Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati Serikali Kuu ikijitahidi kuondoa tofauti ya
Kimaendeleo baina ya Visiwa Vikubwa na Vidogo Wananchi wanapaswa kukataa
ushawishi unaofanywa na baadhi ya Watu wa kuwataka waache kutumia huduma za
maendeleo zinazoimarishwa na Serikali kila kukicha.
Alisema upuuzi wa Watu hao kamwe
hautaleta maana yoyote kwa vile Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayosimamiwa na
Serikali zote mbili Nchini Tanzania imeahidi kuleta mabadiliko makubwa ya
Maisha kwa kila Mwananchi bila ya kujadi utofauti wao wa Majimbo, Dini na hata
itikadi za Kisiasa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli
hiyo wakati wa hafla ya kuzindua Mradi wa huduma za Umeme katika Historia
ya Kisiwa kidogo cha Uvinje kilioko Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni shamra
shamra za Maadhimisho ya kusherehekea kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema kila Mwananchi wa Visiwa vya
Unguja na Pemba ana haki ya kupatiwa huduma muhimu za Kijamii, bila ya
kujali anakotoka hata kama ataamua kuishi kwenye Visiwa vidogo vidogo atakuwa
na haki ya kupata huduma hizo kwa faid ya ustawi wake na familia yake.
Balozi Seif aliwataka Wananchi wa
Kisiwa cha Uvinje kuelewa kwamba kupelekewa Maendeleo katika Visiwa vidogo
vidogo sio kazi ya kubahatisha kama kupiga ramli bali ni mkataba uliowekwa na
Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya Wananchi wa kuwatekelezea matakwa yao kwa
Mujibu wa Ilani yake.
“ Tofauti ya Chama chetu na vyama
vyengine ni kuwa sisi tunatekeleza ahadi zetu bila ya ubaguzi hata katika
Majimbo ambayo Wananchi wake walio wengi kwenye Majimbo hayo hawakuipigia Kura
Chama cha Mapinduzi”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alisisitiza kwamba
kitendo cha kusambazwa huduma za Umeme katika maeneo mbali mbali Nchini ni
hatua muhimu itakayowezesha kufungua milango zaidi ya Maendeleo
yanayomtoa mtu kwenye Umaskini na kumfanya aweze kumudu vyema maisha yake ya
kila siku.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwapongeza Wananchi wa Kisiwa cha Uvinje kwa kuweka rekodi ya nyumba zao
kuungiwa Huduma ya Umeme katika kipindi kifupi ikilinganishwa na Visiwa
vyengine vidogo ambavyo tayari vimeshafikiwa na huduma hiyo muhimu.
Alielezea faraha yake kutokana na
nyumba zipatazo 77 kati ya 92 sawa na asilimia 92% zimeshaunganishwa na huduma
za Umeme rekodi waliyoivunja ni kubwa ikionyesha walivyojipanga katika
kujiletea mabadiliko kwenye maisha yao ya kila siku.
Balozi Seif alisema Wananchi wa
Kisiwa hicho hivi sasa wako katika muelekeo wa kutumia huduma za Umeme jambo
ambalo wanapaswa kuwa makini katika matumizi ya huduma hiyo kwa vile inaweza
kuleta athari iwapo wataitumia visivyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwashukuru Wananchi hao kwa uungwana wao wa kuistahamilia
Serikali katika kipindi kirefu huku ikitafakari na kutafuta njia ya
kuitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto hiyo.
Alisema ustahamilivu wao umeipa moyo
mkubwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakionyesha kwamba wanafahamu
dhamira ya Taifa ya kusambaza Maendeleo kila kona ya Zanzibar hata kama
yanachelewa.
Akitoa Taarifa ya kitaalamu kuhusiana
na mradi huo wa huduma za Umeme Kisiwa cha Uvinje, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Adhi, Nyumba, Maji na Nishati Nd. Tahir Abdullah alisema Mradi huo umekamilika
baada ya kumaliza kazi ya ulazaji wa Waya, njia Kuu ya Umeme pamoja na ufungaji
wa Transfoma.
Nd. Tahir alisema kukamilika kwa
Mradi huo kumetoa fursa kwa Wananchi wa Visiwa Vinane vidogo vidogo vya
Zanzibar kuanza kufaidika na huduma hiyo kazi iliyosimamiwa na kutekelezwa
vyema na Wafanyakazi pamoja na Wahandishi wenyewe wa Shirika la Umeme Zanzibar
{ZECO}.
Alisema huduma za Umeme katika Visiwa
vya Unguja na Pemba hivi sasa imeshafikia asilimia 92% ambapo Wizara
inayosimamia nishati hiyo imekusudia kukamilisha maeneo yaliyobaki itakapofikia
Mwaka 2020 kwa Unguja na Mwaka 2022 kwa Kisiwa cha Pemba.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba Maji na Nishati alifahamisha kwamba ustawi wa Jamii na Maendeleo
ya Wananchi yataongezeka mara dufu kufuatia uimarishaji wa Miundombinu ya
Huduma za Umeme ambao kwa sasa si anasa tena.
Mapema Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji
na Nishati Zanzibar Mh. Salama Aboud Talib alisema Wananchi wa Kisiwa cha
Uvinje wamehamasika kutokana na uwepo wa huduma za Umeme katika Kisiwa
hicho.
Waziri Salama alisema katika kuunga
mkono hamasa hiyo amelazimika kutoa upendeleo maalum wa Kaya 15 zilizobakia
Kisiwani humo zijitokeze kupeleka maombi yao shirika la Umeme kwa malipo ya
shilingi 50,000/- za kuungiwa umeme ili nao wafaidike na huduma hiyo muhimu.
Mh. Salama amewashukuru na
kuwapongeza Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Zanzibar kwa kazi kubwa
waliyoifanya ya kusambaza huduma ya Umeme kwa zaidi ya Shehia 36 ndani ya
Wilaya ya Wete na kubakisha Vijiji Kumi tu kupatiwa nyenzo hiyo.
Katika kuunga mkono Wananchi hao wa
Kisiwa cha Uvinje Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Nd. Juma
Abdullah Saadala ameahidi kulipatia Shirika la Umeme Zanzibar shilingi Laki
750,000/- zitakazolenga kuwasaidia Wananchi wa Kaya 15 zilizobakia ndani ya
Kisiwa hicho waungiwe huduma hiyo.
Jumla ya shilingi za Kitanzania
Milioni Mia Sita na Hamsini zimetumika katika kukamilisha Mradi wa Huduma za
Umeme ndani ya Kisiwa cha Uvinje uliotokea katika Kisiwa cha Fundo.
0 comments:
Post a Comment