METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 11, 2018

"HAKUNA BEI NZURI YA KAHAWA-UGANDA" DKT TIZEBA

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akikisitiza jambo wakati akizungumza na wadau wa biashara ya Kahawa katika ukumbi wa Happiness Hoteli uliopo katika eneo la Mtukula Wilayani Misenyi, Leo 11 Julai 2018. (Picha zote Na Mathias Canal-WK)
Wadau wa biashara ya Kahawa wakifatilia mkutano wa Waziri wa Kilimo Mhe. dkt Charles Tizeba katika ukumbi wa Happiness Hoteli uliopo katika eneo la Mtukula Wilayani Misenyi, Leo 11 Julai 2018.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage akisalimiana na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano wa mawaziri wa nchi hizo mbili, mkutano uliohudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba, Leo 11 julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisalimiana na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano wa mawaziri wa nchi hizo mbili, mkutano uliohudhuriwa pia Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage, Leo 11 Julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati wa mkutano na Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume (Kushoto), Mwingine ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage (Katikati).

Na Mathias Canal-WK, Mtukula-Kagera

Imebainika kuwa bei ya uuzaji wa Kahawa nchini Uganda haina tofauti kubwa na bei ambayo ingepatikana nchini Tanzania endapo wakulima wangeuza Kahawa zao kwenye soko la awali jambo ambalo linawatoa wasiwasi wakulima wa Kahawa nchini waliokuwa wakidanganywa kuwa bei ya Uganda ni kubwa na yenye tija kwa wakulima kuliko hapa nchini.

Kilogramu moja ya Kahawa ya maganda nchini Uganda inanunuliwa kwa shilingi 2000 ya Uganda sawa na Shilingi 1400 za Kitanzania (exchange rate 1.7) kwa mfano hapa nchini Tanzania kwa wiki hii bei ya Kahawa kwa kilo moja ya maganda ni Shilingi 1460 ya bei elekezi ya chini ya kila wiki (Weekly minimum indicative price) inayotolewa na Bodi ya Kahawa kulingana na bei ya Kahawa katika soko la dunia. 

Hata hivyo, wakulima wa Tanzania watapata zaidi kwa kuuza mnadani moja kwa moja na kuachana na bei ya shambani kwa kutumia ushirika wao ambapo bei ya chini inayopatikana ni wastani wa Shilingi 1950 kabla ya gharama za uendeshaji. Kwa kuuza mnadani mkulima anapata bei kutokana na Ubora wa Kahawa yake na ikiwa kwenye madaraja na hivyo kutoa motisha kwa wakulima kuzalisha Kahawa bora kuliko kuuza ikiwa ghafi.

Hayo yamebainishwa leo 11 Julai 2018 na Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba wakati akizungumza na wadau wa biashara ya Kahawa katika ukumbi wa Happiness Hoteli uliopo katika eneo la Mtukula Wilayani Misenyi.

Dkt Tizeba amezungumza hayo ikiwa ni muda mchache tangu alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Biashara na Ushirika nchini Uganda Mhe Fredrick Ngobi Gume katika mkutano uliohudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage.

Mkutano huo ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 2 Julai 2018 na kuitaka Wizara ya Kilimo kufuatilia kwanini wakulima wa zao la Kahawa wanacheleweshewa malipo yao sambamba na kujua kwanini wakulima wanauza Kahawa yao nchini Uganda.

"Ndugu zangu kuna jambo hamlifahamu wale wanaosema Uganda bei ya Kahawa ni nzuri kuliko Tanzania wanawadanganya hakuna bei nzuri Kule kinachofanya watu kupeleka Kahawa Uganda ni kutokana na mikopo wanayokopeshana isiyo rasmi (Butura) hivyo makubaliano ya kurejesha mkopo yanakuwa na masharti magumu yanayowataka wakulima wa Kahawa nchini kulipa madeni kwa kupeleka Kahawa sio fedha" Alisisitiza Dkt Tizeba wakati akizungumza na wadau wa Kahawa eneo la Mtukula Wilayani Misenyi

Waziri wa biashara na ushirika nchini Uganda Mhe Fredric Ngobi Gume amemuhakikishia mwenyeji wake kuwa biashara ya Kahawa nchini humo ina changamoto sawa katika nchi zote mbili kwa kuwa swala la mikopo isiyo rasmi inayowanyonya wakulima (Butura) nchini Uganda ipo kwa kiwango cha juu kiasi kwamba ameomba kuja kuja nchini kwa miadi maalumu kwa minajili ya kujifunza kuhusu namna bora kuendesha ushirika na kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani.

Aidha, Gume alisema kuwa serikali ya Uganda inayoongozwa na Rais wa nchi hiyo Mhe Yoweri Kaguta Museveni itaendeleza ushirikiano na serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli hivyo panapohitajika ushirikishwaji katika biashara hususani kwenye sekta ya Kilimo watakuwa na msimamo wa pamoja.

Katika hatua nyingine pande zote mbili kutoka Tanzania na Uganda wameeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili mipaka ya nchi hizo ikiwemo biashara ya magendo inayofanyika huku wakiahidi kutokomeza kadhia hiyo.

MWISHO. 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com