METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, May 6, 2018

​MAAMUZI YA RAIS YA KUUPANDISHA HADHI MJI WA DODOMA NA KUWA JIJI NI SAHIHI-MAJALIWA


Asisitiza kwamba hakuna sheria iliyokiukwa

WAZIRI MKUUKassim Majaliwa amesema maamuzi ya  Rais Dkt John Magufuli ya kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji ni sahihi na ameyafanya kwa wakati muafaka na hakuna sheria iliyokiukwa.

Aprili 26, 2018 Rais Dkt Magufuli aliupandisha hadhi mji wa Dodoma kutoka Halmashauri ya Manispaa na kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na kumteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Bw. Godwin Kunambi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 3, 2018) wakati akijibu swali la Bibi Felista Bura (Viti Maalumu) katika kipindi cha Maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma. Bibi Felistaalitaka kupata kauli ya Serikali juu ya baadhi ya watu wanaobeza maamuzi ya Rais Dkt. Magufuli ya kuupandisha hadhi mji wa Dodoma.

Amesema kuwa Rais Dkt Magufuli hakukiuka sheria kwa sababu ana mamlaka kwa mujibu wa katiba ibara 2 na sheria ya Mamlaka  ya Serikali za Mitaa sura ya 288 kupandisha hadhi mji au eneo lolote kadiri ya mahitaji yatakavyohitajika .

Waziri Mkuu amesema hata kitendo cha Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali pamoja na upatikanaji wa miundombinu muhimu kama ya afya, maji, umeme, barabara na kuendelea kukua kwa ukusanyaji mapato ni vigezo tosha vya kuufanya mji wa Dodoma kuwa Jiji.

"Pia Dodoma inajitosheleza kwa mahitaji mengi ikiwemo uwepo wa taasisi mbalimbali muhimu kama Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, vyuo vikuu zaidi ya vitano, Ofisi ya UN, hivyo nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt Magufuli kwa uamuzi wake kwani unaleta tija kwa wananchi. Nashauri jambo hili lipongezwe badala ya kubezwa”. 

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufuatilia utaratibu wa uingizwaji wa mafuta ya kula nchini kutokana  na uwepo wa baadhi ya wafanyabishara wasiokuwa waaminifu kuingiza mafuta safi na kudai ni ghafi. 

Waziri Mkuu amesema ghalama za kulipia kodi mafuta hayo inatofautiana, mafuta ghafi yanalipiwa asilimia 10 na safi ni asilimia 25 hivyo lazima Serikali ifuatilie ili wahusika waweze kutozwa kodi inayostahili.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kulinda viwanda vya ndani vya mafuta, hivyo ni lazima taratibu za uingizwaji wa mafuta ukazingatiwa wakati huu ambao nchi inahitaji mafuta ya nje kwa kuwa uzalishaji wa ndani bado haujajitosheleza. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbles Lema aliyetaka kufahamu ni kwa nini Serikali isione umuhimu wa ungizwaji wa mafuta kutoka nje  ili kusaidia kupunguza  bei ya mafuta ya kula ambayo bei yake imeongezeka kwa asilimia 15 hadi 30.
Kuhusu suala la kuongezeka kwa bei ya sukari nchini hususan katika kipindi cha kukaribia kuanza kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa mikoa, wilaya na Maofisa biashara kuhakikisha wanawasimamia wafanyabiashara hawapandishi bei za bidhaa kiholela.
Amesema kitendo cha wafanyabiashara kupandisha bei za baadhi ya bidhaa katika kipindi hicho hususani sukari kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kuwapa adhabu waumini wa madhehebu ya kiislamu watakaokuwa kwenye mfungo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kuteuliwa Bw. Abdalla Bulembo ambaye alisema mwezi Mtukufu wa Ramadhani umekaribia na bei ya bidhaa kama sukari imeanza kupanda  na kufikia 2,800 , 3,000 na 3,200, hivyo Serikali inatoa tamko  gani  juu ya suala hilo.
Waziri Mkuu amesema Serikali  inalifanyia kazi suala hilo na tayari vibali vya kuagiza sukari vimeshatolewa ilikuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana wakati wote, ambapo Bodi ya Sukari kupitia Wizara ya Kilimo inaedelea kufuatilia mwenendo wa uingizwaji wa sukari nchini ili iweze kusambazwa hadi kwenye vijiji.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, MEI 3, 2018.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com