Na David KAFULILA
Machi5, 2018, Gazeti la linalochapishwa kwa lugha ya kingereza la DailyBusiness la Kenya lilibeba habari kubwa "US Agency assigns Tanzania higher credit rating than Kenya" habari iliyobeba maudhui kwamba Tanzania( yenye B1) imepata daraja juu kuliko Kenya(yenye B2) kwenye tathimini ya uwezo wa kukopesheka iliyofanywa na Taasisi ya Moody's yenye makao yake Makuu USA.
Siku hiyo hiyo, Gazeti linalochapishwa kwa lugha ya kiingereza, CITIZEN la Tanzania, likabeba habari hiyohiyo yenye kichwa " Govt dismiss Moody's Report" , habari ambayo maudhui yake yalibeba ujumbe kwamba Tanzania(yenye B1) imefanya vibaya kuliko nchi yoyote Afrika Mashariki( Kenya, Uganda na Rwanda zote zilipata daraja sawa la B2).
Niwazi wasomaji waliobahatika kusoma magazeti haya mawili siku hiyo walitoka wamechanganyikiwa.lakini niseme kwa sentensi moja tu kabla sijaendelea kwamba kwa mujibu wa madaraja(ranking) ya Moody's, B1 yoyote ipo juu ya B2 yoyote, hivyo Tanzania imefanya vema kuliko Kenya, Rwanda na Uganda kwa tafsiri hiyo.
( rejea Moody's rating scale and definition-www.moody's.com).
Sasa tuendelee. Katika Makala yangu Machi6,2018, niliahidi kuzungumzia ripoti ya tathimini iliyotolewa na Kampuni ya Moody's kuhusu uwezo wa Tanzania kiuchumi na daraja lake katika viwango vya kuaminika kukopesheka kwenye masoko ya mitaji duniani.
Katika Makala ile niliishia kwa kugusia maoni ya Katibu Mkuu wizara ya Fedha, ambaye pia ndio mlipaji Mkuu wa Serikali, Ndugu Dotto James.Ambaye katika maoni yake kufuatia Ripoti hiyo ya Moody's iliyowekwa kwenye mtandao wake Machi4, 2018, Ndugu Dotto James alisomeka kupinga vikali kama alivyonukuliwa katika Gazeti la CITIZEN, la Machi5, 2018.
Kauli ya Dotto James ilipokewa kwa maoni mbalimbali, ambapo baadhi walionesha kushangazwa na uamuzi wa Katibu Mkuu huyo kupinga ripoti ya Kampuni ambayo kwa hakika weledi na rekodi yake kwa kiasi kikubwa ni ya juu sana duniani.
Kazi ya kuthimini viwango na kupanga madaraja kuhusu uwezo wa nchi, taasisi, kampuni au shirika kuweza kukopa na kulipa kwa wakati(credit rating) imekuwepo kwa karibu miaka 150.
Ingawa taasisi hizi zinazofanya tathimini ya uwezo na utayari wa serikali au kampuni kulipa deni kwa wakati zipo zaidi ya 70 duniani, lakini kubwa kabisa ni 3. Ambazo ni Moody's , Fitch na Standard&Poor.Kwa ujumla asilimia 95 ya kazi ya tathimini hizi duniani hufanywa na wakala hizi( zinamiliki asilimia 95% ya soko la huduma hii duniani). Tathimini ya Tanzania imefanywa na Moody's
Nchi nyingi duniani pamoja na mashirika na kampuni hulipia fedha ili kufanyiwa tathimini kwa lengo la kupata mikopo kwenye masoko ya fedha kimataifa kwa kuuza dhamana za Serikali kimataifa( maarufu kama eurobonds).
Wanaoshiriki masoko hayo kwa maana ya kukopesha/kuwekeza kwenye dhamana za Serikali wanazingatia sana maoni ya Taasisi hizi(credit agency) kama mwongozo kuamua ni nchi zipi wazikopeshe/wawekeze kwa kununua dhamana za serikali na kwa riba kiasi gani.
