Naibu Waziri Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Mhe. George Joseph Kakunda anayeshughulikia Elimu, Maji, Kilimo,
Mifugo na Maliasili, amefungua Mkutano wa kwanza wa kazi kwa Kaimu Makatibu
Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) katika ukumbi wa chuo cha Mipango
mjini Dodoma leo.
Mkutano huo ni wa kwanza tangu
kuanzishwa kwa Tume ya TSC mwaka 2015, ambao hutakiwa kufanyika kila baada ya
miaka mitatu kwa malengo mbalimbali likiwemo kupitia kanuni, sheria na taratibu
za Tume hiyo.
Akifungua kikao kazi hicho
mjini Dodoma, ameagiza kuwepo kwa ushirikiano baina ya TSC, Idara ya Elimu na
Wadhibiti Ubora wa Elimu (Wakaguzi) ngazi ya wilaya bila kuwepo kwa muingiliano
wa majukumu ili kuinua kiwango cha elimu nchini badala la kuendelea kubishana
na kuingiliana katika majukumu yao.
“Kuanzia sasa naagiza
Maafisa Elimu wa Wilaya wote nchini, Wadhibiti wa Ubora kote nchini na Makatibu
wa Tume ya Utumishi wa Walimu katika Halmashauri zote nchini; kwamba
ushirikiano wa kikazi ni jambo la lazima kwenu vinginevyo tutaendelea
kudidimiza Ubora wa Elimu nchini”
Mhe. Kakunda amewaasa
Wajumbe wa Mkutano huo kuendeleza mafanikio ambayo Tume mpya ya TSC imeyapata
kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja kama kusimamia vema mikataba ya ajira za
waalimu wanapoanza kazi, kwani ndio maisha yao.
“Mnapowasainisha mikataba
ya kudumu ya kazi walimu wapya yenye masharti ya pensheni, tambueni kwamba,
walimu wanaithamini sana mikataba hiyo kwa sababu licha ya kuhakikishia walimu
uhakika wa ajira, mikataba hiyo huwaongoza walimu jinsi wanavyotakiwa
kujiheshimu kazini ikiwa ni pamoja na kuainisha baadhi ya maadili yao kazi”
Aidha, amewataka wajumbe
kutumia kanuni ya kuwathibitisha walimu kazini ndani ya mwaka mmoja bila
kusubiri malalamiko ya walimu. “walimu wote wanaotimiza masharti yanayoonesha
kuwa wameweza kutekeleza majukumu yao kwa ustadi na weledi unaotakiwa,
wathibitisheni kazini ndani ya muda usiozidi miezi 12”,
Katika hatua nyingine, Mhe.
Kakunda ameiagiza TSC kuwachukulia hatua wale wote watakaochelewesha
kuwathibitisha walimu bila sababu za msingi, “nataka kuona hatua hatua
zikichukuliwa dhidi ya wote ambao kwa namna moja au nyingine watachelewesha
kuwathibitisha kazini walimu kwa muda mrefu bila sababu za msingi”
Pia amewaasa wajumbe
kusimamia vema suala la kuwapandisha madaraja walimu kwa mujibu wa kanuni ili
kuondoa malalamiko na manung’uniko na kuongeza ufanisi wa kazi.
Lakini pia, Mhe. Kakunda
ameshauri Kitengo cha Sheria katika Tume ya TSC Makao Makuu iwe Kurugenzi ya
Sheria (Idara kamili) kutokana na umuhimu wa kazi za Tume kama Mamlaka ya
Nidhamu.
Naye Katibu Tume ya
Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Winfrida Rutaindurwa,
amesema Tume hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tangu
kuanzishwa kwake, kwa sheria namba 25 ya mwaka 2015, ikiwa ni pamoja na kuandaa
Mpango Mkakati wa Tume kwa miaka mitano 2017/18 hadi 2021/22, kufunga mtambo wa
malipo ya mishahara na upatikanaji wa taarifa muhimu za watumishi kwa wakati.
Amesema Tume pia imeweza,
“kuandaa bajeti ya matumizi ya kawaida na mishahara wa Tume kwa mwaka
2017/2018, kutengeneza barua pepe za Serikali kwa ajili ya Watumishi wa Tume
Makao makuu, kutengeneza tovuti ya Tume, kujiunga na Mkongo wa Taifa kutoka
TTCL na kuratibu madai ya Watumishi ya likizo, kusafirisha Wastaafu, gharama za
matibabu na posho za kujikimuambayo yaliwasilishwa kwa Mwajiri wa zamani ambayo
ilikuwa ikiitwa Tume ya Utumishi wa Umma”
Rutaindurwa amesema pamoja
na mafanikio zipo baadhi ya changamoto zinazoikabili Tume ya TSC ambazo ni
ufinyu wa bajeti unaopelekea kutofanya uteuzi wa Viongozi wa ngazi ya Wilaya ambao
ni Makatibu Wasaidizi, uhaba wa Ofisi za Tume ngazi ya Makao Makuu na Wilaya,
upungufu wa vitendea kazi na samani Makao makuu na Wilayani.
Changamoto nyingine ni
upungufu wa watumishi unaozorotesha utendaji wa Tume hiyo, “upungufu wa
watumishi wa kada mbalimbali wilayani na makao makuu. Wanaopaswa kuwepo ni
watumishi 775”na waliopo ni 417 na upungufu uliopo ni watumishi 358.
Aidha, amesema baadhi ya
ofisi za TSC katika mikoa na Halmashauri
zisizo na Wakuu wa Wilaya zimeondolewa na kusababisha kupungua kwa ufanisi kwa
ofisi za Tume ngazi ya Makao makuu na wilaya 139, ikiwa ni kutokana na ukosefu
wa usimamizi wa karibu katika ngazi za mikoa.
Rutaindurwa amesema TSC inarajia kukamilisha zoezi la uteuzi
wa Viongozi wa wilaya kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2017/18, kufuatilia
mabadiliko ya muundo wa TSC ili kukidhi mahitaji yake, kutafuta uwezeshaji wa
kuboresha mawasiliano ya kielektroniki makao makuu na wilayani, na pia kuandaa
mazingira ambayo TSC itaongezewa bajeti kwani inahudumia watumishi zaidi ya
asilimia 55 wa Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya TSC, Oliva Mhaiki
amesema, tangu kuanzishwa kwa TSC mwaka 2015 na kuanza kazi mwaka 2016, “Tume ilianza kushughulikia mashauri ya
kawaida, lakini kutokana na wingi wa mashauri, tuliona tuyarudishe wilayani na
kama Tume tumeona tujikite na mashauri ya rufaa”
0 comments:
Post a Comment