Tuesday, January 8, 2019

BALOZI SEIF ASEMA SERIKALI HAINA UBAGUZI





Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati Serikali Kuu ikijitahidi kuondoa tofauti ya Kimaendeleo baina ya Visiwa Vikubwa na Vidogo Wananchi wanapaswa kukataa ushawishi unaofanywa na baadhi ya Watu wa kuwataka waache kutumia huduma za maendeleo zinazoimarishwa na Serikali kila kukicha.
Alisema upuuzi wa Watu hao kamwe hautaleta maana yoyote kwa vile Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayosimamiwa na Serikali zote mbili Nchini Tanzania imeahidi kuleta mabadiliko  makubwa ya Maisha kwa kila Mwananchi bila ya kujadi utofauti wao wa Majimbo, Dini na hata itikadi za Kisiasa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kuzindua Mradi wa huduma za Umeme katika  Historia ya Kisiwa kidogo cha Uvinje kilioko Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni shamra shamra za Maadhimisho ya kusherehekea kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema kila Mwananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba  ana haki ya kupatiwa huduma muhimu za Kijamii, bila ya kujali anakotoka hata kama ataamua kuishi kwenye Visiwa vidogo vidogo atakuwa na haki ya kupata huduma hizo kwa faid ya ustawi wake na familia yake.
Balozi Seif aliwataka Wananchi wa Kisiwa cha Uvinje kuelewa kwamba kupelekewa Maendeleo katika Visiwa vidogo vidogo sio kazi ya kubahatisha kama kupiga ramli bali ni mkataba uliowekwa na Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya Wananchi wa kuwatekelezea matakwa yao kwa Mujibu wa Ilani yake.
“ Tofauti ya Chama chetu na vyama vyengine ni kuwa sisi tunatekeleza ahadi zetu bila ya ubaguzi hata katika Majimbo ambayo Wananchi wake walio wengi kwenye Majimbo hayo hawakuipigia Kura Chama cha Mapinduzi”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alisisitiza kwamba kitendo cha kusambazwa huduma za Umeme katika maeneo mbali mbali Nchini ni hatua muhimu itakayowezesha kufungua  milango zaidi ya Maendeleo yanayomtoa mtu kwenye Umaskini na kumfanya aweze kumudu vyema maisha yake ya kila siku.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi wa Kisiwa cha Uvinje kwa kuweka rekodi ya nyumba zao kuungiwa Huduma ya Umeme katika kipindi kifupi ikilinganishwa na Visiwa vyengine vidogo ambavyo tayari vimeshafikiwa na huduma hiyo muhimu.
Alielezea faraha yake kutokana na nyumba zipatazo 77 kati ya 92 sawa na asilimia 92% zimeshaunganishwa na huduma za Umeme rekodi waliyoivunja ni kubwa ikionyesha walivyojipanga katika kujiletea mabadiliko kwenye maisha yao ya kila siku.
Balozi Seif  alisema Wananchi wa Kisiwa hicho hivi sasa wako katika muelekeo wa kutumia huduma za Umeme jambo ambalo wanapaswa kuwa makini katika matumizi ya huduma hiyo kwa vile inaweza kuleta athari iwapo wataitumia visivyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru Wananchi hao  kwa uungwana wao wa kuistahamilia Serikali  katika kipindi kirefu huku ikitafakari na kutafuta njia ya kuitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto hiyo.
Alisema ustahamilivu wao umeipa moyo mkubwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  wakionyesha kwamba wanafahamu dhamira ya Taifa ya kusambaza Maendeleo kila kona ya Zanzibar hata kama yanachelewa.
Akitoa Taarifa ya kitaalamu kuhusiana na mradi huo wa huduma za Umeme Kisiwa cha Uvinje, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Adhi, Nyumba, Maji na Nishati Nd. Tahir Abdullah alisema Mradi huo umekamilika baada ya kumaliza kazi ya ulazaji wa Waya, njia Kuu ya Umeme pamoja na ufungaji wa Transfoma.
Nd. Tahir alisema kukamilika kwa Mradi huo kumetoa fursa kwa Wananchi wa Visiwa Vinane vidogo vidogo vya Zanzibar kuanza kufaidika na huduma hiyo kazi iliyosimamiwa na kutekelezwa vyema na Wafanyakazi pamoja na Wahandishi wenyewe wa Shirika la Umeme Zanzibar {ZECO}.
Alisema huduma za Umeme katika Visiwa vya Unguja na Pemba hivi sasa imeshafikia asilimia  92% ambapo Wizara inayosimamia nishati hiyo imekusudia kukamilisha maeneo yaliyobaki itakapofikia Mwaka 2020 kwa Unguja na Mwaka 2022 kwa Kisiwa cha Pemba.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba Maji na Nishati alifahamisha kwamba ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Wananchi yataongezeka mara dufu kufuatia uimarishaji wa Miundombinu ya Huduma za Umeme ambao kwa sasa si anasa tena.
Mapema Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Zanzibar Mh. Salama Aboud Talib alisema Wananchi wa Kisiwa cha Uvinje  wamehamasika kutokana na uwepo wa huduma za Umeme katika Kisiwa hicho.
Waziri Salama alisema katika kuunga mkono hamasa hiyo amelazimika kutoa upendeleo maalum wa Kaya 15 zilizobakia Kisiwani humo zijitokeze kupeleka maombi yao shirika la Umeme kwa malipo ya shilingi 50,000/- za kuungiwa umeme ili nao wafaidike na huduma hiyo muhimu.
Mh. Salama amewashukuru na kuwapongeza Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Zanzibar kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kusambaza huduma ya Umeme kwa zaidi ya Shehia 36 ndani ya Wilaya ya Wete na kubakisha Vijiji Kumi tu kupatiwa nyenzo hiyo.
Katika kuunga mkono Wananchi hao wa Kisiwa cha Uvinje Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Nd. Juma Abdullah Saadala ameahidi kulipatia Shirika la Umeme Zanzibar shilingi Laki 750,000/- zitakazolenga kuwasaidia Wananchi wa Kaya 15 zilizobakia ndani ya Kisiwa hicho waungiwe huduma hiyo.
Jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni Mia Sita na Hamsini zimetumika katika kukamilisha Mradi wa Huduma za Umeme ndani ya Kisiwa cha Uvinje uliotokea katika Kisiwa cha Fundo.

No comments:

Post a Comment