Hivyo kiasi cha riba kinazingatia sana daraja ambalo nchi imepewa. Daraja la juu unapata mkopo kwa riba chini, na riba inaongezeka kadiri daraja (grade) inavyoshuka kwa msingi kwamba nchi zenye daraja la chini zinauwezekano mkubwa wa kushindwa kulipa mikopo.
Huu ndio ukweli hata kwa wanaochukua mikopo Benki za kawaida, kwamba riba ya mkopo hutegemea uwezo wako wa kulipa.Benki nyingi zimeleza kwamba moja ya sababu ya zenyewe kutoa mikopo kwa riba juu imetokana na tatizo kubwa la uwezo na utayari mdogo katika kulipa.
Labda nije sasa kwenye swali niloanza nalo ambalo ni serikali kupinga ripoti ya Moody's kama ilivyoripotiwa na gazeti la CITIZEN , Machi5,2018.
Swali la ,Je, Katibu Mkuu Dotto James alikuwa sahihi kupinga ripoti ya Moody's kwa Tanzania? Labda kabla ya kujibu swali hilo, niseme kwamba ripoti ya Moody's kwa Tanzania imeipa Tanzania daraja la B1. Daraja ambalo linaiwezesha nchi kukopa katika masoko ya fedha kimataifa kwa riba ya wastani.
Na pengine kabla sijashughulika nalo, ieleweke wazi kwamba daraja la B1 ambalo Tanzania imepewa ni daraja la juu kulinganisha na daraja ambalo Kenya, Kenya na Rwanda walipewa.wote walipewa B2. Ipo chini ya Tanzania. Hii ndio kusema kwamba Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri zaidi kuliko Kenya kufaidi mikopo katika masoko ya mitaji kimataifa.
Labda tujikumbushe tu kwamba, Februari22, 2018, Rais Uhuru Kenyatta aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akifurahia Kenya kufanikisha mkopo wa dola 2bn kwenye Soko la mitaji la London Stock exchange, akijigamba kusisitiza kwamba bado wawekezaji wana imani na Uchumi wa Kenya kwani walitaka kukopa dola 2bn lakini maombi yalifika dola 14bn.
Nadhani furaha ya Rais Uhuru Kenyatta ilitokana na ukweli kwamba Kenya ipo kwenye hali mbaya ya mzigo wa madeni. Deni lilifokia asilimia 60% ya pato la Taifa, na ni moja ya sababu ya kushushwa daraja kutoka B1 kuja B2).
Shirika la Fedha na Bank ya dunia wamesisitiza Mara kadhaa tangu mwaka 2016 kuhusu mwenendo wa madeni kwa nchi nyingi za bara la Afrika. Ambapo kwa nchi 46 zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara( katika nchi za afrika ondoa Libya, Tunisia, Misri, Djibout, Somalia, Sudan, Moroco na Algeria). Nchi 25 kati ya hizo 46 zipo kwenye hali mbaya ya madeni kwa maana yamevuka asilimia 50% ya pato la Taifa.
Walau Tanzania bado hatujaingia kundi hilo. Bado deni la Taifa la Tanzania ni kiwango cha wastani kwa vipimo vya IMF. Tanzania deni lipo asilimia 34%, .(Moodys report, March4,2018).
Najaribu kutafakari kama Kenya yenye daraja chini ya Tanzania hali ni hiyo, Tanzania si itakuwa na hakika zaidi? Naam, tupate dola hizo tubadili sura ya nchi kwa miradi ya kimkakati kama ilivyobainishwa kwenye Mpango wa pili wa maendeleo 2016/21.
Ndiyo!,Kukopa kwajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati yenye tija kubwa kwenye Uchumi ndio mikopo inayoshauriwa kitaalamu.Kutokopa kwajili hiyo ni kupoteza fursa na hasara kiuchumi.
Bado mtu atajiuliza, kwanini basi Katibu Mkuu Dotto apinge ripoti hiyo wakati inaiweka Tanzania kwenye nafasi nzuri kuliko Kenya? Nadhani Katibu Mkuu huyu sio mwanafunzi mwenye kufurahia ushindi kwa kuzingatia amekuwa wangapi bali anazingatia amepata ngapi.
