Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ( wa pili toka kulia) akipewa maelezo ya kitaalamu juu ya matumizi ya vifaa tiba vilivyotolewa na mradi wa Uzazi Salama na mmoja wa wawakilishi wa mradi huo (wa kwanza Kulia).
Mradi wa uzazi salama Mkoani Rukwa
umekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi 211,145,850/= kwa ofisi
ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa ili kuvisambaza katika vituo 198 vya kutolea huduma za
afya, ikiwa ni muendelezo wa jitihada na dhamira yao ya kuhakikisha
wanashirikiana na Mkoa katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto katika
Mkoa.
Mradi huo unaoundwa kwa ushirikiano wa
mashirika matatu ya Plan International Tanzania, AFRICARE na JHPIEGO kwa
ufadhili wa serikali ya watu wa Canada umekabidhi vifaa hivyo vikiwemo vitanda
vya kujifungulia, vifaa vya upasuaji kwa kinamama wajawazito, vifaa vya
kumsaidia mtoto mchanga na mama kupumua, vifaa vya kuwasaidia watoto njiti,
majokofu ya kuhifadhia damu na vifaa vya kufanyia tathmini ya hali ya lishe kwa
watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanaratibu kufanyika
kwa siku ya afya kwa mwaka mara moja kwa kila kijiji na kuwataka wakuu wa
wilaya wasimamie zoezi hilo. Na kuwaomba wanaume, wazee na viongozi wote wa
dini pamoja na vijiji kutambua jukumu la afya ya uzazi na mtoto pamoja na
familia ni la wote na sio la kinamama na wanawake peke yao.
“Viongozi wa serikali katika ngazi za vijiji na
kata wanao wajibu wa kuhakikisha akina mama wanahudhuria katika vituo vya afya
pindi wanapojigundua ni wajawazito kwa huduma na ushauri wa kiafya. Tuwe mstari
wa mbele kuelimisha wengine hasa vijana wetu kuhusu afya ya uzazi na
kuwasisitiza kushiriki katika matukio mbalimbali yahusuyo afya kama huduma
rafiki kwa vijana na siku ya afya ya kijiji “village health day” yanayoratibiwa
na mradi wa Uzazi Salama.”
Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Plan International
Tanzania Paul Lusato aliziomba halmashauri pamoja na vituo vinavyotoa huduma za
afya vitakavyopatiwa vifaa hivyo kuhakikisha wanavitunza vizuri ili kuendelea
kutoa huduma tarajiwa kwa wananchi.
“Tunashauri pia viongozi katika ngazi ya mkoa
kuendelea kutembelea maeneo ambayo wadau mbalimbali wa maendeleo wametoa msaada
ili kujiridhisha kuwa uwekezaji uliofanywa unathaminiwa na kutunzwa na kuwa na
manufaa yaliyotarajiwa,” Alibainisha.
Awali akitoa taarifa ya huduma za afya ya uzazi na
mtoto Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alieleza kuwa katika
kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2018 tayari kina mama 39 wameshapoteza
maisha kutokana na matatizo ya uzazi ambayo ni sawa na uwiano wa vifo 97 kati
ya vizazi hai 100,000 huku watoto wachanga 537 wakipoteza maisha kwa kipindi
hicho hicho ambao ni sawa na uwiano wa vifo 14 katika kila vizazi hai 1000.
Makabidhiano hayo yamefanyika pamoja na uzinduzi wa
kampeni inayojulikana kwa jina la “JIONGEZE TUWAVUSHE SALAMA”katika
Mkoa wa Rukwa, Kampeni ambayo ilizinduliwa kitaifa tarehe 6 Novemba, 2018
na Mh.Samia Suluhu Hassani, Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inayolenga kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto
wachanga nchini Tanzania.
0 comments:
Post a Comment