Tarehe 29 Desemba 2018 Taasisi ya Kijana Initiative Foundation imeungana na familia mia moja (100) zinazoishi katika mazingira magumu wakiwemo wajane pamoja na wanawake wajasiriamali wadogo kubadilishana mawazo na kula chakula cha pamoja katika ukumbi wa Chuo Kikuu Cha Jordan mkoani Morogoro.
Katika hafla hiyo Iliyojumuisha Viongozi mbalimbali ilihudhuriwa na Ndg Shaka Hamdu Shaka Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro akiwa ndiye Mgeni rasmi pamoja Ndg Said Said Nguya mdau wa maendelea na Afisa wa CCM aliyehudhuria kama mgeni mzungumzaji, wanawake wajasiriamali pamoja na familia zinazoishi katika mazingira magumu zimeonesha furaha ya wazi kwa msaada mkubwa wanaoupata.
Katika Hafla hiyo Ndg Shaka amsisitiza kuwa kama Chama Mkoa wa Morogoro watahakikisha wanawake hao wajasiriamali wanapata mitaji zaidi ili kuondokana na utegemezi kama ilivyokuwa sasa.
"Hii taasisi ya Kijana Initiative foundation inafanya kazi nzuri sana, mimi ninawaunga mkono na wakati wote waje ofisini kwangu nitawasaidia kwa kadri itakavyowezekana kwa sababu haya yote wanafanya wanatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, tunahitaji Taasisi kama hizi zinazogusa maisha ya watu na tutahakikisha wanawake hawa wanapata mikopo". Shaka amesisitiza.
Katika hatua nyingine Ndg Said Said Nguya akiongea katika hafla hiyo, amesema, "Hawa ni wananchi wanyonge, na Rais Magufuli hawa ndio watu ambao kila siku anawatetea ili wajikwamue kutoka hapa walipo, naomba muendelee kuwasaidia zaidi na zaidi ili watoto hawa katika familia hizi waje kuwa tegemeo kwa Taifa letu, pale mnapokwama ama kukwamishwa na mtu yeyote kwa matakwa yake, kimbilio lenu ni Chama Cha Mapinduzi."
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Ndg Grace Meena kwa kushirikiana na Mgeni Rasmi wamegawa Vifaa mbalimbali vya shule ikiwemo Madaftari, kalamu, na sare kwa watoto kutoka familia hizo na kuweka bayana mpango wao wa kuwatafutia mitaji familia hizi ili zijikwamue katika hali walionayo sasa.
Wageni wengine waliohudhuria katika hafla hiyo ni pamoja na Katibu wa Vijana Mkoa wa Morogoro Ndg Isack Kalaiya na Muwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Ambapo wote kwa pamoja wameonesha kuguswa na changamoto za familia hizi na kuahidi kutoa ushirikiano wa usaidizi ili zijikwamue kutoka hapa zilipo sasa.
Imetolewa na,
Afisa habari
Kijana Initiative Foundation
Morogoro
0 comments:
Post a Comment