METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, November 3, 2017

Mohammed Dewji apongeza jitihada za Rais Magufuli kufufua viwanda


 Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji akizungumza katika mkutano wa Global Business Forum 2017 kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika, mkutano huo wa siku mbili umefanyika Dubai, UAE na kuhudhuriwa na watu 5860 wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wafanyabiashara. (Picha na Clouds Media)

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji amepongeza uamuzi wa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kufufua viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi.
Dewji ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa Global Business Forum 2017 (GBF) kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).
Mfanyabiashara huyo ambaye anamiliki viwanda 41 alisema uamuzi aliochukua Rais Magufuli ni mzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati.

Dewji alisema kampuni yake ya MeTL Group itaendelea kushirikiana na serikali na katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo amejipanga kuhakikisha anatoa ajira kwa Watanzania 100,000 jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa nchi na kwa wananchi..
 “Nianze kwa kumpongeza Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa shabaha yake ya viwanda, ni nzuri sababu kuna ongezeko la thamani lakini pia watu wanaweza kupata ajira na pia hizi biashara zitalipa kodi ambazo zitaisaidia serikali kuwekeza kwenye mambo ya afya na maji na huduma za jamii. Mimi shabaha yangu kwenye miaka saba au nane ijayo MeTL Group tunataka tuajiri watu 100,000,” alisema Dewji.
Dewji ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes ni tajiri namba moja nchini aliongeza kuwa utendaji wa Rais Magufuli ni wa kasi hivyo anategemea kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo uchumi wa Tanzania utakuwa umekuwa  sana.
“Mimi naona kwa kasi ya Mhe. Rais kwenye miaka miwili au mitatu ijayo tutakuwa tumefika mbali sana, uchumi wetu kwasasa ni asilimia sita au saba lakini kama tukitaka kuondoa umaskini lazima nchi yetu ukuaji wa uchumi uanze kukua kwa zaidi ya asimilia 10, mimi nina muamini sana Mhe. Rais na shabaha yake kwahiyo Mungu atutangulie na sisi tupo nyuma yake tutafika hivi karibuni,” alisema Dewji.
Pia Dewji alizungumzia umuhimu wa mkutano wa GBF ambao umekutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wawekezaji alisema ni nafasi ya kipekee kwani pamoja na kujadili viwanda pia amepata nafasi ya kuwaelezea washiriki wa mkutano fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.
“Umuhimu ni mkubwa sana nakuja hapa kama MO lakini pia nawakilisha nchi yangu Tanzania, nimeitangaza nchi yangu ili watu waje na wawekeze, nimewaeleza mazingira yetu ya uwekezaji ni mazuri, tuna malighafi na tunahitaji viwanda angalau watu wetu wa Tanzania wapate ajira na serikali ipate kodi,” aliongeza Dewji.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com