WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka maafisa ushirika wawahimize wakulima wafungue akaunti benki ili kuepuka wizi wa fedha za vyamma vya msingi (AMCOS).
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Julai 7, 2018) wakati akizungumza na wanaushirika na mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini humo.
Amesema kumekuwa na wizi wa kupanga unaofanywa na watu wachache wasio waaminifu. "Kuna AMCOS walienda kuchukua sh. milioni 50 benki, wakaja nazo kwenye pikipiki, wakati wanafungua mlango na boksi la hela liko hapo chini, ikaja pikipiki nyingine na watu wawili wakabeba boksi na kupotea nalo."
"Sasa ujiulize hao waliokuja na pikipiki ya pili walijuaje kama wale wa mbele walikuwa na fedha? Mtu anaporwa hela yote hiyo hata mchubuko hana, hiyo siyo sahihi, hizo ni hela za Chama cha msingi tunapaswa kuzilinda," alisisitiza.
Aliwataka maafisa ushirika wakasimamie jukumu hilo ili fedha ikilipwa na mnunuzi baada ya mnada, meneja wa AMCOS anaenda benki anaingiza hela kwenye akaunti za wanachama wake mara moja.
"Hii itaondoa shaka ya wanachama kuibiwa fedha zao, itaondoa hatari ya maafisa wa vyama vya msingi kutembea na fedha nyingi za Chama, na kuepusha wizi usio wa lazima. Hivi sasa wakulima wengi wana simu za mkononi. Ni rahisi kwao kupata ujumbe mfupi wa maandishi kwamba kuna fedha imetumwa katika akaunti yako," alisema.
Alisema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwepo wa mfumo jumuishi wa huduma za kifedha (financial inclusion) ambao umesaidia kuwepo kwa mawakala wa kibenki hadi vijijini.
"Mkulima akitaka kuichukua fedha yake hana haja ya kusafiri hadi wilayani, sasa hivi anapata huduma hizo pale alipo kupitia kwa mawakala au kwenye mtandao wa simu," alisema.
Siku ya Ushirika Duniani huadhimishwa Jumamosi ya kwanza ya Julai kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Ushirika kwa ulaji wa uzalishaji endelevu wa bidhaa na huduma.”
MWISHO
0 comments:
Post a Comment