METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, March 15, 2020

KAMATI YA BUNGE YAUBEBA MRADI WA MAKTABA YA CHUO CHA ARDHI TABORA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitolea ufafanuzi hoja zilizowasilishwa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusiana na mradi wa ujenzi wa Maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora wakati kamati hiyo ilipokwenda kukagua maendeleo ya mradi huo mwishoni mwa wiki . Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati Kemilembe Lwota na kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Tabora Agrey Mwanri.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwaongoza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipowasili chuo cha ardhi Tabora kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Maktaba ya chuo hicho mwishoni mwa wiki.
Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora Biseko Musiba akimuoongoza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kemilembe Lwota alipowasili chuoni hapo na ujumbe wake kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Maktaba ya chuo hicho mwishoni mwa wiki.
 Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Magdalena Sakaya akiwasilisha hoja kuhusiana na Mradi wa ujenzi wa Maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora mwishoni mwa wiki wakati Kamati yake ilipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeamua kuubeba mradi wa ujenzi wa Maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora kilichopo mkoani Tabora kwa lengo la kuhakikisha mradi huo unapatiwa fedha za kutosha na kukamilika ili kukiwezesha chuo kuwa na Maktaba kubwa na ya kisasa.
Uamuzi huo wa Kamati unafuatia kuelezwa kuwa, ujenzi wa mradi wa Maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora umeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na changamoto ya fedha pamoja na na majadiliano ya muda mrefu kati chuo na Mshauri Msimamizi wa ujenzi ambaye ni Wakala Ujenzi Tanzania (TBA).
Akizungumza mwishoni mwa wiki mkoani Tabora wakati Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua maendeleo ya mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati Kemilembe Lwota alisema, kamati yake imeamua kuubeba mradi huo kama suala maalum na kulipeleka mbele zaidi na kuhakikisha kama kamati wanaifanya kazi hiyo kwa uhakika ili kusaidia kukamilika kwake.
‘’Hata hiki kizuri kilichokuja cha kujenga maktaba mlichoanza kukitengeneza lakini ndani ya miaka mitano ujenzi umesimama kweli kuna shida, naungana na wajumbe wenzangu hili suala tutalichukua kama issue mahsusi ya kamati na tutalipeleka mbele zaidi na kufanya kazi hiyo kwa uhakika na umakini zaidi’’ alisema Kemilembe.
Mbunge wa jimbo la Mtama mkoa wa Lindi Nape Nnauye ameshangazwa na mradi wa ujenzi wa maktaba hiyo kutokamilika kwa wakati pamoja na kamati hiyo kusaidia mara kadhaa kujenga hoja za kusaidia upatikanaji fedha. Ameitaka Serikali kuhakikisha fedha za ukamilishaji ujenzi huo zinapatikana.
Naye Mbunge wa jimbo la Kaliau mkoani Tabora Magdalena Sakaya alisema, pamoja na Tanzania kuwa na vyuo vya ardhi viwili (Morogoro na Tabora) vinavyotoa wahitimu wa ngazi ya Cheti na Diploma lakini kutokamilika kwa mradi wa Makataba ya Chuo hicho unachangia migogoro ya ardhi inayosababishwa na ukosefu wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbali za ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula aliwaeleza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili na Utalii kuwa, changamoto iliyosababisha kutokamilika mradi wa ujenzi wa Maktaba ya chuo cha ardhi Tabora kwa wakati ni upatikanaji mafungu ya fedha kutokuja kama ilivyokusudiwa.
Hata hivyo, Dkt Mabula alisema pamoja na changamoto hiyo chuo kimeendelea kufanya vizuri katika utendaji kazi ikiwemo kuongeza udahili kila mwaka na kubainisha kuwa katika jitihada za kukijengea uwezo wa chuo Wizara imekipa mradi wa kuzalisha baadhi ya nyaraka zinazohusiana na masuala ya ardhi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com