Na Stella Kalinga, Simiyu
Wafanyabiashara
kutoka nchini Uturuki wameonesha nia na dhamira ya kuwekeza katika ujenzi wa
kiwanda cha kutengeneza nguo mkoani Simiyu ambacho kitakuwa na uwezo wa kuajiri
watu zaidi ya 4000.
Hayo
yamebainishwa katika kikao kati ya Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mhe. Prof.
Elizabeth Kiondo ambaye aliambatana na Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na
mwakilishi wa Wafanyabiashara wa Uturuki kutoka makampuni saba ya nchi hiyo,
katika kikao maalum na viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Wakuu wa Taasisi mbalimbali
na jumuiya ya wafanyabiashara ya mkoa wa Simiyu, kilichofanyika Novemba 22,
2018 Mjini Bariadi.
Balozi
Kiondo amesema Wafanyabiashara hao wanayo azma ya kuwekeza katika kiwanda cha
kutengeneza nguo katika mnyororo mzima wa utengenezaji kutoka bidhaa ya awali
ya pamba mpaka bidhaa ya mwisho kabisa, ambayo ni nguo kwa ubia(partineship) na
Watanzania.
Rais
wa Jumuiya ya Wafanyabiashara kutoka Uturuki, Bw. Cengiz ERTAS amesema
mpaka sasa ni makampuni sita kutoka nchini humo yameonesha nia ya
kuwekeza katika kiwanda cha nguo mkoani Simiyu na akaahidi kwenda kuwashawishi
wafanyabiashara wenzake hivyo watakaporudi kwa mara nyingine makapuni
mengi yatakuja kuwekeza katika viwanda vya nguo.
“Nikirudi
nyumbani kama kiongozi wa wafanyabiashara nitawashawishi wengine pia waje
wawekeze katika viwanda vya nguo,ombi langu kwenu ni kwamba ninahitaji
Mfanyabiashara Mtanzania ambaye tutashirikiana naye katika uwekezaji
huu(partinership), lakini niwahakikishie tu kuwa katika kiwanda tutakachojenga
mashine na vifaa vyote vipo tayari kule Uturuki” alisema Cengiz.
Mkuu
wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka amewahakikishia wafanyabiashara hao upatikanaji
wa soko la uhakika la nguo zitakazotengenezwa, pamoja na upatikanaji wa
malighafi kwa kuwa Simiyu ndiyo mkoa unaozalisha zaidi ya asilimia 55 ya pamba
yote nchini, ambapo kwa mwaka 2018 Simiyu imezalisha takribani kilo
milioni 131.
Ameongeza
kuwa pamoja na uhakika wa soko na malighafi Simiyu ina viwanda
vingi vya kuchambua pamba, ardhi itatolewa bure, miundombinu muhimu yote
ipo, utashi wa kisiasa kwa viongozi wa wilaya upo, hivyo akawatoa hofu
wawekezaji hao na kuwaeleza kuwa mkoa utashirikiana nao, huku akiomba waone
uwezekano wa kuwekeza katika uongezaji thamani wa mazao ya mifugo kama ngozi na
nyama
Mkurugenzi
wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliance Ginnery, Bw. Boaz Ogola amesema
wako tayari kushirikiana na mwekezaji huyo, huku akibainisha kuwa kuanzishwa
kwa kiwanda hicho kitawasaidia wanaochambua pamba na wakulima kupata faida
ikilinganishwa na sasa ambapo zaidi ya asilimia 75 ya pamba inasafirishwa nje
ya nchi.
Naye
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu, Mhe. Najlu Silanga ameahidi
ushirikiano kwa wawekezaji aho kutoka Uturuki na kuiomba Wizara ya Viwanda,
Baiashara na Uwekezaji kuzitambu na kusughuliakia changamoto mbalimbali za
wafanyabiashara hapa nchini .
Wakati
huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) Prof. Mkumbukwa Mtambo amepongeza Mkoa wa Simiyu kwa kuzingatia Utafiti
na maendeleo katika Viwanda, huku akisisitiza kuwa ili viwanda vinavyoanzishwa
viweze kuwa endelevu ipo haja ya kufanya utafiti na maendeleo na akaahidi kuwa
Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Simiyu katika tafiti mbalimbali
za maendeleo ya viwanda
No comments:
Post a Comment