METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 15, 2017

SERIKALI YAIAGIZA MAKUMBUSHO YA TAIFA KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO





Serikali kupitia Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ameipa Menejimenti ya Makumbusho ya Taifa muda usiozidi miezi miwili iwe ishabuni vyanzo vipya vya mapato ili iweze kutatua changamoto mbalimbali  zinazoikabili baadala ya kutegemea ruzuku pekee kutoka serikalini.

Amesema Makumbusho ya Taifa ina mali nyingi lakini imekuwa hajui namna ya kuzitumia ‘’Mkae chini mnambie namna gani mnaweza kuongeza mapato katika rasilimali mlizo nazo  halafu mniletee andiko  ofisini kwangu ndani ya muda usiozidi miezi miwili ’’ Aliagiza

Amesema kazi kubwa ya Makumbusho ya taifa ni kuhifadhi lakini wakati ikihifadhi inahitaji kupata mapato kidogo hapo hapo ili iweze kuendelea kuwepo.

Aliyasema hayo  leo  alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Makumbusho ya Taifa makao Makuu jijini Dares Salaam wakati alipofanya ziara ya siku moja ya kujionea namna Taasisi hiyo inavyofanya kazi

,Aliwataka Watumishi hao wasitumie muda mwingi  kulalamika baadala yake wasaidie katika kubuni vyanzo vipya vya mapato ili viwasaidie katika kujikwamua kimapato.

Naibu Waziri Hasunga aliongeza kuwa, licha ya Serikali  ya kutambua umuhimu wa Makumbusho hayo lakini hata hivyo Serikali imekuwa na masuala mengi yakufanya na yanayohitaji pesa katika kuyashughulikia.

Wakati huo huo, Ameiagiza taasisi hiyo ijitangaze kwa vile imekuwa haijulikani licha ya  kuwa na umuhimu mkubwa katika kuihudumia jamii.

‘’Mmekuwa mnafanya mambo makubwa  kisiri kisiri kwa ajili ya wananchi lakini wananchi mnaowahudumia hawajui mnayoyafanya kwa ajili yao hivyo jitangazeni’’  alisisitiza.

Pia, Aliwaagiza watumishi kuendelea kufanya tafiti ili waweze kuvumbua mambo mengi zaidi yatakayoisadia Taasisi hiyo kuweza kupiga hatua katika kuihudumia jamii.

‘’Sisi kama serikali hatujaweza kufanya vizuri katika eneo la utafiti tumekuwa  tukitenga bajeti ndogo lakini kwa kulitambua hilo nataka mpate pesa ya kutosha ili mfanye tafiti nyingi zaidi’’ alisisitiza

Aidha, Ameiagiza Menejimenti hiyo iimarishe mfumo wa ndani katika masuala ya Tehama, alisema haiwezekani taasisi hiyo hadi hivi sasa isiwe na kanzidata licha ya changamoto kubwa ya udukuzi unafanywa na mataifa makubwa katika masuala ya uhifadhi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu, Prof. Fortunatus Mabula amemuhakikishia Naibu Waziri Hasunga   ushirikiano mkubwa katika kazi.

Aidha, Prof. Mabula alimwambia  Naibu Waziri kuwa tayari wameshapata eneo la kujenga makumbusho ya Marais katika eneo la Iyombe  mjini Dodoma ikiwa ni kutekeleza agizo alilolitoa Waziri  wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangwalla alipozungumza na wadau wa Wizara mwezi uliopita mjini Dodoma
MWISHO


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com