WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mwenendo wa
ukuaji wa uchumi wa Taifa unaridhisha, ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka
2017 ulikua kwa asilimia 5.7.
Ameyasema
hayo leo (Ijumaa, Novemba 17, 2017) wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano
wa Tisa wa Bunge, mjini Dodoma.
“Mwenendo
wa uchumi wetu ni wa kuridhisha, mfano, ukuaji wa uchumi katika robo ya kwanza
ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7, robo ya pili ilikuwa asilimia 7.8 na
nusu ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa ni asilimia 6.8.”
Amesema
hali hiyo inafuatia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na usimamizi thabiti wa
matumizi ya Serikali, ambapo nakisi ya bajeti ya Serikali imeshuka na kufikia
asilimia 1.9 kwa mwaka 2016/2017
Pia
amesema akiba ya fedha za kigeni inatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya
nchi kwa zaidi ya kipindi cha miezi mitano, ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi
minne.
Akizungumzia
kuhusu kasi ya upandaji bei, Waziri Mkuu amesema takwimu zinaonyesha kwamba
katika nusu ya mwaka 2017, mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika kiwango cha
tarakimu moja.
“Takwimu
zinaonyesha kwamba mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Oktoba 2017 ulikuwa ni
asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilima 5.3 mwezi Septemba, 2017.”
Amesema
kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa bei wa bidhaa za
vyakula, ambavyo vimepungua kutoka wastani wa asilimia 9.3 mwezi Septemba, 2017
hadi asilimia 8.8 mwezi Oktoba, 2017.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii ianzishe Mamlaka ya
Fukwe za Bahari na Maziwa ili kutangaza na kuendeleza fukwe ambazo hazina
shughuli.
Amesema fukwe za bahari ni eneo mojawapo ambalo likiendelezwa vizuri, linaweza
kuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi, hivyo ni lazima zipewe kipaumbele.
Pia ametoa wito kwa
wizara hiyo iongeze kasi ya kuleta mabadiliko katika sekta nzima ya maliasili
ili iweze kuchangia zaidi kwenye uchumi.
Ametolea mfano Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo imefanikiwa kuongeza mapato kutoka shilingi
bilioni 60.1 mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi bilioni 102 mwaka 2016/2017.
Waziri Mkuu
amesema ongezeko hilo la mapato limekuja baada ya Serikali kuboresha mifumo ya
ukusanyaji wa mapato kwa kutumia njia ya kielektroniki.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P.
980,
DODOMA.
IJUMAA, NOVEMBA 17, 2017.
0 comments:
Post a Comment