METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, December 20, 2018

MHE. SAMIA AJITAMBULISHA KAMA MLEZI WA CCM MKOA WA PWANI


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Taifa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wajumbe wa kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani mara baada ya kujitambulisha rasmi kama Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Pwani, hafla hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji Kibaha. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ndugu Ramadhani Maneno (kulia) akimtambulisha Mlezi wa CCM mkoa huo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani, kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kutumia fedha za ndani zaidi kwenye shughuli za kimaendeleo kuliko kutegemea misaada.

Mhe. Samia ameyasema hayo leo mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Pwani kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Kibaha.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alijitambulisha rasmi kama mlezi wa CCM mkoa wa Pwani na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha .

Akizungumza na Wajumbe hao Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa Chama mkoani hapo kuhakikisha mali zote za Chama zinaleta tija kwa Chama.

“Sasa ni wakati umefika kuangalia mali zetu ndani ya Chama labda Wilaya ilikuwa inamiliki vitu gani? Viwanja vya kujenga nyumba au vya michezo mali zozote ni kuziweka vizuri na kuhakikisha zinazalisha kwa manufaa ya Chama.”

Mhe. Samia amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimejipanga kutoa mafunzo ya Uongozi katika ngazi mbali mbali ambapo yeye binafsi amepangiwa mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ambapo atashirikiana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndugu Rodrick Mpogolo.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Samia amewataka Viongozi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani kufanya kazi kwa Umoja na Ushirikiano ndani ya Chama pamoja na Serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Ndugu Ramadhani Maneno amemshukuru Mjumbe huyo wa Kamati Kuu kwa kuja kujitambulisha na kutoa muongozo mzuri uliokubalika na kila mjumbe na kuahidi kutoa ushirikiano mzuri kwa manufaa ya Chama Cha Mapinduzi.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com