METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, March 15, 2020

NAIBU WAZIRI SHONZA,FILAMU YA DALTON NI INAFAA KWA VIPINDI VYA WATOTO

Naibu Waziri Mhe.Juliana Shonza akisisitiza kusambazwa kwa filamu ya Dalton katika vituo vya televisheni mbalimbali nchini ikiwemo TBC ili filamu hiyo itumike kutoa elimu kwa watoto ionyeshwe katika vipindi vya watoto,leo jijini Mwanza alipokuwa akizindua filamu hiyo.
Naibu Waziri Mhe.Juliana Shonza (katikati)akifungua CD ya Filamu ya Dalton kuashiria uzinduzi wa filamu hiyo leo jijini Mwanza,wakwanza kulia ni Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana Jonas Maduhu na kushoto ni Mtayarishaji wa Filamu hiyo Bw.Cherrif Daudi.
Mtayarishaji wa Filamu ya Dalton Bw.Cherrif Daudi akitoa shukrani kwa Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza  (hayupo pichani) na kumwahidi kusambaza filamu hiyo mapema kila mahali kwa manufaa ya watoto,mara baada uzinduzi wa filamu hiyo leo jijini Mwanza.
Baadhi ya watoto waliyohudhuria hafla ya uzinduzi wa filamu ya Dalton wakifuatilia filamu hiyo wakati ikionyeshwa wakati wa uzinduzi wake leo jijini Mwanza ambapo filamu hiyo imebeba maudhui ya watoto.

Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza amemsisitiza  mwandaaji wa filamu ya Dalton kuhakikisha anaisambaza filamu hiyo kila mahali ili kuwapa fursa watoto kujifunza.

Mhe.Shonza ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza alipokuwa akizindua filamu hiyo yenye kutoa elimu kwa watoto namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika jamii. 

"Filamu hii niya kipekee sababu imebeba maudhui mazuri ambayo yanatoa elimu kwa watoto na ni vyema ikaonyeshwa katika vipindi vya watoto katika  televisheni badala ya watoto kuangalia katuni tu,"alisema  Mhe.Shonza.

Akiendelea kuzungumza Naibu Waziri huyo aliwasisitiza wazazi kuwa makini  na katuni ambazo watoto  wao wanaangalia kwani baadhi ya katuni hizo zinamaudhui ambayo siyo mazuri na zinachangia mmomonyoko wa maadili.

Pamoja na hayo naye mtayarishaji wa filamu hiyo Bw. Cherrif Daudi alimwahidi Naibu Waziri huyo kuwa atahakikisha katika kuisambaza filamu hiyo mikoa yote nchini.

 "Niliamua kuandaa filamu hii sababu niliona familia nyingi zimeshindwa kutenga muda wa kuongea na watoto kuhusu  kusimamia ndoto zao na namna ya kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika jamii,pamoja na kuwa na utii,uwajibikaji na kutokata tamaa,"alisema Bw. Daudi.

Aidha,nae Bw.Daudi aliendelea kusisitiza kuwa ni imani yake filamu hii itakuwa mkombozi kwa watoto na vijana katika kutoa elimu kuhusu mmomonyoko wa maadili. 

Pamoja na hayo nae Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana Bw.Jonas Maduhu alimpongeza mheshimiwa Naibu Waziri Shonza kwa namna wizara yake anavyofanya kazi kwa bidii ya kusimamia wasanii na pamoja na kuwasapoti katika kazi zao.

Halikadhalika nae mmoja ya wanafunzi  waliyohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa filamu ya Dalton kutoka  Shule ya Kingdom Heritage School Joan Mwalukasa wa Darasa la tano alieleza kufurahishwa na filamu hiyo na namna inavyotoa elimu ya maadili kwa watoto na kufundisha kuhusu heshima kwa wakubwa.

Katika kuhitimisha Mhe.Shonza aliwasisitiza wasanii wa mwanza kujisajili BASATA ilikuendesha shughuli zao katika mfumo rasmi,pamoja na kupendana na kuhakikisha wanazalisha kazi zenye ubora pamoja na muandaaji wa filamu ya Dalton kujipanga kuwa na programu ya kuibua vipaji vya watoto.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com