METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, November 21, 2018

Miradi mipya ya umeme ilenge maeneo yenye changamoto za upatikanaji umeme -Dkt Kalemani

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akiongoza kikao kati yake na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia kwa Waziri) pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati,  Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) ambacho kililenga  kupata taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa mijini na vijijini.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewataka wataalam wanaopanga maeneo yanayopaswa kupelekewa umeme kupitia miradi mbalimbali kuhakikisha kuwa wanakuwa makini katika upangaji wa maeneo hayo ili kutorundika miradi mingi katika maeneo ambayo tayari yameshasambaziwa umeme.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao chake na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati,  Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) ambacho kililenga  kupata taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa mijini na vijijini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara ya Nishati, Raphael Nombo ( amemwakilisha Katibu Mkuu), Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Eng. Innocent Luoga, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Eng. Amos Maganga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma.

“Kuna maeneo ambayo tayari yana umeme au kuna miradi kadhaa inayotekelezwa katika maeneo hayo hivyo kwa miradi tunayotaka kutekeleza sasa lazima tuweke msisitizo katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na nishati hiyo au hayajasambaziwa umeme kwa kiasi kikubwa,” alisema Dkt Kalemani.

Dkt. Kalemani alitoa kauli hiyo baada Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Eng. Amos Maganga  kueleza miradi mbalimbali ambayo ipo katika mchakato wa kutekelezwa ukiwemo wa kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme  (Densification) mzunguko wa pili  katika maeneo mbalimbali nchini na mradi wa usambazaji umeme wa awamu ya Tatu mzunguko wa pili.

Akielezea  kazi ya usambazaji umeme vijijini, Maganga alisema kuwa hadi kufikia Novemba 15, 2018, jumla ya vijiji  4,024  vimepatiwa umeme kupitia miradi ya REA ya Awamu ya Kwanza hadi Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza unaokamilika Juni 2019, mradi wa Makambako- Songea, Mradi wa umeme wa kV 400 wa Iringa hadi Shinyanga,  mradi wa Densification mzunguko wa kwanza na nishati jadidifu.

Kuhusu usambazaji umeme kwa kutumia nishati jadidifu, alisema kuwa vijiji 161 vimepangwa kupelekewa umeme kutokana na vyanzo hivyo ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba 2018 jumla ya vijiji 74 vimepatiwa umeme.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, alitaja miradi mbalimbali inayotekelezwa ambayo imelenga kuunganisha umeme Wilaya kwa Wilaya, kuboresha hali ya umeme na mingine ikilenga kupata wateja wapya.

Baadhi ya miradi aliyoitaja ni pamoja na ujenzi wa laini ya msongo wa 33kV kutoka Nanyumbu hadi Tunduru ambao umekamilika kwa asilimia 98 na sasa upo katika majaribio ya kuwashwa.

Mradi mwingine ni wa ujenzi wa laini ya msongo wa 33kV ambayo imekamilika kwa asilimia 100 na  kusambaza umeme katika eneo la kuchenjulia dhahabu mkoani Geita.

Aidha alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa laini ya msongo wa 19.13kV na ujenzi wa transfoma tano zenye ukubwa wa 50kVA katika vijiji vya Samaria, Bondani, Zaire, Savana na KKKT- Arusha mkoani Arusha  ambao umefikia asilimia 20.

Akitoa majumuisho ya Kikao hicho, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amezipongeza Taasisi hizo kwa kusimamia miradi mbalimbali lakini alitoa angalizo kuwa, Idara za manunuzi zisiwe vizingiti vya utekelezaji wa miradi, hivyo wahakikishe kuwa taratibu za manunuzi zinafanyika ndani ya muda muafaka.

Vilevile aliwataka TANESCO kupitia tena taratibu za uunganishaji umeme vijijini hasa katika viwanda kwani kumekuwa na malalamiko kuwa wananchi wanatozwa gharama kubwa hivyo kukwamisha juhudi za uanzishaji wa viwanda vijijini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka watendaji wa Taasisi hizo kuhakikisha kuwa wanaboresha miundombinu ya umeme katika maeneo yenye kasi ya ujenzi wa viwanda ili maeneo hayo yawe na umeme wa kutosha na wa uhakika.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com