Zamani kidogo/sijui siku hizi ilikuwa sekondari ukipata alama chini ya 21 maanake umefeli vibaya, yaani una F. Sasa kuna mwanafunzi alikuwa anafurahia alama 20 kwakuwa amewazidi wenzake wakati wote wamepata F. Hivyo, kwa Ndugu Dotto James, kwake hoja sioTanzania kuwa pazuri kuliko Kenya bali daraja zuri zaidi analodhani Tanzania tulistahili.
Aidha, inawezekana alikwazwa na maoni ya Moody's katika ripoti yao kwamba msimamo wa Tanzania katika sekta ya madini ni kasoro katika kuvutia wawekezaji kutoka nje kwani wataona kuwa Tanzania ni nchi isiyotabirika kisera kutokana na mabadiliko makubwa ya kisheria yaliyofanywa kwenye sekta hiyo.
Hili la mwisho, hata Mimi limenikwaza, nimeona kwenye tovuti yao(Moody's)na ripoti yao wakiweka uzito mkubwa kulalamikia sheria mpya za madini na mtazamo mpya wa watanzania kupitia Rais wao katika uwekezaji kwenye sekta ya madini.
Hili limenikwaza kwasababu Moody's kulalamikia mabadiliko ya serikali katika kutazama sekta ya madini nisawa na kusema tungendelea kama ilivyokuwa. Ilivyokuwa tunaibiwa tangu mwanzo!
Labda kama tunakuwa mahayawani!.Najua hoja ya Moody's ya kutokutabirika, lakini naelewa hoja ya Serikali kwamba ilikuwa lazima tutoke kwenye kuibiwa, tutengeneze sheria kuhakikisha hatuibiwi. Baada ya hapo sasa tutatabirika kwa muda mrefu!
Nasema hilo kwamsisitizo kwasababu tumetoka mbali, Nakumbuka mwaka 2010, Nchi14 za Ulaya zilizokuwa zikichangia bajeti kwa mfumo wa Government Budget Support-GBS, zilikata kiasi cha mkopo nafuu zaidi ya dola milioni 534(zaidi ya 1Trilion/Tsh) kwa hoja ya serikali kushindwa kukabili Ufisadi mkubwa uliokuwa ukiendelea nchini( Reuters, Desemba9,2010).
Nakumbuka mwaka 2014, nikiwa mjumbe wa Kamati ya Bunge Uchumi, viwanda na Biashara, aliyekuwa Katibu Mkuu wizara ya fedha wakati huo, Ndugu Likwilile alisema kwenye Kamati " moja ya sababu ya kukwama mikopo nafuu tuliyotarajia nikutokana na kelele za hawa kina Kafulilia kuhusu escrow"alieleza akilalamikia kelele kupinga Ufisadi.
Niwazi moja ya maeneo yaliyokuwa na ufisadi mkubwa na kupigiwa kelele muda mrefu ni kwenye mikataba ya madini na Umeme.Serikali awamu ya tano imeshughulikia ufisadi kwa kiwango kikubwa.
Zaidi ya hatua kali kwenye madini, pia mikataba ya kinyonyaji kama ile ya symbion iliyongezewa muda kipindi cha lala salama, mwishoni 2015, Serikali ya awamu ya tano ilifuta, na hata waliotwa wawekezaji wengine kwenye umeme akina Habinder Singh Sethi wa IPTL ,tulioambiwa wakichukuliwa hatua wawekezaji watakimbia, sasa wapo keko!
Pengine Ndio sababu ripoti ya Transparency International imeonesha kwamba tumetoka nchi ya 117 mwaka 2015 mpaka 103 mwaka 2017,sasa kuirekebisha ufisadi kwenye madini tena inakuwa sababu tusiaminike? Kutafuta uaminifu wa namna hiyo nafuu tubaki na alama B1.
Kabla sijajibu kama Ndugu Dotto James alikuwa na uhalali wa kuhoji au la!, Nianze na swali la jumla, Kwamba Je, nchi au kampuni inaweza kuhoji au kupinga na kukosoa ripoti hizi?
Profesa wa Uchumi , Methew Ocran alipata kusema "credit rating is opinions which are bound to be disputed or criticism" kwamba tathimini za uwezo na utayari wa kulipa mikopo zinazofanywa na Taasisi hizi ni maoni tu, yanayoweza kupingwa na hata kukosolewa.
Inakumbukwa mdororo wa kiuchumi duniani mwaka 2008 ulisababishwa na wakala hawa Moody's , Fitch na Standard&Poor kutofanya tathimini kiuweledi kwa kiwango cha kutosha na kusababisha mikopo isiyolipika na Uchumi wa dunia kuyumba vibaya Marekani na nchi za Ulaya, athari ambazo kwetu Tanzania zilipelekea Serikali ya Kikwete kutenga trilioni 1.7/Sh kama mfuko wa kunusuru Uchumi( Stimulus Package).
Sitaki kuulizwa kama kweli zilienda kunusuru Uchumi kweli au la!, kwani tofauti na nchi zingine ambazo mfuko kama huo ulitungiwa mpaka sheria kuhakikisha udhibiti , kwetu zilitolewa bila utaratibu madhubuti na nyingi zikaishia kwa waliotwa wajanja wachache!.
Huko sio lengo langu,Nilichotaka kusema tu nikwamba mwaka 2008 nchi nyingi zilihoji umakini na umahili wa Taasisi hizi, hivyo Tanzania haitokuwa ya kwanza kuhoji weledi na umakini wa wakala/Taasisi hizi.
Kama nilivyosisitiza hapo juu kauli ya Prof wa Uchumi kutoka Chuo kikuu cha Western Cape, Methew Koffi Ocran alipohojiwa na mtandao maarufu wa Conversation kuhusu uhakika na umadhubuti wa Taasisi hizi nakusema kwamba ripoti zao pamoja na umahiri na weledi wote bado zinabaki kuwa maoni. Na kuna nyakati taasisi hizi zilipata kushitakiwa na kulipa faini.
Mwaka 2008 , Taasisi ya Moodys ililipa faini ya dola 864 kwa mamlaka za Marekani ( karibu trilioni 2/=) kutokana na kukosa umakini katika tathimini zake.( Mtandao wa Deutschwell-DW-Januari14,2017).
Mbali na matukio hayo, wakala hawa wamepata kupingwa na nchi mbalimbali kwa nyakati tofauti baada ya nchi husika kutoridhishwa na ripoti.
India mwaka 2016 ilipinga ripoti ya Moodys kwa hoja kwamba ilipewa daraja la chini (Baa3)kwa hoja ya ukubwa wa deni wakati Uchumi wa India ni imara na kuhoji kwanini India ishushwe daraja kwa hoja hizo wakati nchi kama Japan na Ureno zina picha ibayofanana na wao, zina madeni karibu mara mbili ya uchumi lakini bado zimendelea kupewa alama nzuri na taasisi hizo.(Reuters, Desemba25,2016)
Acha India. China, Taifa kubwa la pili kiuchumi duniani, linalomiliki asilimia 10% ya Uchumi wa dunia, mwaka jana 2017.lilipinga ripoti ya taasisi ya Moody's ilipoishusha daraja/grade kutoka Aa3 mpaka A1 kufuatia maoni ya Moody's kwamba China ilikuwa na matatizo ambayo Mara kwa mara yalisababisha kuingiza fedha kurekebisha hali (Stimulus package).(Reuters May24,2017)
Hata Marekani yenyewe mwaka 2011,Chini ya Rais Barack Obama, ilipinga tathimini ya Taasisi ya Standard& Poor iliyoishusha daraja/grade kutoka daraja AAA Kwenda AA+ kutokana na sintofahafahamu ya kiwango kikubwa cha mikopo.(New York Times, August6,2011).
Nimejaribu kutoa mifano hii kusisitiza kwamba kupinga ama kukosoa ripoti za taasisi hizi sio jambo la ajabu nchi inapokuwa haijaridhika.
Wanaofanya kazi hizi ni wanadamu. Na hata mfumo wao wa kufikia maamuzi, pamoja na ukweli kuwa kazi kubwa kitaalamu inafanyika, lakini kwenye kuamua daraja gani nchi ipewe wanapiga kura na maamuzi yanafikiwa kwa wingi wa kura(simple majority).
Katika hali ya kawaida upo uwezekano hata ndani ya jopo lao baadhi kuwa na maoni tofauti kuhusu daraja wanalofikia uamuzi kuipa nchi fulani.
Kusema hivyo sina maana kwamba wakala/taasisi hizi ripoti zake ni za kupuuza kirahisi kama alivyopuuza mwaka jana, Waziri wa Fedha wa Kenya, Bw Henry Rotch baada ya Moody's kusema kwamba Kenya inastahili kushushwa daraja/grade kutokana na hali mbaya ya deni la Taifa.Waziri Ritch alisema "Ripoti ya Moody's nikama imeandaliwa mezani,haina umakini wowote" (East Africa,Nov9,2017.)
Hapana. Wakala/Taasisi hawa kwa kiasi kikubwa wanafanya kazi kwa weledi wa juu. Wanazingatia mambo muhimu kama mwonekano na mwenendo wa uchumi mkubwa, hali ya kifedha kwa nchi kumudu majukumu yake, uimara katika sera za Fedha na Kodi pamoja na uhusiano wake katika biashara kimataifa sanjari umadhubuti wa kitaasisi na uimara wa dola husika kisiasa.
Nikutokana na weledi na umakini huo, pamoja na kasoro za kibinadamu kujitokeza hapa na pale, bado ripoti za taasisi hizi zimebaki kuwa mwongozo kwa taasisi zote za fedha na wawekezaji wakubwa duniani wanapotaka kufikia maamuzi.hakujawa na mbadala.
Taasisi hizi zina nguvu sana, wanaofuatilia siasa za Afrika ya kusini wanajua, ilikuwa kila hatua Rais Jacob Zuma aliyokosea walitoa matokeo kuishusha daraja mpaka kufikia nchi isiyostahili kuwekeza. Lakini baada tu ya Ramaphosa kutangazwa kuwa Rais wa ANC, zikatangaza kuimarika na hata alipotangazwa mshindi halikadharika.
Kujua kwa kina rejea taarifa kwenye mtandao maarufu duniani kwa habari za uchumi na Biashara-Bloomberg-Februari21,2018 au Businesstech ya Februari19,2018 iliyobeba kichwa cha Habari " Moody's is optimistic about Ramaphosa's first move as President".ikimaanisha kwamba taasisi ya Moody's ina imani na Rais Ramaphosa na hivyo wawekezaji wawe na hakika Afrika kusini ni mahala salama kuwekeza baada ya Ramaphosa.
Sitaki kusema taasisi hizi zimeshiriki kumwondoa komredi Zuma, la-hasha!.Nimejaribu tu kueleza namna zilivyo na nguvu hata kwenye mwenendo wa siasa za nchi.
Shirika la Fedha Kimataifa( IMF), limepata kubainisha kwamba , tangu mwaka 1975-2009, nchi zote zilizotajwa na Taasisi hizi( Moody's, Fitch, Standard& Poor) hizi kuwa sio sehemu salama kuwekeza, zilishindwa kulipa madeni na kuingia mgogoro wa madeni.Hili linathibitisha umahili wa Taasisi hizi.
Pia ni asilimia1% ya kampuni ambazo zilipewa daraja kuwa zinakopesheka zilishindwa kulipa madeni.Hili pia linathibitisha umahili wao.
Hivyo basi, Nikatika msingi huo naona takwimu hizi zinaongea mengi kwamba ripoti za taasisi hizi , husuani hizi tatu, Moodys , Fitch pamoja na Standard&Poor ni za kuaminika kwa kiwango kikubwa hata kama zinaweza zisiwe sahihi kwa asilimia 100 (RaiaMwema,Machi14,2018)
0 comments:
Post a Comment