METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, November 23, 2018

WAFANYABIASHARA WA UTURUKI WAONESHA NIA YA KUWEKEZA KATIKA KIWANDA CHA NGUO SIMIYU





Na Stella Kalinga, Simiyu

Wafanyabiashara kutoka nchini Uturuki wameonesha nia na dhamira ya kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nguo mkoani Simiyu ambacho kitakuwa na uwezo wa kuajiri watu zaidi ya 4000.

 Hayo yamebainishwa katika kikao kati ya Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo ambaye aliambatana na Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na mwakilishi wa Wafanyabiashara wa Uturuki kutoka makampuni saba ya nchi hiyo, katika kikao maalum na viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Wakuu wa Taasisi mbalimbali na jumuiya ya wafanyabiashara ya mkoa wa Simiyu, kilichofanyika Novemba 22, 2018 Mjini Bariadi.

Balozi Kiondo amesema Wafanyabiashara hao wanayo azma ya kuwekeza katika kiwanda cha kutengeneza nguo katika mnyororo mzima wa utengenezaji kutoka bidhaa ya awali ya pamba mpaka bidhaa ya mwisho kabisa, ambayo ni nguo kwa ubia(partineship) na Watanzania.

Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara kutoka Uturuki, Bw. Cengiz ERTAS amesema  mpaka sasa ni makampuni sita kutoka nchini humo yameonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha nguo mkoani Simiyu na akaahidi kwenda kuwashawishi wafanyabiashara wenzake hivyo watakaporudi kwa mara nyingine  makapuni mengi yatakuja kuwekeza katika viwanda vya nguo.

“Nikirudi nyumbani kama kiongozi wa wafanyabiashara nitawashawishi wengine pia waje wawekeze katika viwanda vya nguo,ombi langu kwenu ni kwamba ninahitaji Mfanyabiashara Mtanzania ambaye tutashirikiana naye katika uwekezaji huu(partinership), lakini niwahakikishie tu kuwa katika kiwanda tutakachojenga mashine na vifaa vyote vipo tayari kule Uturuki” alisema  Cengiz.

 Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka amewahakikishia wafanyabiashara hao upatikanaji wa soko la uhakika la nguo zitakazotengenezwa, pamoja na upatikanaji wa malighafi kwa kuwa Simiyu ndiyo mkoa unaozalisha zaidi ya asilimia 55 ya pamba yote nchini, ambapo kwa  mwaka 2018 Simiyu imezalisha takribani kilo milioni 131.

Ameongeza kuwa pamoja na uhakika wa soko na malighafi  Simiyu ina viwanda vingi  vya kuchambua pamba, ardhi itatolewa bure, miundombinu muhimu yote ipo, utashi wa kisiasa kwa viongozi wa wilaya upo, hivyo akawatoa hofu wawekezaji hao na kuwaeleza kuwa mkoa utashirikiana nao, huku akiomba waone uwezekano wa kuwekeza katika uongezaji thamani wa mazao ya mifugo kama ngozi na nyama

Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery, Bw. Boaz Ogola amesema wako tayari kushirikiana na mwekezaji huyo, huku akibainisha kuwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho kitawasaidia wanaochambua pamba na wakulima kupata faida ikilinganishwa na sasa ambapo zaidi ya asilimia 75 ya pamba inasafirishwa nje ya nchi.

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu, Mhe. Najlu Silanga ameahidi ushirikiano kwa wawekezaji aho kutoka Uturuki na kuiomba Wizara ya Viwanda, Baiashara na Uwekezaji kuzitambu na kusughuliakia changamoto mbalimbali za wafanyabiashara hapa nchini .

Wakati huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda  (TIRDO) Prof. Mkumbukwa Mtambo amepongeza Mkoa wa Simiyu kwa kuzingatia Utafiti na maendeleo katika Viwanda, huku akisisitiza kuwa ili viwanda vinavyoanzishwa viweze kuwa endelevu ipo haja ya kufanya utafiti na maendeleo na akaahidi kuwa Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Simiyu katika tafiti mbalimbali  za  maendeleo ya viwanda
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com