METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 15, 2017

WANANCHI IYUMBU WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KUWAREJESHEA MAENEO YAO

 Rais Dk. John Magufuli akiwasalimia wananchi wa Iyumbu waliohudhuria katika uzinduzi wa nyumba 300 za Shirika la Nyumba (NHC)
 Viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa nyumba 300 za Shirika la Nyumba (NHC)
 Wananchi wa Iyumbu waliohudhuria uzinduzi wa nyumba 300 za Shirika la Nyumba (NHC)
Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana Anthony Mavunde akizungumza katika uzinduzi wa nyumba 300 za Shirika la Nyumba (NHC)

WANANCHI wa kata ya Iyumbu katika jimbo la Dodoma mjini wamempongeza na kumshukuru Rais Dk.John Magufuli kwa kuwarejeshea ekari 129 ambazo zilitengwa kwa ajili ya makaburi ya Viongozi wa Kitaifa.

Rais Magufuli alifikia uamuzi huo baada ya kupokea maombi ya Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde wakati wa ufunguzi wa nyumba 300 za Shirika la Nyumba Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu.

Wakizungumza kuhusu hatua hiyo, wananchi hao wamesema wamepokea kwa furaha kubwa sana na kwamba dhamira ya Rais ya kuwajali wanyonge imetimia.

Mmoja wa wananchi hao, George Makapi amesema urejeshaji huo utawawezesha kuendeleza maeneo yao ambayo yalichukuliwa tangu mwaka 2006 kwa lengo la kutumiwa kuzikia viongozi hao.

Katika maombi yake, Mavunde alimuomba Rais Magufuli kulirejesha kwa wananchi eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya makaburi ya Viongozi wa Kitaifa kwa kuwa ni zaidi ya miaka 7 imepita bila wananchi kulipwa fidia yoyote na kushindwa kuyatumia maeneo hayo kwa shughuli za kilimo na ufugaji kama walivyokuwa wanafanya awali.

Kufuatia ombi hilo, Rais Magufuli ameagiza ekari zote 129 zirejeshwe kwa wananchi kwa kuwa serikali haina mpango wa kulitumia eneo hilo kwa sasa.

Aidha Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kuwa na Mbunge mchapakazi na anayewajali wananchi wake na ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi yao.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com