Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Dkt. Bashiru Ally ametembelea maonesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa almaarufu Sabasaba yaliyopo katika viwanja vya Mwalimu Nyerere wilayani Temeke ili kujionea utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ulivyo kwenye maonesho hayo.
Dkt. Bashiru Ally alipokelewa na Naibu Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji Enjinia Stellah Manyanya na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Ndugu Edwin Rutageruka ambaye alizungushwa kwenye mabanda mbalimbali ya viwanjani hapo yakiwemo banda la NSSF, Banda la Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), banda la Chuo kikuu, banda la Bunge, banda la JKT, banda la Maliasili na utalii, banda la TBC, banda la Takukuru, Banda la Umoja wa wafanyabiashara wanawake Tanzania, banda la Watu wa Zanzibar pamoja na banda la kampuni ya simu la TTCL.
Katika majumuisho mara baada ya kutembelea maonesho hayo, Dkt. Bashiru Ally amesifu maonesho ya mwaka huu yamejaza Wafanyabiashara Wazalendo wengi, pia amefurahishwa na fursa mbalimbali za kiuchumi na ajira hali iliyompelekea kutamani maonesho hayo yafanyike na upande wa Zanzibar pia.
“Utekelezaji wa ilani ya uchaguzi umejionyesha dhahiri kwenye maonesho haya. Natamani na Watu wa Zanzibar nao pia wapate fursa ya kuwa na maonesho kama haya ili nao waweze kuona, kujifunza na kutanua wigo wa ajira na biashara. Natoa rai suala hili mlipokee na mlifanyie kazi pia” alisema Dkt. Bashiru Ally.
Pia Dkt. Bashiru amesifu utaratibu uliowekwa wa kuwa na matukio mbalimbali kila siku kwenye maonesho hayo. Matukio hayo ni kuwa na siku ya mazingira, rushwa, asali, sanaa na utamaduni ambayo yalishirikisha jumla ya Watu 2560.
“Malengo ya ilani ya uchaguzi yamejikita kwenye uchumi, ajira, rushwa na ufisadi pamoja na amani na usalama. Nawapongeza kwa kuwa na siku ya rushwa. Hongereni kwa kujumuika nasi kwenye kupambana na rushwa na kutangaza mafanikio ya mapambano hayo ya rushwa yanayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.
Katika msafara wake Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally aliambatana na Naibu Katibu Mkuu CCM, Ndugu Rodrick Mpogolo, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga, Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi Ndugu Erasto Sima, Katibu Mkuu Jumuiya ya Wanawake (UWT) Queen Mlozi, Katibu Mkuu Jumuiya ya Vijana (UVCCM) Mwl. Raymond Mwangwala pamoja na maofisa mbalimbali toka CCM Makao Makuu.
0 comments:
Post a Comment