Na.
Fred J. Kibano
Mashindano ya michezo kwa Shule za Msingi Tanzania
(UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yameanza kufanyika
baada ya kufanyika kwa tathmini ya mashindano hayo ya mwaka jana, 2017 ambapo
baadhi ya michezo itaongezwa.
Akifungua kikao kazi cha siku mbili mjini Dodoma,
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu anayeshughulikia Sekondari, Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Paulina Mkwama, amesema kikao hicho nyeti kimewakutanisha wajumbe
toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na
Wadau wengine wakiwemo Maafisa Michezo toka Mikoa na Halmashauri, Maafisa Elimu
wa Mikoa na Halmashauri na Baraza la Michezo la Tanzania ili kufanya tathmini
na kuanza maandalizi ya michezo hiyo Juni, mwaka 2018.
“Kimsingi Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo pamoja na Wadau wengine wamekutana kwa
ajili ya kufanya tathmini ya mashindano ya UMITASHUMTA (Michezo kwa Shule za
Msingi Tanzania) na ile ya shule za sekondari (UMISSETA), yaliyofanyika mwaka
jana (2017), na kuweka mikakati ya namna bora ya kuendesha michezo kwa mwaka
2018, ndio lengo kuu la kikao hiki”
Bi. Mkwama amesema, baada ya kikao hicho, kitawezesha
kupata mikakati madhubuti kwa mashindano mapya hasa baada ya kupitia taarifa za
michezo iliyofanyika mwaka uliopita, 2017 ili kuweka mikakati mizuri
itakayoboresha michezo hiyo ambayo ndiyo muhimili wa wachezaji wote wa Taifa
hili.
Aidha, amesema watapitia bajeti ya michezo ya mwaka
2017 na kuona changamoto zilizotokea ili kuzikabili kwa michezo ya mwaka huu,
2018 ikiwa ni pamoja na kushirikisha Wadau ambao wataiunga mkono Serikali
hususani katika bajeti na vifaa.
Pia Miongozo yote ya michezo itapitiwa ili kujua
changamoto zote lengo likiwa ni kuboresha michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA
nchini ambayo pia hukuza taaluma mashuleni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Michezo
Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja, amewataka Maafisa Michezo kuteua Walimu ambao
wanauelewa wa michezo na ifanyike mapema ili kuondoa kasoro zilizo jitokeza
michezoni mwaka 2017.
Naye Mratibu wa Michezo Ofisi ya Rais TAMISEMI, Salum
Mkuya, amesema watatoa mapendekezo kwa baadhi ya michezo iongezwe kama vile
soka la wanawake ambalo Tanzania inafanya vizuri ikiwa ni nchi tano tu kwa bara
zima la Afrika, lakini pia ngoma kwani michezo inasaidia sana vijana kujenga
uzalendo kwa nchi yao.
Michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA hufanyika kila mwaka
kwa kukutanisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini na kwa mwaka
huu matarajio ni kuwahusisha wanafunzi wasiopungua 6,480 wa shule za msingi na
sekondari. Changamoto zilizojadiliwa ni pamoja na wanafunzi wenye mahitaji
maalum, vigezo vya umri, vifaa, bajeti ya usafiri na chakula na mengineyo
ambayo yatafanyiwa kazi kimkakati.
0 comments:
Post a Comment