Halmashauri ya manispaa ya Ilemela
imezindua majaribio ya mradi wa udhibiti majanga kielektroniki utakaotekelezwa
kuanzia June 01, 2018 na kugharimu zaidi ya dola milioni tano za kimarekani kwa
kushirikiana na jiji rafiki la Daegu la nchi ya Korea ya kusini, taasisi ya
Egis labs, shirika la teknolojia (NIPA) kwa ufadhili wa shirika la maendeleo la
nchi ya Korea kusini la KOICA.
Akizungumza katika uzinduzi huo
mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela Mheshimiwa Renatus Mulunga amesema kuwa
uzinduzi wa mradi huo umekuja wakati sahihi kwa manispaa yake kwani imekuwa
ikikabiliwa na majanga makubwa ya mafuriko na moto kwa baadhi ya maeneo yake
huku akiomba kurithishwa taaluma hiyo kwa wataalamu wake ili mradi huo uweze
kuwa endelevu
‘… Tunawashukuru sana wenzetu
kutoka nchini Korea, tunaamini mradi huu umekuja wakati sahihi kwani watu wetu
wamekuwa wakikabiliwa na majanga makubwa ya mafuriko kipindi cha mvua na moto
hivyo kuzinduliwa kwa mradi huu hivi leo kutaleta tija na chachu katika
kudhibiti majanga haya …’ Alisema
Kwa upande wake kiongozi wa
ugeni huo kutoka nchini Korea ya kusini ndugu Kim Dae Wuk mbali na
kufafanua juu ya umuhimu wa mradi huo kwa jamii katika udhibiti wa
majanga na utekelezwaji wake amewataka wataalam wa manispaa ya Ilemela na
viongozi wake kutoa ushirikiano ili kufanikisha mradi na kuwa endelevu.
Akihitimisha uzinduzi huo
mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela John Wanga mbali kuahidi ushirikiano na
kushukuru kwa kuanzishwa mradi huo ameongeza kuwa hayo ni matunda ya jitihada
za mbunge wa jimbo la Ilemela Mheshimiwa Daktari Angeline Mabula kama muasisi
wa ushirikiano na urafiki wa jiji la Daegu na manispaa ya Ilemela katika
shughuli mbalimbali za kijamii zenye lengo la kuwaletea wananchi unafuu wa
maisha na maendeleo.
Uzinduzi wa mradi huo
ulihudhuriwa na wataalam kutoka manispaa ya Ilemela, vyombo vya ulinzi na
usalama vya wilaya hiyo na viongozi mbalimbali.
' Ilemela ni yetu, tushirikiane
kuijenga'
0 comments:
Post a Comment