METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, November 23, 2018

WAZIRI KAIRUKI AAHIDI KUSAIDIA UENDELEZAJI MADINI YA NIKEL NA CHUMVI SIMIYU





Na Asteria Muhozya, Bariadi

Waziri wa Madini Angellah Kairuki  ametembelea Kituo cha Umahiri cha Bariadi ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kumhaidi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka kuwa, Wizara  ya Madini itaangalia namna ya kuusaidia mkoa huo katika uendelezaji wa madini ya Nikel na chumvi yanayopatikana mkoani humo.

Pia, Waziri Kairuki ametoa pongezi kwa Mkandarasi SUMAJKT anayejenga kituo hicho  kwa kazi iliyofanyika na kumtaka mkandarasi huyo kuzingatia muda wa kukamilisha ujenzi na ubora wake.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuridhia kuondoa tozo 9 kati ya 16 zilizokuwa zikitozwa na Taasisi mbalimbali  za serikali  katika Sekta ya Madini.

Amesema uwepo wa kituo hicho mkoani humo, utawezesha wachimbaji wadogo  wa madini kuchimba kwa tija.

Pia, ametoa rai kwa wananchi walio tayari kuwekeza katika Sekta ya Madini kuwekeza mkoani humo pamoja na maeneo mengine nchini.

Vilevile, amewataka wale wenye leseni za madini kutoshikilia leseni hizo bila  kuziendeleza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka, ameishukuru Wizara kwa kuuchagua mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa ambayo vituo hivyo vya umahiri vinajengwa.

Amesema  kuwa, uwepo wa kituo hicho utawezesha wachimbaji kupata mafunzo ya uchimbaji bora wenye tija  ikiwemo kupata mahali sahihi ambapo shughuli za uendelezaji Sekta ya Madini utafanyika.

Aidha, ameleeza pia, kituo hicho kitatumika kama sehemu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi ikiwemo  taarifa kuhusu bei elekezi ambazo wizara kupitia Tume ya Madini imekua ikitoa kila mwezi.

Vituo vya Umahiri vinajengwa na mkandarasi kampuni ya SUMAJKT maeneo mbalimbali nchini, kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia.

 Vituo hivyo vya umahiri vinalenga kutoa mafunzo ya jiolojia katika utafiti, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususan kemikali zisizotumia zebaki.

Pia, vinalenga katka kutoa mafunzo ya biashara kwa wachimbaji wadogo, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo bora za utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji.

Mbali na Bariadi, kituo kama hicho kinachojengwa Bukoba, Mara, Chunya, Handeni, Songea, na Chuo Cha Madini Dodoma.

Wakati huo huo, Waziri Kairuki jana alitembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Handeni. Akiwa kituoni hapo, Waziri Kairuki alisema wizara inaendelea kuweka jitihada kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia zaidi katika pato la taifa  na hivyo kuwataka watumishi katika sekta husika kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa weledi na kuongeza kuwa,“ mjue kuwa kosa moja mtakalofanya katika sekta hii, linawakosesha watanzania wote manufaa.

Aliongeza kuwa, hatosita kumwondoa afisa yoyote atakayekwamisha  kazi ya serikali na watanzania na kueleza kuwa, bado analikumbushia suala hilo kwa kuwa ni wajibu wake na kusema kuwa, ni vema watumishi katika sekta ya madini kuongeza nguvu  katika utendaji kazi na kuhakikisha kuwamba wanatoa kipaumbele kwa rasilimali hiyo ya madini.

“ Mwaka huu tumewekewa malengo ya kukusanya shilingi bilioni  310, natamani tufike makusanyo ya shilingi bilioni 500. Nitawapima Maafisa Maadini kwa hayo. Sitasita kuchukua hatua kwa wanaolegalega,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Pia, alizungumzia kuhusu wamiliki wa leseni na kueleza kuwa, wote wanaomikili leseni hizo wanapaswa kuziendeleza badala ya kuzihodhi bila kuzifanyia kazi na kusema kuwa “ lengo letu ni kuhakikisha kwamba leseni zinachangia  katika upatikanaji wa mapato,” alisema Kairuki,

Aidha, alieleza kwamba, Serikali kupitia Wizara ya madini inaandaa Jukwaa la uwekezaji kati ya nchi ya China na Tanzania ambalo linatarajiwa kufanyika mwezi Disemba na hivyo kutoa wito kwa wadau wa sekta ya madini kuchangamkia fursa hiyo.

Pia, aliendelea kusisitiza kuhusu wadau wa sekta ya madini kufuata sheria na kuzingatia taratibu zilizopo wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe, alisema kuwa, uwepo wa kituo hicho katika wilaya hiyo kutakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi wilyani humo na hivyo kutoa wito kwa wale wenye ni ya kufanya biashara ya madini wilayani humo kutosita kufanya hivyo.

Alisema Wilaya hiyo itasimamia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kutokana na manufaa yake kwa wilaya hiyo na kueleza kuwa, wilaya hiyo ni mzalishaji mkubwa wa madini ya viwandani hivyo uwepo wa kituo hicho kitahamasisha wawekezaji zaidi kuwekeza wilayani humo.

Mwisho alimtaka Mkandarasi SUMAJKT kuharakisha ujenzi huo kabla ya msimu wa mvua na kumwomba Waziri Kairuki kuhakikisha  kusaidia upatikanaji wa haraka wa fedha za ujenzi.

Xxxxxxx        xxxxxxx        xxxxxxx        xxxxxxx        xxxxxxx        xxxxxx

PICHA  BARIADI  1

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia matofali yanayotumika kujenga Kituo cha Umahiri cha Bariadi, alipokitembelea kituo hicho ili kukagua maendeleo ya ujenzi wake. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka.



PICHA BARIADI 2
Sehemu ya jengo la Kituo cha Umahiri Bariadi katika hatua zake za ujenzi.

PICHA  BARIADI 3
Waziri wa Madini  Angellah Kairuki na Mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka wakimsikiliza Mkandarasi  SUMAJKT (hayupo) akieleza maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Umahiri cha Simiyu. Waziri Kairuki alitembelea kituoni hapo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo husika.


BARIADI 4
Waziri wa Madini Angellah katika picha ya pamoja katika Kituo cha Umahiri kinachojengwa Bariadi na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Athony Mtaka, Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Ofisi ya Madini , Mkandarasi SUMAJKT  na Uongozi wa Mkoa huo


PICHA HANDENI 1
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimsikiliza Mkandarasi SUMAJKT anayejenga kituo cha Umahiri cha Handeni akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho. Anayefuatilia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe , uongozi wa Mkoa, watalaam wa Ofisi ya Madini Handeni na Tanga na watalaam kutoka Wizara ya Madini.

PICHA HANDENI 2 & 3
Mafundi wa SUMAJKT wakiendelea na ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Handeni.


PICHA 4
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe, akimtambulisha waziri wa Madini Angellah Kairuki kwa viongozi wa Wilaya alipofika wilayani humo kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri kinachojengwa Handeni.




Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com