi hiyo Salehe Kang'e ataondolewa
imemnusuru mkuu huyo wa sekta ya ardhi kutumbuliwa katika nafasi yàke.
Kauli hiyo inafuatia Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula kueleza kuwa Mkuu wa
Idara ya Ardhi katika halmashauri hiyo hafai kuwa mkuu wa idara kutokana na
kushindwa kusimamia vyema ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri
ya wilaya ya Muheza Bakari Mhando alimuomba Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kutomuondoa katika nafasi hiyo mkuu huyo wa Idara na
kubainisha kuwa mapungufu aliyoyaonesha atahakikisha yanarekebishwa ndani ya
mwezi mmoja.
Akiwa katika ziara ya kustukiza katika
halmashauri ya wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga tarehe 15 Januari 2019 Dk Mabula alionesha kuchukizwa na mkuu huyo wa idara kushindwa
kusimamia ukusanyaji kodi ya ardhi ikiwemo kutoa hati za madai kwa wadaiwa wa
kodi ya ardhi katika wilaya ya Muheza.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Ardhi
halmashauri ya wilaya ya Muheza Kang'e ambaye amebakiza mwaka mmoja kustaafu
kazi, halmashauri ya wilaya yake imeingiza viwanja 3000 katika mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya kielektronik
na mashamba1009 lakini imetoa hati
moja ya madai kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi.
Dk Mabula alisema alichotegemea baada
ya kuingizwa viwanja na mashamba kwenye mfumo huo wa ulipaji kodi kwa njia ya
kielektronik mkuu wa idara ya ardhi angehakikisha wadaiwa wote sugu
wanafuatiliwa ili walipe kodi lakini kinyume chake kazi hiyo haijafanyika na ni
mdaiwa mmoja tu aliyepelekewa hati ya madai.
Alisema msisitizo wa serikali ya awamu
ya tano ni kuhakikisha inakusanya mapato yakiwemo ya kodi ya ardhi ili kuweza
kusaidia shughuli za maendeleo ambazo haziwezi kupatikana iwapo serikali
haitakuwa na makusanyo mazuri ya kodi.
" Haya yote yanayofanyika ununuzi
wa ndege ujenzi wa SGR bila ya kukusanya kodi hayawezi kufanyika na siku zote
Rais wa Janhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli amekuwa akisisitiza
ukusanyaji kodi, people are not serious" alisema Dk Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi alitoa mwezi mmoja kwa Mkuu huyo wa Idara ya Ardhi katika
halmashauri ya wilaya ya Muheza kuhakikisha wadaiwa wote wa kodi ya ardhi
wanapelekewa hati za madai na watakaokaidi wafikishwe katika mabaraza ya ardhi
na ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi kanda ya Kaskazini ifuatilie utekelezaji
wa agizo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Muheza Hajjat
Mhandisi Mwanaasha Tumbo alisema, baada ya maelekezo ya Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alihakikisha utekelezaji
unafanyika na matunda yameanza kuonekana katika baadhi ya maeneo ya sekta
ardhi ikiwemo uingizaji wamiliki wa viwanja na mashamba katika mfumo na
amemuahidi Dk Mabula kuwa suala la hati za madai nalo atalisimamia kikamilifu
ilii liweze kutekelezwa.
Alisema, changamoto kubwa inayoikabili
halmashauri ya wilaya ya Muheza ni kukosekana watendaji wa sekta ya ardhi wenye
uwezo mkubwa wa kusimamia masuala ya ardhi na kubainisha kuwa mbali na mkuu wa
idara aliyepo sasa lakini halmashauri hiyo haina watendaji wa kutosha.
------------MWISHO----------
No comments:
Post a Comment