Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Mhe Miraji Mtaturu ametoa onyo kwa wanaohamasisha kufanyika kwa maandamano katika wilaya hiyo kuacha mara moja vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kufuatia hilo amewaasa wananchi kutokubali kurubuniwa na watu hao na badala yake wajikite katika shughuli zitakazowaingizia kipato.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mtaturu amesema kumekuwa na minong`ono ya uwepo wa maandamano jambo ambalo anawaasa waachane nalo.
“Nimesikia dalili kwamba kutakuwa na maandamano,nawaomba wananchi waachane na hayo mambo ambayo hayana msingi kwao,hao wanaotaka kuandamana hawana kazi za kufanya,
“Sisi tuna kazi za kufanya tusiingie kwenye mkumbo wa kushiriki katika jambo ambalo litatuathiri sisi na familia zetu hivyo tusipoteze muda twendeni tukafanye kazi,mtu anayekuhamasisha jambo ambalo halina manufaa na wewe achana nae muda wa kufanya siasa haupo sasa hivi kila mmoja afanye shughuli zake,”aliongeza Mtaturu.
Mbali na hilo Mtaturu aliwataka wananchi ambao hawakupanda mikorosho waweze kupanda zao hilo huku akiwahakikishia kuwa miche ipo ya kutosha.
Alisema kama wilaya imejiwekea mikakati ikiwemo kuwa na eneo maalum litakalotumika kama shamba darasa kwa ajili ya zao hilo lengo likiwa baada ya miaka mitatu kuwe na uchumi mkubwa wa korosho.
“Tumetenga eneo katika kijiji cha Mkiwa heka mia tano kwa ajili ya upandaji wa mfano,tayari kijiji kimeridhia hivyo kwa sasa tunaweka utaratibu wa watu kupata maeneo yao ili wakapande mikorosho kwa wingi,”alisema Mtaturu.
Aliongeza kuwa miche ipo na inatolewa bure hivyo watumie vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa ajili ya kupanda.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment