Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo Idara ya Uendelezaji Mazao pamoja na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini leo wamedhuru Mkoa wa Tanga lengo likiwa ni kuangalia namna ya uendelezaji wa zao la muhogo mkoani humo na changamoto zinazolikabili.
Akiongea na timu hiyo Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi Zena Ahamedi Saidi amesema, mkoa wa Tanga umekuwa na mkakati wa muda mrefu wa kuendeleza zao hilo ambapo kila nyumba ilitakiwa kuwa na ekari moja ya muogo ili kuimarisha usalama wa chakula mkoani humo.
Aidha mipango imeendelea kufanyika baina ya mkoa na Taasisi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili waweze kuzalisha mbegu ya kutosha na kuzisambaza kwa wakulima,alisisitiza Bi Zena.
Hata hivyo aliendelea kusema kwamba bado upatikanaji wa soko ni changamoto kubwa kwa wakulima kwani bado hawajapata soko la uhakika.
Naye mkuu wa msafara na mtaalamu wa mazao ya bustani bi Tabu Likoko amewaeleza kwamba kupitia mradi wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) zao la muhogo limepewa kipaumbele kwakuwa ni moja ya mazao ya biashara na chakula hasa katika mikoa ya Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara na sehemu nyinginezo.
Akijibu changamoto ya soko Bi Tabu amesisitiza kwamba tayari nchi ya china na Tanzania wameingia kwenye itifaki ya uzalishaji wa zao la muhogo na kuliuza nchini china hivyo serikali inaangalia namna nzuri ya kuzishirikisha sekta binfsi ili zishiriki kikamilifu katika kuingia mikataba na wakulima wanaozalisha muhogo.
Naye mkulima wa mbegu za muhogo kutoka kijiji cha Parungu kata ya Kasela Wilaya ya Mkinga Bwana Ilale Protasi ambaye ana shamba lenye ukubwa wa ekari saba (7) zilizopandwa muhogo anasema amepata faida kubwa kutokana na kilimo cha mbegu za muhogo ambapo kimemuwezesha kubadili maisha na kuwasomesha watoto wake.
Aidha bwana Ilale ameiomba serikali kuwasaidia wakulima wa zao hilo kupata soko la uhakika na uanzishwaji wa viwanda vidogovidogo vya kuongeza thamani ya zao hilo ili kuepuka hasara ambazo zimekuwa zikipatikana kwa kuuza mihogo kwa bei ya chini.
0 comments:
Post a Comment