TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
HATUA ZA KISHERIA NA KIUDHIBITI KWA
MAKAMPUNI YA SIMU YALIYOSHINDWA KULINDA WATEJA WAKE KITEKNOLOJIA NA
KISHERIA KUHAKIKISHA USALAMA WA MAWASILIANO YAO.
1. Katika shughuili zake za udhibiti
wa huduma za mawasiliano nchini, Mamlaka ya Mawasilaino Tanzania
imepokea malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano dhidi
ya kuwepo mazingira yasiyo salama katika huduma za mawasiliano na hivyo
kusababisha kufanyika kwa vitendo vya utapeli unaofanywa kwa kutuma
jumbe za udanganyifu na kulaghai, hivyo kusababisha watu kujipatia pesa
kwa njia ya udanganyifu.
Kwa mfano kupokea ujumbe kutoka namba
unayoifahamu ukikuagiza utume fedha au ujumbe wa kashfa au matusi
wakati hautoki kwa mhusika mwenye namba. Mamlaka imepokea malalamiko
mengi kutoka kwa wateja na malalamiko mengine hupelekwa Polisi. Kwa
miezi miwili tu, matukio 42 yameripotiwa Polisi pamoja na TCRA ambayo
tukio moja tu linakuwa na ulaghai wa takribani milioni 25 peke yake.
2. Tarehe 16 Oktoba, 2015 Mamlaka
iliwakumbusha watoa huduma za simu nchini juu ya wajibu wao kuchukua
hatua za kusheria na kitaalamu ili kulinda watumiaji dhidi ya utumaji wa
jumbe za kilaghai na kuchukua hatua mara moja kuzuia mitandao yao
kutumika kutuma jumbe za udanganyifu na kulaghai.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na
Mamlaka tarehe 16 Desemba, 2015 Mamlaka ilibaini kuwa kampuni za Benson
Informatics Limited (inayojulikana kama Smart), MIC Tanzania Limited
(inayojulikana kama Tigo), Airtel Tanzania Limited, Viettel Tanzania
Limited (inayojulikana kama Halotel) and Zanzibar Telecom Limited
inayojulikana kama Zantel) zimeshindwa, zimepuuzia na zimekataa kufuata
maagizo ya Mamlaka kuchukua hatua mara moja kuzuia mitandao yao kutumika
kutuma jumbe za kilaghai kinyume na Kanuni Na.8(a) ya Kanuni za
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2011 [the Electronic and
Postal Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations,
2011].
3. Tarehe 18 Disemba, 2015 Mamlaka
iliwaamuru watoa huduma za mawasiliano waliotajwa hapo juu kufika mbele
ya Mamlaka na kujieleza kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi
yao kwa kuvunja sheria na kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya
Kielectroniki na Postal ya Mwaka 2011 [the Electronic and Postal
Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011] kwa
kushindwa kuweka mazingira salama kwa watumiaji wa huduma za
mawasiliano.
4. Watoa huduma walifika na kutoa maelezo ya utetezi kati ya tarehe 21 na 23 Desemba, 2015.
5. Baada ya kuwasikiliza na kutilia
maanani utetezi wa watoa huduma na kwa mujibu wa uchunguzi na majaribio
uliofanywa na Mamlaka, Mamlaka imejiridhisha kuwa mitandao ya watoa
huduma waliotajwa hapo juu haikuwa salama na kuwa watoa huduma hao
walishindwa kufuata maelekezo ya Mamlaka juu ya kuweka mazingira salama
katika huduma wanazotoa.
Hivyo Mamlaka imejiridhisha kuwa watoa
huduma wamekiuka matakwa ya Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya
Kielectroniki na Postal ya mwaka 2011 (The Electronic and Postal
Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011)
inayowataka watoa huduma kuweka mazingira ya mitandao salama kwa
kuchukua hatua za kusheria na kitaalamu ili kulinda watumiaji dhidi ya
uhalifu ikiwa ni pamoja na utumaji wa jumbe za kilaghai kupitia mitandao
yao.
6. Kwa mujibu wa Kifungu cha 17 cha
Jedwali la Pili katika Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta,
Sura ya 306 ya Sheria za Nchi, kinachoipa Mamlaka uwezo wa kutoa adhabu
kwa Wenye Leseni dhidi ya uvunjifu wa Sheria, Kanuni na Masharti ya
Leseni, Mamlaka ya Mawasiliano imetoa:
A. Onyo kali kwa Kampuni za:
(i) Benson Informatics Limited (inayojulikana kama Smart),
(ii) MIC Tanzania Limited (inayojulikana kama Tigo),
(iii) Airtel Tanzania Limited,
(iv) Viettel Tanzania Limited (inayojulikana kama Halotel), na
(v) Zanzibar Telecom Limited (inayojulikana kama Zantel).
kwa kushindwa kutimiza matakwa ya
Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Postal ya
mwaka 2011 [the Electronic and Postal Communications (Computer
Emergency Response Team) Regulations, 2011] kwa kushindwa kuweza
mazingira salama kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano.
B. Imeamuru Kila Kampuni husika:
(i) Kuhakikisha kuwa, kuanzia siku
ya kutolewa kwa amri hii, inaweka mazingira salama katika mtandao wake
yatakayozuia utumaji wa jumbe za kilaghai (yaani ‘spoofed messages’) na
matishio mengine ya kiusalama;
(ii) Kulipa faini ya Shilingi za
Kitanzania Milioni Ishirini na Tano (Shs 25,000,000.00) kwa Mamlaka ya
Mawasiliano kabla ya tarehe 29 Januari, 2016; na
(iii) Endapo Makamuni haya yatashindwa
kutimiza amri Na.2 hapo juu, Mamlaka itachukua hatua zaidi za kisheria
na kiudhibiti dhidi ya Kampuni ya Simu husika.
7. Aidha, Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania inapeda kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi kuwa
makini na jumbe za kuwataka kutuma fedha bila ya kuwa na uhakika.
Inashauriwa kuhakiki ujumbe husika kwa kupiga simu na kuongea na mhusika
kabla ya kufanya maamuzi ya kutuma fedha hata kama namba inayotumika
unaijua.
Vilevile wawe makini wanapopokea jumbe
zinazoonesha zinatoka kwa mtu fulani wanayemjua kumbe ni matapeli
wanaotumia ulaghai kwa njia hii ya “spoofing”.
IMETOLEWA NA
Dkt. Ally Y. Simba
MKURUGENZI MKUU
30 Disemba, 2015
0 comments:
Post a Comment