Na Mathias Canal, Singida
Mamia ya wananchi Wilayani Manyoni Mkoani Singida wameshiriki katika mazishi ya Padre Onesphor Lazaro Kayombo (C.PP.S) aliyezikwa Jana Jumanne 20 Machi 2018 kwenye makabuli maalumu ya shirika la mapadre wa DAMU ya Yesu.
Katika misa Takatifu ya kuaga mwili wa marehemu iliyofanyika katika kanisa la kupaa kwa Bwana Parokia ya Manyoni, Baba Askofu Edward Mapunda wa kanisa la Roman Catholic jimbo la Singida amewasihi waumini kote ulimwenguni kutenda mambo mema kwa wanadamu wengine ili kuacha alama ya kiutume kama aliyoacha marehemu Padri Kayombo.
Askofu Mapunda ameeleza kuwa safari ya utimilifu wa Padri Kayombo umefika ukomo japo ameacha pengo kubwa katika kanisa sambamba na Jamii kwa ujumla na atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka ikiwa ni pamoja na kuwa msaada kwa masikini na wasiojiweza.
Padri Onesphor Lazaro Kayombo alifariki dunia usiku wa tarehe 14 Machi 2018 saa 5:14 usiku katika Hospitali ya Kinondoni Jijini Dar es salaam alipokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu ambapo mpaka anafariki dunia alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya figo (CARDIO PULMONARY FAILURE).
Akizungumza kwa niaba ya Familia Mpwa wa Marehemu ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo aliwashukuru mamia ya wananchi wakiwemo ndugu, marafiki, jamaa na majirani likiwemo kanisa la Roman Catholic katika kumuuguza na hatimaye kwa ushiriki wa mazishi ya mjomba wake.
MD Kayombo Alisisitiza kuwa waumini wa kanisa la kupaa kwa Bwana Parokia ya Manyoni na makanisa yote kwa pamoja wanapaswa kumuombea marehemu Padri Onesphor Lazaro Kayombo ili apumzike kwa amani kwa kuvipiga vita na kumaliza mwendo hapa Duniani.
Akitoa salamu za serikali katika Misa ya kuaga mwili Wa marehemu, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt Rehema Nchimbi anatoa pole kwa kanisa kwa kuondokewa na moja ya walimu katika dini sambamba na kutoa pole kwa wananchi na ndugu wote.
Dc Mtaturu Alisema kuwa maisha ya mwanadamu yana siri kubwa kwani haitambuliki ni lini atatoweka duniani hivyo waumini wote wanapaswa kufanya mambo mema na kuacha alama kubwa na muhimu katika Jamii.
Aidha, alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa dini hivyo inawasihi viongozi wote wa dini nchini kuendelea kudumisha amani kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika mapambano dhidi ya wavunjifu wa amani na umoja wa wananchi.
Padri Onesphor Lazaro Kayombo alizaliwa 8 Septemba 1960 ambapo mpaka mauti inamkuta 14 Machi 2018 alikuwa na umri wa miaka 58.
0 comments:
Post a Comment